April 20, 2021

 


MTIBWA Sugar imeshinda mechi sita tu kati ya 24 walizoshuka dimbani hadi sasa, ikiwa imepoteza mechi 12 na imetoa sare mechi sita, Mtibwa Sugar pia imeondoshwa kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho la Azam.

 

Msimu uliopita Mtibwa Sugar iliponea chupuchupu kushuka daraja baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Ruvu Shooting kwenye mchezo wa mwisho wa kumaliza msimu wa 2019/20.

 

Mtibwa Sugar imekuwa na muendelezo wa matokeo yasiyoridhisha kwa msimu wa tatu mfululizo, tangu kuondoka kwa aliyekuwa kocha mkuu wa timu hiyo Mecky Maxime na baadaye Zubeir Katwila timu hiyo imekuwa na mwendo wa kinyonga kwenye Ligi Kuu Bara.

 

Kwa miaka mingi Toto Africa ilikuwa na mwenendo kama walionao Mtibwa Sugar hivi sasa na sasa Toto imepotea kabisa kwenye ramani ya soka inashiriki Ligi ya Mabingwa wa Mikoa ambako pia haifanyi vizuri.

 

Mtibwa Sugar wamefunga mabao tisa tu kwenye mechi 24 huku wakiruhusu nyavu zao kutikiswa mara 23, kwa mwenendo huu sioni Mtibwa ikinusurika na janga la kushuka daraja kwenye mechi 10 walizobakisha kumaliza msimu kutokana na presha kubwa ambayo ipo kwenye timu nyingine zikipambana kujiweka kwenye mazingira mazuri pia.

 

Mwezi Januari Mtibwa walimtangaza Hitimana Thierry kuwa kocha mkuu wa timu hiyo akirithi mikoba ya Katwila lakini jambo la kusikitisha Hitimana hakuchukua hata miezi miwili ametimka ndani ya timu hiyo huku sababu kubwa ikitajwa ni kuingiliwa kwenye majukumu yake.

Huu umekuwa ugonjwa sugu kwa timu nyingi nchini kuanzia zile za Kariakoo hadi zile za madaraja ya chini makocha wengi ambao wamekuwa wakipita kwenye baadhi ya timu hizo wamekuwa wakilalamika kuingiliwa majukumu yao na baadhi ya watu wenye sauti ndani ya timu.

 

Inafikia kipindi kocha anapangiwa ni nani aanze na nani akae benchi kwenye mechi husika jambo ambalo kwa kiasi kikubwa ni kinyume na taratibu na si weledi hata kidogo.

 

Huenda ndani ya Mtibwa mambo si mazuri hususan kwenye uongozi jambo ambalo labda ndiyo chanzo cha timu kufanya vibaya kwani ukiangalia kwa ujumla timu haina morali na ari ya upambanaji inazidi kushuka kadri siku zinavyozidi kusonga.

 

Kwa jinsi ratiba ilivyo ni wazi Mtibwa wana mtihani mgumu kukikwepa kikombe cha kushuka daraja kutokana na aina ya timu ambazo wanakwenda kukutana nazo kuwa na shinikizo la kupambana kupata matokeo ili waweze kujinusuru na janga la kushuka daraja pia.

 

Kwa kocha kama Vicent Barnabas ambaye ndiyo anatafuta uzoefu kumpa jukumu la kuivusha timu kwa kipindi hiki ni kumpa jukumu ambalo sidhani kama ataweza kulimudu kikubwa Mtibwa wakae chini haraka iwezekenavyo kupanga mikakati ya kuinusuru timu laa sivyo kuti la mazoea litawaangusha wagema.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic