July 10, 2021


BERNARD Morrison, mchezaji ambaye alitajwa kuwa na matukio mengi ya utovu wa kinidhamu wakati akiichezea Yanga, leo hii amekuwa na faida kubwa kwa Simba.

 

Tangu kiungo mshambuliaji huyo ajiunge na Simba msimu huu wa 2020/21, mara kadhaa amekuwa anabadili matokeo ya mchezo pindi anapoingia uwanjani.

 

Ukianza kuzungumzia mechi ambazo umeonekana umuhimu wake kwa kubadilisha matokeo, ni nyingi, lakini kwa za karibuni, ni ile ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Ruvu Shooting iliyochezwa Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

 

Nyingine ni ile ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam dhidi ya Azam FC, iliyochezwa Uwanja wa Majimaji, Songea mkoani Ruvuma.

 

Katika mchezo huo, Morrison alitumia akili kubwa sana na kuisababishia timu yake ya Simba kupata ushindi uliowapeleka fainali ya michuano hiyo.

 

Simba wakiwa mabingwa watetezi wa michuano hiyo, walipata wakati mgumu sana kwa Azam ambapo hadi inafika dakika ya 88, matokeo yalikuwa 0-0.

 

Morrison ambaye alianzia benchi, kuingia kwake kipindi cha pili ikawa ni hatari zaidi kwa Azam ambapo dakika ya 88, Bruce Kangwa wa Azam, alimfanyia faulo nje kidogo ya eneo lao la hatari.

 

Uanzishwaji wa mpira kwa haraka alioufanya Morrison, pasi ikaenda kwa Luis Miquissone na kufunga bao pekee kwa Simba, ndicho kitu ambacho ningependa kukiongelea zaidi leo.

 

Morrison alitumia akili kubwa sana kufanya jambo lile, na hii hutokea kwa wachezaji wenye uelewa mkubwa wa mchezo wa soka, siyo kila mmoja anaweza kufanya namna ile.

 

Hii inanikumbusha msimu wa 2018/19 katika mchezo muhimu wa hatua ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Simba dhidi ya Nkana ya Zambia.

 

Siku hiyo, Simba ilikuwa ikihitaji ushindi wa uwiano mzuri wa mabao dhidi ya Nkana Uwanja wa Mkapa, Dar, baada ya mchezo wa kwanza ugenini kufungwa mabao 2-1.

 

Hadi inafika dakika ya 87 ya mchezo, matokeo yalikuwa 2-1, hapo ikimaanisha kwamba wanakwenda muda wa nyongeza kabla ya kufika kwenye changamoto ya mikwaju ya penalti kama matokeo yangebaki hivyo hadi mwisho.

 

Wakati wachezaji wa Nkana wakizubaa baada ya kufanya faulo iliyoelekeza kwao, Clatous Chama anaanzisha haraka mpira kwenda kwa John Bocco, anampa Hassan Dilunga, anakimbia kidogo pembeni, anapiga ndani kwa Chama, anafunga bao ambalo wachezaji wa Nkana hawakuwa wamejiandaa. Matokeo yanakuwa 3-1, Simba wanakwenda makundi kwa ushindi wa jumla wa 4-3.

 

Chama alivyofanya kipindi kile kwa Nkana, ndivyo amefanya Morrison kwa Azam. Wachezaji wa Azam wakiwa wanazungumza na mwamuzi baada ya kufanya faulo, anaanzisha mpira fasta kwa Luis aliye ndani ya boksi, anaachia shuti linalotikisa nyavu. 1-0 hadi mwisho wa mchezo.

 

Yule Morrison ambaye Yanga walisema ni mtovu wa nidhamu, leo hii ndani ya Simba ni mtu muhimu sana. Hapa pengine kuna kitu watu hawakifahamu.

 

Huyu Morrison wa Simba tunayemuona, kwa mujibu wa Kocha wa Viungo, Adel Zrane, anasema walitumia nguvu ya ziada kumbadilisha kuwa hivi alivyo sasa.

 

Licha ya nje ya uwanja kuonekana ni mtu mwenye matukio mengi ya ajabu, lakini ndani ya uwanja ni mtu muhimu sana. Kocha Mkuu wa Simba, Didier Gomes aliwahi kusema, Morrison ni mzuri zaidi akianzia benchi.

 

Sasa Adel Zrane anasema, Morrison wakati anatua Simba, ilibidi wambadilishe kiakili awe tofauti na vile alivyokuwa akiitumikia Yanga.

 

Kwa mujibu wa Adel, Morrison wakati anacheza Yanga, alionekana ni mchezaji staa wa timu, mambo mengi yanafanywa na wenzake, yeye ni mmaliziaji tu, lakini ndani ya Simba, yeye ndiye mtafutaji, wengine wamaliziaji.

 

Sasa kumbadilisha hapo ndiyo ikawa shida, lakini wakafanikiwa na leo hii, Morrison anawapa raha Simba.

2 COMMENTS:

  1. Morrison yakuwa na tatizo la nidhamu Ila yenyewe ndio wenye tatizo la nidhamu.

    ReplyDelete
  2. Uongozi kitu cha msingi Sana kwenye mafanikio la sivyo mtaishia kubwabwaja tu.... Siataja mtu

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic