April 10, 2021


 KAZI namba moja ya kipa duniani ni kuzuia mpira kwa namna yoyote ile usiingie kwenye lango lake ili kulifanya lango liwe salama ndani ya uwanja.

Mbali na kwamba ana ruhusa ya kutumia mikono akiwa eneo lake la kujidai ila haruhusiwa kumchezea faulo mchezaji wa timu pinzani.


Haya hapa makosa manne ambayo yamekuwa yakipoteza tabasamu la kipa namba moja wa Yanga Metacha Mnata.


Bao lake la dakika ya 89 mbele ya Polisi Tanzania lilimfanya apoteze furaha na ilitajwa kwamba mabosi wa Yanga walimpigia simu na kumpa vitisho jambo ambalo lilimfanya ajiweke kando kwa muda kabla ya kurejea tena ndani ya Yanga.


Sasa twende sawa tuone namna mambo yalivyo kwa Mnata namna hii:-


Mwendo wake

Amekaa langoni kwenye jumla ya mechi 20 kati ya 23. Ana jumla ya clean sheet 11 ambazo amekusanya ndani ya kikosi cha Yanga msimu wa 2020/21. Mechi tisa ameokota mabao kwenye nyavu zake ndani ya uwanja.


Clean sheet

Clean sheet za Mnata zipo namna hii:-Yanga 1-0 Mbeya City, Kagera Sugar 0-1 Yanga, Mtibwa Sugar 0-1 Yanga, Yanga 3-0 Coastal Union, Yanga 1-0 Polisi Tanzania, Biashara 0-1 Yanga, Gwambina 0-0 Yanga, Azam 0-1 Yanga, Yanga 1-0 JKT Tanzania, Mwadui 0-5 Yanga, Ihefu 0-3 Yanga.


Alitunguliwa


Hizi hapa alitunguliwa ilikuwa mbele ya Tanzania Prisons 1-1 Yanga, Mbeya City 1-1 Yanga, Kagera Sugar 3-3 Yanga, Yanga 3-1 Dodoma Jiji, Yanga 2-1 Ruvu Shooting, Yanga 1-1 Simba, Yanga 1-1 NamungoKMC 1-2 Yanga, Polisi Tanzania 1-1 Yanga.

Makosa yake ilikuwa namna hii:-


Kupanga ukuta


Moja ya jukumu la kipa ni kuhakikisha kwamba anaunganisha ukuta wakati wa mipira ya adhabu ikiwa ni kona pamoja na faulo inapopigwa kwenda upande wa lango lake ili kuwa salama.


Imekuwa ngumu kwa Mnata kutimiza jukumu hili kwa kuwa amekuwa akitunguliwa kwa mipira ambayo inatokana na mipira iliyokufa.


Uwanja wa Nelson Mandela , wakati ubao ukisoma Tanzania Prisons 1-1 Yanga alitunguliwa bao dakika ya 51 na Jeremiah Elifadhili kwa mpira wa adhabu uliopigwa nje ya 18.


Uwanja wa Sheikh Amri Abeid pia alifungwa bao la mtindo huo baada ya kushindwa kuokoa mpira ambao ulizamishwa kwa kichwa cha Pius Buswita langoni mwake.


Alifungwa bao moja lililotokana na kona mbele ya Kagera Sugar. Pia mbele ya Simba , Uwanja wa Mkapa.


Mapigo ya penalti


Licha ya kwamba aliweza kuokoa penalti moja kwenye mchezo dhidi ya Namungo FC alikwama kuokoa penalti, Uwanja wa Sokoine wakati ubao uliposoma Mbeya City 1-1 Yanga.


Mahesabu, (Timing)

Mnata amekuwa akikwama kwenye mahesabu wakati timu yake ikiwa inashambuliwa. Mchezo dhidi ya Kagera Sugar wakati akiokota nyavuni mabao matatu bao la kwanza na la pili aliyumbishwa na mfungaji na kushindwa kuwa na chaguo la sehemu sahihi kuokoa mabao hilo.


Punching, (Okoa kwa ngumi)

Kanuni namba moja kwa makipa katika kuokoa kwa ngumi ni lazima mpira utoke nje ya 18. Imekuwa tatizo pia kwa Mnata ukirejea bao alilotunguliwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mbele ya Dodoma Jiji.

Alichokuwa anakifanya ni yeye mwenyewe ambaye anajua kwa kuwa aliokoa ndani ya 18 bila akadhani mfungaji yupo mbali akamtungua kwa kichwa alikuwa ni Seif Rashid.

Championi Jumamosi liliweza kuzungumza na kocha wa makipa, Mfaume Athuman ambaye yupo ndani ya kikosi cha Dodoma Jiji aliweza kuweka wazi kuwa makosa ya makipa wengi ikiwa ni pamoja na Mnata, Kakolanya, Manula ni kushindwa kuwa na timing jambo linalowafanya waruhusu mabao.

“Jambo la kwanza ni timing, kipa ana kazi ya kuweza kujua ni wakati upi anapaswa kuruka na upande upi kwa kumtazama mpigaji na kujua uelekeo sahihi.

“Jambo la pili makipa wengi huwa wanafungwa kwa krosi. Ili uwe kipa mzuri ni lazima uwe na uwezo wa kuokoa krosi.

“Kujiamini muda mwingine imekuwa ni tatizo na hilo linawaponza wengi. Jambo hilo linapelekea washindwe kujua uelekeo upi ambao mshambuliaji anapenda kwenda,” anamaliza. 


1 COMMENTS:

  1. Timu ni kama mnyonyoro. Ni lažima vipigili vyote viwe vižuri. Ikiwa vipigili vingi legelege kipa peke yake asilaumiwe

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic