KUELEKEA mchezo wao wa leo dhidi ya KMC, mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara klabu ya Simba wanatarajiwa kupata ahueni kufuatia kukosekana kwa mlinzi nyota wa KMC, Bryson David anayesumbuliwa na majeraha ya nyama za paja.
Bryson ambaye amekuwa katika kiwango bora msimu huu kiasi cha kutajwa kuwa kwenye rada za kusajiliwa ndani ya kikosi cha Yanga, amekosa mazoezi ya pamoja ya KMC kujiandaa na mchezo dhidi ya Simba, mchezo utakaochezwa kwenye uwanja wa Mkapa Dar es Salaam.
KMC imeingia katika mchezo wa leo ikiwa na kumbukumbu ya kupoteza mchezo wao wa mzunguko wa kwanza mbele ya Simba, baada ya kukubali kipigo cha bao 1-0, mchezo uliopigwa Desemba 16, mwaka jana.
Akizungumzia maandalizi yao Ofisa habari wa KMC, Christina Mwagala alisema: “Mchezaji wetu Bryson
David bado ana changamoto ya majeraha ya nyama za paja, ambayo yamemfanya
akosekane kwenye mazoezi ya pamoja kujiandaa na mchezo dhidi ya Simba.
“Lakini hatuna shaka kwani, tunao wachezaji wengine ambao wanaweza kuziba pengo lake na kukamilisha lengo letu la kumaliza kwenye nafasi za juu za msimamo.”
0 COMMENTS:
Post a Comment