WATANI wa jadi wanapaswa wajiandae kisaikolojia kutokana na orodha ya waamuzi ambao wataamua mchezo wa Simba v Yanga, Mei 8, Uwanja wa Mkapa.
Emmanuel Mwandembwa wa Arusha ambaye ni mwamuzi wa kati, Novemba 25, Uwanja wa Azam Complex alikuwa ni mwamuzi wa kati na ubao ulisoma Azam FC 0-1 Yanga.
Katika mchezo huo Lamine Moro beki wa Yanga na Nicolas Wadada wa Azam FC walionyeshwa kadi za njano.
Aprili 27, Mwandembwa alikuwa mwamuzi wa kati mchezo wa Simba 3-1 Dodoma Jiji, Mbwana Kibacha na Cleophance Mkandala walionyeshwa kadi za njano hawa ni wachezaji wa Dodoma Jiji, pia wachezaji wa Simba walionekana wakimlalamikia kwa bao ambalo walifungwa kwa madai kwamba Aishi Manula alikuwa amechezewa faulo.
Machi 10, Mwandembwa alikuwa mwamuzi wa kati wakati ubao ukisoma Simba 1-1 Tanzania Prisons, kwenye mchezo huu alifuta bao la Chris Mugalu wa Simba baada ya kudai kwamba alikuwa ameotea.
Pia alitoa penalti moja kwa Simba ambayo ilipigwa na Mugalu huku kipa Jeremia Kisubi akiokoa na kuwa shujaa na alitoa kadi nyekundu kwa beki Jumanne Elifadhili ambaye alimchezea faulo Mzamiru Yassin.
Ni Kassim Mdoe wa Tanzania Prisons yeye alionyeshwa kadi ya njano ambapo Prisons nao walionekana kulalamika bao la Luis Miquissone la kusawazisha kwa madai kwamba nalo alikuwa ameotea.
Wengine ambao atafanya nao kazi ni pamoja na Frank Komba ni mwamuzi msaidizi namba moja, Hamdani Saidi ni mwamuzi msaidizi namba mbili na Ramadhan Kayoko ni mwamuzi wa akiba kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Shirikisho la Soka Tanzania, (TFF).
Ramadhan Kayoko rekodi zinaonyesha kuwa aliwahi kuwa mwamuzi wa kati kwenye mechi ya Ngao ya Jamii iliyowakutanisha Simba na Namungo, Agosti 30, Uwanja wa Sheikh Amri Abeid alitoa penalti moja kwa Simba baada ya nyota Bernard Morrison kuchezewa faulo ndani ya 18 na ilifungwa na John Bocco.
Kwenye mchezo huo alitoa jumla ya kadi mbili za njano ambapo moja alimuonyesha aliyekuwa Kocha Mkuu wa Simba Sven Vandenbroeck na moja mchezaji wa Namungo Steve Duah ambaye alicheza faulo kwa Morrison. Pia alikuwa na Frank Komba ambaye atakuwa naye pia Mei 8.
Rekodi zinaonyesha kuwa kwenye dabi ya Kariakoo, Julai 12 wakati Simba ikishinda mabao 4-1 ambapo mwamuzi wa kati alikuwa ni Kayoko alifanya kazi na Frank Komba ambaye naye pia yupo kwenye orodha Mei 8.
Kayoko pia aliwa kuwa mwamuzi wa mezani Desemba 6, wakati ubao ukisoma Yanga 2-1 Ruvu Shooting.
0 COMMENTS:
Post a Comment