May 8, 2021


VURUGU mechi uwanjani huwa inatokea pale ambapo haki inashindwa kutokea ambapo timu inaposhindwa kupata matokeo mwisho wa siku huwa zinaanza lawama na kazi ya kumtafuta mchawi nani.

 

Kuelekea Mei 8, Uwanja wa Mkapa kwa wale ambao watapewa kibarua cha kuwa wasimamizi wa mchezo huo wanapaswa kuzingatia haki kwa kujali kila idara.

 

Hapa ninazungumzia kuanzia walinzi, waamuzi wa mchezo huo pamoja na mashabiki ambao watajitokeza kushuhudia mchezo huo.

 

Imekuwa ikiripotiwa kwamba wapo baadhi ya Polisi hutumia nguvu kubwa pale mambo yanapokuwa tofauti. Hii nayo imekuwa ikichangia kwa kiasi kikubwa mashabiki kuhofia kwenda uwanjani.

 

Kwa hali hii ikiendelea itazidi kufanya mashabiki wapungue kwenye mechi kubwa ambazo zitakuwa zinawahusu Simba na Yanga.

 

Waamuzi ambao watapewa kazi ya kusimamia mchezo huu nina amini kwamba jukumu lao wanalitambua kwa uzuri. Muhimu kuingia uwanjani na kutimiza sheria 17, hakuna jambo jingine.

 

Kumekuwa na hofu wakati mwingine katika kufanya maamuzi ambapo wapo ambao wanapepesa macho na kufanya jambo ambalo ni nje ya sheria 17 za uwanjani.

 

Hili halipendezi kwa kuwa maamuzi ambayo hayafuati sheria ni maumivu kwa wale ambao watakuwa wamekutana na rungu hilo kwa wakati huo.

 

Kwa wachezaji nao wana kazi ya kutimiza majukumu yao huku kazi kubwa ikiwa ni kutafuta matokeo chanya. Hii itawafanya waweze kufikia malengo yao kwa muda huu ambapo timu zote zinasaka pointi tatu.

 

Ili uweze kupata pointi tatu ni lazima ushinde hakuna namna nyingine ya kufanya ni hiyo tu na kazi ni kwenu kutimiza majukumu ambayo mmepewa na benchi la ufundi.

 

Pia ikumbukwe yale matendo ya ubabeubabe yawekwe kando kwani imekuwa ikionekana kwamba mechi hizi ubabe unakuwa mkubwa kuliko weledi.

 

Yale masuala ya Pascal Wawa kumkanyanga Ditram Nchimbi, Clatous Chama kumkanyanga Fei Salum yasiwepo kwa kuwa kuna suala la kuomba msamaha yasiwepo kabisa.

 

Pia ikumbukwe kwamba kuna mchezo mmoja wa Simba na Yanga, mchezaji wa Simba alitemewa mate usoni, hili sio jambo la uungwana ni lazima kwa sasa kila timu icheze kwa nidhamu kwenye kusaka ushindi.

 

Mpira ukiwa ni wa burudani katika kusaka ushindi utasaidia kuweza kumpata mshindi wa haki ambaye atatoa taswira ya bingwa wa ligi ajaye.

 

Kila timu ina nafasi ya kushinda mchezo huo ujao ikiwa itafanya mambo makubwa mawili ambayo ni nidhamu pamoja na jitihada isiyo kuwa ya kawaida.

 

Kupitia nidhamu nje ya uwanja na ndani ya uwanja itawafanya waweze kupata matokeo mazuri na hilo lipo mikononi mwa wachezaji wenyewe ambao wanatambua wajibu wao.

 

Kwa waamuzi ikitokea ni penalti basi wahusika wapewe kama ni faulo pia acha ipigwe tu bila kupepesa macho. Kwa kufanya hivyo kutaongeza ile nguvu na ari ya upambanaji.

 

Itapendeza ikiwa waamuzi hawatatepesa macho watachezesha kwa umakini katika kusimamia matokeo ambayo yatapatikana na hili linawezekana.

 

Ukiachana na mchezo wa ligi wa Simba dhidi ya Yanga, Uwanja wa Mkapa bado ni lala salama kwenye Ligi Kuu Bara, Ligi Daraja la Pili, Ligi ya Wanawake ambayo imekuwa na ushindani mkubwa.

 

Ukiweka kando suala la Simba na Yanga bado kuna suala la kushuka daraja kwa timu ambazo zinashiriki Ligi Kuu Bara, Ligi Daraja la Kwanza.

 

Hapa kuna jambo ambalo Shirikisho la Soka Tanzania, (TFF) inapaswa ilifanye kwa kuboresha maisha ya timu hizi ili kuongeza ushindani.

 

    Kama ambavyo kwenye ligi kuu umetengenezwa mfumo mzuri wa kuwa na mechi za nyumbani na ugenini pamoja na kuwa na timu 16 ambazo zitakuwa msimu ujao basi na huku pia kuwe na mfumo mzuri.

 

Ikiwa mtindo wa makundi utaachwa na huku pia ikawa ni ligi ambayo haina makundi itaongeza pia ushindani kwa kuwa kila timu itakuwa katika kazi ya kusaka ushindi na kuonyesha ule uwezo wake.

 

Kumekuwa na sera kubwa ya kuepuka vilio kwenye mechi zao kwani wengi wamekuwa wakilia na suala la maamuzi ndani ya uwanja.

 

Muhimu kuboresha mfumo wa kuendesha Ligi Daraja la Kwanza na kuwafanya wachezaji wawe huru pia katika kazi zao bila kuingiliwa na waamuzi ambao wamekuwa wakiharibu ile ladha ya soka.

 

Kila kitu kinawezekana kikubwa kwa sasa ni kujipanga upya kwa timu ambazo zinapambana kushuka na zile zinazopambana kupanda kuweza kufikia mafanikio yao.  

 

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic