May 28, 2021


UNAWEZA kusema uamuzi wa Azam Media Limited kumwaga mabilioni ya fedha katika 
Ligi Kuu Bara ni wa kibiashara, lakini si vibaya kusema ni imani kubwa inayohitaji mapenzi ya dhati kuuamini mpira kukubali kufanya hivyo.


Kampuni hiyo ya masuala ya habari imeandika rekodi kwa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kufikia uamuzi huo ambao sasa unaufanya mpira wa Tanzania kuwa na thamani kubwa.


Azam Media imemwaga kitita cha Sh bilioni 225.6 katika Ligi Kuu Bara huku bingwa akitengewa zawadi ya Sh milioni 500, hii ni rekodi.


Hakuna tena anayeweza kuinua mdomo na kusema mpira ni burudani pekee. Jambo ambalo binafsi nimelisema kwa zaidi ya miaka 10 kuwasisitiza wadau kuwa hii ni biashara kubwa.


Soka ni biashara kubwa na inapaswa kupewa heshima ya kiwango cha juu badala ya watu kuwa wanaamini ni sehemu ya kwenda kujiburudisha pekee, hivyo kuyachukulia mambo yake kimzahamzaha.



Wako wanaweza wakafanya hivyo na hasa mashabiki lakini hata wao wanapaswa kuonyesha heshima kubwa kwa mchezo wa mpira. Watu wanapofikia kuwekeza kiasi kikubwa hicho cha fedha, maana yake wamewaamini wadau wa mchezo huo na kuwapa heshima kubwa, basi lazima nao wairudishe heshima hiyo kwa wale ambao wamewaonyesha heshima.


Bila ya ubishi, Azam Media Limited wameonyesha heshima kubwa kwa wachezaji, makocha, viongozi lakini pia mashabiki na wadau wengine wa mpira kwamba wanawaamini na ndio maana wameamua kuwekeza fedha nyingi kiasi hicho kwa kuwa sehemu wanayowekeza ni salama.


Sasa ili kulithibitisha hilo, wadau wana deni kubwa kuwaonyesha Azam Media kwamba walichofanya ni kitu sahihi na hawana sababu ya kuwa na hofu hata kidogo.

Watafanyaje hivyo, ni kufanya mambo kama yanavyotakiwa kwa kufuata usahihi na kuendelea kuupa heshima mpira wa Tanzania ili wadau zaidi na zaidi wazidi kujitokeza wakifuata mwendo wa Azam Media.


Ukianza na wachezaji, wacheze mpira hasa, mpira wa kiwango bora na sahihi. Kiwango ambacho kitawafanya Azam Media waone walichokitoa kilistahili kufika walipokipeleka na wao watarudisha faida na heshima yao.


Unapojua thamani ya Ligi Kuu Bara imepanda na wewe ni kati ya wachezaji ambao wanachezea katika moja ya vikosi vya ligi hiyo. Basi ni vizuri angalau kuonyesha thamani yako kuwa na wewe imepanda kwa kucheza kwa kujituma, kutoa upinzani sahihi wa kiushindani badala ya kubaki kama vile ile ligi kuu ambayo haikuwa na thamani iliyopo sasa.


Kuingia kwa Azam Media kutazifaidisha klabu katika mengi kama mgawo lakini zawadi pia ambazo inaweza kushinda timu yoyote lakini unaona hadi mshindi wa tano na kuendelea bado ana zawadi kubwa tu, hili si jambo dogo.


Achana na kubadilisha nia na aina ya utumishi kwa maana ya hadhi ya ulipo. Lakini nawakumbusha wachezaji kuachana na tabia ovu, zile tabia za kutumiwa na baadhi ya viongozi au wadau wengine kwa kupokea fedha ili kuiumiza timu yako.


Kama kutakuwa na kesi za mambo hayo, hata kama yanafanyika kwa siri kwa kuwa watoaji na wapokeaji hufurahia pamoja lakini kuna siku atakamwatwa mtu. 

Hii itawafanya wadhamini walioingiza fedha zao kwa wingi kama Azam Media kukata tamaa. Maana yangu ni hivi, lazima kuendelea kuonyesha thamani ya ligi hiyo kwa kufuata weledi na kuhakikisha mpira unachezwa kwa kufuata sheria 17 pamoja na Fair Play.


Hakuna kinachoshindikana, hakuna kisichowezekana lakini lazima kuwe na hisia na uhalisia ndani ya vichwa vyenu kwamba mafanikio na mwenendo bora umechangia Azam Media kujitokeza na kuongeza dau.

Maana yake, juhudi za namna hiyo zipewe nafasi ili kuwashawishi wengine na siku moja bingwa apewe Sh bilioni moja.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic