GANZI ilitawala Julai 10 2019 baada ya taarifa za aliyekuwa mwandishi chipukizi kwenye masuala ya michezo katika Kampuni ya Global Group, Ibrahim Mressy kueleza kwamba amefikiwa na umauti.
Ilikuwa ni ghafla kwa kuwa hata kuumwa kwake ilikuwa ni ghafla ila mwisho wa siku kazi ya Mungu haina makosa, tunakuombea kheri ndugu yetu.
Leo Championi Jumamosi inakuletea mambo 10 ambayo alikuwa anapenda kuyafanya Mressy enzi za uhai wake:-
Ibrahim Mressy
Ibada
Ni chaguo namba moja kwake katika yale ambayo alikuwa anafanya. Hili nilikuwa naliona kwake kipindi chote kazi na ilikuwa ikijidhihirisha wakati wa kipindi cha mfungo. Funga zote alikuwa anafuata hakuwa kobe kwenye kutimiza zile nguzo tano za dini yake kwa kuwa alikuwa ni Muislam.
Mressy alikuwa ananiambia nami nifunge ili nipate thawabu nilikuwa namzingua kwamba nimefunga mwisho wa siku ananinunulia futari maisha yanaendelea.
Tabasamu
Sijabahatika kumuona akiwa kwenye hasira licha ya kwamba nilikuwa mkorofi katika kumkasirisha kila wakati nikipata muda.
Nakumbuka niliripoti kwa mhariri wa gazeti la Championi Jumamosi zama hizo na kwa sasa anasimamia gazeti la Championi Jumatano kuhusu Mressy kugandamizia stori yangu. Hakuwa na chaguo la kufanya zaidi ya kuishia kutabasamu kisha akasema:”Kwamba bob Dizo unahitaji stori yako, mbona fresh tu”.
Chakula
Hapa alikuwa sio mvungaji wala mtegeaji kwenye suala la chakula.Hata kama hajamaliza kazi zake ikifika muda wa kula lazima afuate chakula. Ilikuwa ni wali maharage chakula chake pendwa na wakati mwingine alikuwa anapenda kula Chipsi yai pembeni ni soda ilikuwa inahusika.
Kazi
Ni mwandishi ambaye alipewa jukumu la kuanza kunifundisha kazi. Gazeti la kwanza mimi wakati naingia Global Group lilikuwa ni Championi Jumatano na ninakumbuka tulikuwa pale makao makuu ya Shirikisho la Soka Tanzania, (TFF).
Hakuwa akipenda kuona ninakwama kuandika stori kwa namna yoyote na alikuwa anajua kuandika stori. Kuna wakati alikuwa ni mwandishi tegemeo wa habari za burudani kwa magazeti pendwa. Huku alikuwa akiandika masuala ya burudani na bado alikuwa anafanya vizuri licha ya kwamba alikuwa kwenye habari za michezo.
Kusaidia wengine
Ilikuwa ni ngumu kwake kufanya hivyo kwa wakati ule kwani hakuwa na uwezo wa kutengeneza mkwanja mrefu wa kuweza kutoa sapoti kwa wengine ila hakuwa mchoyo.
Kila wakati alikuwa ananiambia namna ambavyo anapenda kuona ndugu zake pamoja na marafiki zake wakipata matunda ya kile ambacho anakitengeneza licha ya kwamba ni kidogo.
“Dizo eh unaona hiki nilichopata kimahesabu ni cha kishkaji lakini ni lazima tugawane na ndugu zangu, halafu sijui nani huwa anawaambia kwamba mimi muda Fulani nipata hela maana nikipewa tu mkwanja naanza kupokea simu zao,”
Muziki
Ni wimbo wa Inatosha wa Marioo ulikuwa ni pendwa kwake pamoja na ule wa Chibonge. Kwa upande wa msanii ambaye alikuwa anampenda alikuwa ni Ali Kiba ila hakuwahi kasirikia kazi za Diamond kwani alikuwa anapenda ngoma zake pia.
Matunda
Tikitimaji ilikuwa ni tunda lake pendwa pamoja na ndizi pale anapopata muda wa kula matunda.
Utani
Alikuwa ni mtu wa utani muda mwingi jambo ambalo lilimfanya awe na marafiki wengi kila mahali.
Mpira
Timu yake mbele ni Barcelona na mchezaji wake aliyekuwa anampenda alikuwa ni Lionel Messi kisa jina lake la pili linafanana na jina lake.
Pia alikuwa anapenda kucheza mpira na kwenye matukio yote ya mpira alikuwa anahusika kwa asilimia 100 bila kukosa.
Kupumzika
Ibra aliniambia kati ya vitu ambavyo huwa vinampa shida ni kusumbuliwa siku yake ya mapumziko ambayo ilikuwa ni Jumatatu.
“Jumatatu kuna watu huwa wananisumbua kweli nami sipendi ninapenda kupumzika, ikifika muda wa kupumzika mara nyingi huwa ninazima simu,”alikuwa akiniambia enzi za uhai wake .
Yote kheri, pumzika kwa amani rafiki yetu, mshikaji wetu kipenzi cha watu, Amen.
Na: Lunyamadzo Mlyuka
GANZI ilitawala Julai 10 2019 baada ya taarifa za aliyekuwa mwandishi chipukizi kwenye masuala ya michezo katika Kampuni ya Global Group, Ibrahim Mressy kueleza kwamba "amefikiwa na umauti"
ReplyDeleteHii sentensi sijaielewa.