TUME ya Ushindani Tanzania (FCC) sasa ni gumzo sana miongoni mwa wanamichezo wengi na hasa wapenda soka na bahati mbaya sana, wengi hawajui hata imeingiaje huku katika michezo.
Suala la mchakato wa mabadiliko ya Klabu ya Simba linawahusu na hasa katika kuhakikisha mchakato wa mabadiliko unapita katika njia sahihi.
Siku chache zilizopita, Mkurugenzi wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba, Mohammed Dewji aliandika mtandaoni akionyesha kusikitishwa na uamuzi wa FCC kuwataka kuanza mchakato huo wa kwenda katika mabadiliko upya kabisa.
Siku chache baadaye, bosi wa FCC naye akaibuka na kusema hawajawahi kusema mchakato urudiwe upya na mambo yanaendelea na yako ukingoni.
Haya tu mawili yalitosha kuwa sehemu inayowachanganya wadau wa mchezo wa soka hasa wale ambao wana hamu ya kuiona Simba inaingia mabadiliko hayo.
Simba kutoka klabu ya wanachama pekee, kwenda kuwa klabu ya wanachama na yenye hisa kwa maana ya kuendeshwa kibiashara zaidi na kutoa nafasi ya kuingiza wataalamu kadha wa kadha kama masoko na mengineyo.
Tayari Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa ameeleza namna atakavyolisimamia suala hilo kuhakikisha pande hizo mbili za FCC na Simba zitakavyokutana na kulisimamia hilo kupata mwafaka.
Wakati niliposikia FCC wamesema mchakato uanze upya kabisa, ilinishangaza sana. Niliamini haiwezekani Simba wakawa wamekosea kila sehemu ya mabadiliko yake na badala yake, FCC ingetuma wataalamu kuungana na kamati iliyosimamia mchakato huo wa mabadiliko, kubadilisha kila sehemu wanayoona ilikuwa na upungufu.
Haiwezekani Simba wawe wamekosea kila kitu katika mchakato wao kwa kuwa walitumia magwiji mbalimbali kutoka katika tasnia kadha wa kadha ikiwemo ya sheria, ambako walikuwemo baadhi ya magwiji.
Kusema kila kitu kirudiwe, lingekuwa jambo linaloonyesha moja kwa moja badala ya nia njema, basi kuna walakini.
FCC ni wataalamu wa kile wanachokitaka Simba na sote tunaungana kwamba hata kama Simba inafanya mabadiliko, basi ni lazima ipite njia sahihi kwa mujibu wa sheria za nchi yetu.
Tunataka kuona Simba inapita katika njia sahihi kufikia hayo mabadiko, ila wengine nao wafuate na kupita katika njia hiyo ili baadaye kuwe na klabu zilizoingia katika mabadiliko na kutengeneza mfumo bora zaidi wa kibiashara.
FCC kwa sasa suala la Simba linawagusa lakini baadaye kidogo litawagusa la Yanga na klabu nyingine ambazo zitalazimika nazo kuingia katika mchakato wa mabadiliko.
Inawezekana kabisa, klabu nyingine hazitapitia njia ndefu kabisa kwa kuwa tayari Simba watakuwa wameonyesha njia kutokana na njia waliyopita. Funzo litakuwa limepatikana na kutakuwa na wepesi katika kufanikisha kwa upande wao.
Hivyo kama FCC wanaona kusema sehemu ina upungufu, basi waishughulikie kwa kuwaonyesha Simba njia sahihi ya kupita badala ya kuacha malumbano yaendelee.
Siku moja historia ya Simba itawahukumu kwa kuonekana waliwahi kukwamisha mchakato wa mabadiliko.
Inawezekana ikawa wanaowahukumu hawako sahihi, au wako sahihi. Kikubwa kwa FCC wanatakiwa kuwa sehemu ya daraja sahihi la mabadiliko na si kuonekana wamekwamisha.
Tayari bosi wao ameshasema hakuna suala la kurudia, lakini hadi kufikia wanakutanishwa na waziri maana yake kulikuwa na tatizo.
Simba nao wanapaswa kuheshimu mchakato sahihi, kama kuna sehemu wanaelekezwa, iko haja ya kufanya utekelezaji ili kufanya mambo yaende kwa
usahihi ili watakaokuja kufuata mchakato huo nao wapitie katika njia sahihi na inayotakiwa.
Ninaamini Simba na FCC watalimaliza hili, wakikutana nia yao itakuwa ni kuhakikisha linafanikiwa na baadaye kuwa dira kwa wengine huku mbele.
0 COMMENTS:
Post a Comment