Saleh Ally
MARA ya
mwisho Yanga ilibeba ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara katika msimu wa 2016/17
ikiwa imelingana kabisa pointi na watani wao wa jadi, Simba.
Yanga
ilifikisha pointi 68 sawa na Simba, lakini tofauti ya mabao ya kufunga, Yanga
ikiwa na GD ya 43 baada ya kufunga mabao 57 na kufungwa 14, Simba ikiwa na GD
ya 33 baada ya kufunga 50 na kuruhusu 17.
Kama
unakumbuka, msimu huu ndio wafungaji bora walikuwa wawili baada ya Saimon Msuva
wa Yanga na Abdulrahman Mussa wa Ruvu Shooting kufungana kila mmoja akiwa na
mabao 14.
Baada ya
hapo, sasa ni misimu minne mfululizo, Simba imebeba kombe hilo kubwa zaidi
katika mchezo wa soka nchini.
Msimu
uliofuata wa 2017/18, Simba ilimaliza bingwa baada ya kukusanya pointi 69, Azam
FC wakafuatiwa wakiwa na 58 huku Yanga wakimaliza katika nafasi ya tatu wakiwa
na pointi 52.
Mfungaji
bora msimu huu akawa ni Emmanuel Okwi wa Simba akiwa na mabao 20, akafuatiwa na
John Bocco wa Simba akiwa na mabao 14 sawa na Marcel Bonaventura Kaheza wa
Majimaji ambaye alikuwa mali ya Simba, akiwa huko kwa mkopo.
Msimu wa
2018/19, Simba wakawa mabingwa kwa mara ya pili mfululizo, safari hii wakiweka
rekodi ya kukusanya pointi 93, Yanga nao walikuwa vizuri, wakawasogelea wakiwa
na pointi 86 katika nafasi ya pili huku Azam FC wakiwa na pointi 75 katika
nafasi ya tatu.
Simba
wakafunga mabao 77, wakafuatiwa na Yanga wenye 56 na Azam FC katika nafasi ya
tatu wakiwa na mabao 54.
Mfungaji
bora akawa Meddie Kagere wa Simba akiwa na mabao 23, akafuatiwa na Salim Aiyee
wa Mwadui FC aliyetupia 18, halafu Heritier Makambo wa Yanga aliyetupia mabao
17.
Msimu wa
2019/20, Simba ikabeba ubingwa kwa mara ya tatu mfululizo, yaani hat trick na
kulibeba kombe moja kwa moja. Safari hii Simba ikaandika pointi 88 hadi mwisho
wa msimu, ikifuatiwa na Yanga iliyokuwa na 72 na Azam FC tena katika nafasi ya
tatu wakiwa na pointi 70.
Mfungaji
bora wa msimu akawa Kagere tena akiwa na mabao 22, akifuatiwa na Yusuf Mhilu wa
Kagera Sugar aliyekuwa na mabao 13 sawa na Waziri Junior wa Mbao FC.
Katika
misimu hii mitatu, Simba imetwaa mataji ya ubingwa mfululizo, wafungaji bora
mfululizo na fowadi na beki kali mara zote mfululizo.
Huu ndio
msimu wa nne, yaani 2020/21, Simba tayari ni mabingwa wakiwa na pointi 76
lakini wana mechi tatu mkononi na ndio timu pekee yenye uwezo wa kufikisha
pointi 80 au zaidi. Simba wana mabao mengi zaidi ya kufunga na safu ngumu zaidi
kwa maana ya kuruhusu mabao. Kimoja tu wamezidiwa na Yanga ambao wamepoteza
mechi mbili za ligi na Simba wamepoteza tatu.
Yanga
angalau washinde mechi moja kujihakikishia kushika nafasi ya pili ili waweze
kupata nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa ingawa pia wanaweza kuipata
kama watawafunga Simba katika fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam Julai 25
kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma.
Utawala huu
wa Simba ni wa takwimu na ndio uhalisia, hapa unaachana na sifa za kishabiki na
unaangalia kuna jambo kubwa sana la kujifunza.
Kwani wakati
Simba inabeba ubingwa, ina nafasi kubwa sana ya kuibuka na mfungaji bora tena
kwa mara ya nne mfululizo pia. Utaona ilikuwa Okwi, akafuatia Kagere mara mbili
na sasa inaonekana atakuwa Bocco, Chris Mugalu au Kagere kama hawatatibuliwa na
Prince Dube wa Azam FC.
Wakati Dube
ana mabao 14 sawa na Bocco, Mugalu ana 12 na Kagere ana 11. Utaziona hizi mbio
zilivyo na unaona Simba walivyo na nafasi ya kuchukua ubingwa mara nne na taji
la mfungaji bora mara nne. Wengine wako wapi na wanafanya nini?
Nilitaka
kuwakumbusha kwamba kuna jambo timu nyingine zinapaswa kujifunza kupitia Simba
badala ya kutaka kuonyesha wanabahatisha au kupendelewa.
Haiwezekani
Simba wakapendelewa kwa misimu minne mfululizo, ukiachana na ubingwa wakawa na
safu bora ya ulinzi, safu bora ya ushambuliaji. Wakatwaa tuzo ya mfungaji bora
misimu mitatu mfululizo, tukiwatarajia na wanne, wana jambo linaweza kuwa shule
kwa timu nyingine.
Simba
wamejipanga, wanafanya mambo yao kwa mpangilio na hata usajili wao umepangiliwa
na kuna mambo wanafanya yanakwenda kwa utaratibu.
Tumeona,
hata kimataifa wao ndio wamekuwa gumzo na kuitangaza Tanzania kwa kiasi kikubwa
ukiachana na uchangiaji wao wa pointi nyingi zaidi Tanzania kupata timu nne
zitakazoshiriki michuano ya klabu ya CAF kwa maana ya Ligi ya Mabingwa Afrika
na Kombe la Shirikisho Afrika.
Hata kama si
kuiga kila jambo lao, kuna nafasi ya kujifunza na kuangalia namna nyingine
ambayo itazisogeza timu katika ubora sahihi na baadaye ziwe washindani sahihi
wa Simba.
Maana kila
wakichukua ubingwa, pengo la pointi linakuwa kubwa. Wafungaji wao wanakuwa bora
kama ilivyo safu ya ushambulizi lakini tuliona hata alipoondoka Okwi, wengi
waliamini Simba watayumba, leo ubora wao ni zaidi ya wa msimu ule Okwi
akiondoka. Na umekuwa ukizidi kupanda na kuwafanya wawe gumzo zaidi.
Uchezaji wa
Simba, leo imefikia hakuna anayeweza kubisha kuhusiana na ubora wao, akikataa
itakuwa mdomoni lakini ndani ya nafsi yake, anajua anachokiwaza.
Tukubali,
walipofikia Simba haiwezi kuwa maombi tu na majaaliwa tu. Kuna matumizi makubwa
ya akili, ushirikiano na umoja unaofanya haya yafikiwe. Acheni kujimwambafai,
jifunzeni la sivyo, Simba wataendelea kutawala tena na tena.
Utopolo jifunzeni kwa waliofanikiwa co mnakalia majungu tu na kubeza kusikokuwa na tija
ReplyDeleteNi kweli kabisa,takwimu zinaongea.
ReplyDeleteHuna jipya wachambuzi walopoteza mwelekeo endeleeni kutumika jana manara kasema acheni ushabiki fateni taaluma yenu simba bora kwa watoto wenzake huko sio kwa yanga ndio maana hatuumii tunajuwa wanapataje ubingwa na wanakosa furaha kama unabisha weka ligi ya timu nne ruvu yanga simba na prison tupate bingwa kama atashinda
ReplyDelete