HAKUNA ambaye alitarajia kwamba inaweza kutokea kama ilivyotokea na mwisho wa siku imetokea na hauwezi kubadili jambo la nyuma zaidi unapaswa kuangalia ni jambo gani waweza kufanya kwa wakati ujao ili uwe imara na bora.
Wengi wamezungumza kuhusu mchezo wa Simba na Yanga ambao ulipaswa kuchezwa Mei 8, Uwanja wa Mkapa saa 11:00 jioni ila masaa machache kabla ya mchezo ulipelekwa mbele baada ya Shirikisho la Soka Tanzania, (TFF) kueleza kwamba mchezo huo utachezwa saa 1:00 usiku hapo ndipo tatizo lilianzia.
Yanga waliweka wazi kwamba watapeleka timu muda uliopangwa
awali kwa kuwa mabadiliko yamefanywa kinyume na kanuni ya 15, (10) ambayo
inasema:”Mabadiliko yoyote ya muda wa kuanza mchezo yatajulishwa ipasavyo kwa
pande zote husika za mchezo angalau saa 24 kabla ya muda wa awali,” . Hapo
ndipo ambapo waliamua kusimamia Yanga.
Yote kwa yote imani yangu ni kwamba yaliyotokea yatafanyiwa
kazi kwa kuwa wahusika na mamlaka zinajua namna ambavyo hali ilikuwa pamoja na
vurugu ambazo zilianza kutokea .
Kikubwa ambacho leo ninahitaji kuongea ni kuhusu wawakilishi
wa Tanzania kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika ambao ni Simba.
Kibarua chao kikubwa mbele yao ni mchezo wao wa kwanza wa
hatua ya robo fainali dhidi ya Kaizer Chief ambao unatarajiwa kuchezwa Mei 15
na ule wa marudio unatarajiwa kuchezwa Mei 22.
Hapo sasa kwa Simba kilichotokea kwa Mkapa kisiwaondoe kwenye
reli kwa sababu bado kuna jambo la kufanya kwa ajili ya taifa la Tanzania.
Katika kuwakilisha nchi ni muhimu kwenda na nguvu mpya na
kufanya juhudi kusaka ushindi kwenye mchezo huo ambao ushindani wake utakuwa
mkubwa.
Msiwadharau wapinzani wenu kwani nao wanahitaji ushindi
jambo pekee ambalo mnatakiwa kulifanya ni kuingia uwanjani kwa nidhamu na
kutimiza majukumu yenu bila kuogopa dakika zote 90.
Leo nina amini kwamba mtaendelea na maandalizi ya mchezo wenu Afrika Kusini,
basi mawazo ya kutochezwa kwa mechi yenu dhidi ya Yanga kusiwafanye mkaboronga
mchezo wenu ujao.
Wahenga walisema kwamba yaliyopita si ndwele nasi tugange
yajayo, kila la kheri wawakilishi wetu na tunaamini kwamba mtafanya vizuri.
Mamlaka imeeleza kuwa mchezo huo utapangiwa tarehe itakayochezwa hivyo muhimu kuwa na subira kwa sasa.
0 COMMENTS:
Post a Comment