September 13, 2021

 


WAWAKILISHI wa Tanzania, Azam FC kwenye Kombe la Shirikisho Afrika walikuwa na dakika 90 za kipekee kwenye mchezo wao dhidi ya Horseed FC ya Somalia na ubao wa Uwanja wa Azam Complex uliweza kusoma Azam FC 3-1 Horseed FC.

Licha ya ushindi huo rekodi zinaonyesha kuwa Azam FC walikuwa wachezaji wao walikuwa wanavitu vyao vya kipekee katika kusaka ushindi na kuipeperusha bendera ya Tanzania na kuweza kuonyesha maana halisi ya timu.

Dakika 45 za awali ngoma ilikuwa ni ngumu kwa timu zote ambapo mabao yaliyofungwa yalikuwa yanafana kwa mtindo wa upatikanaji wake kwa sababu lile la Horseed FC lilipachikwa na Ibrahim Nor aliyevalia jezi namba 28 mgongoni kwa pigo huru akiwa nje ya 18 baada ya Bruce Kangwa wa Azam FC kucheza faulo dakika ya 21.

Mathias Kigonya kipa namba moja wa Azam FC hakuwa na jambo la kufanya kwa kuwa alishuhudia mpira ukizama nyavuni huku yeye akidaka upepo na kuwafanya Horseed kushangilia kwa furaha.

Matajiri hao wa Dar es Salaam iliwabidi wasubiri kwa muda wa dakika 10 ili wapachike bao lilifungwa na Ayoub Lyanga kwa kichwa akitumia pasi ya Idd Seleman, 'Nado' ambaye alipiga faulo nje kidogo ya 18.

Kazi ilikamilika katika dakika 45 za awali kwa timu hizo kutoshana nguvu na dakika 45 za kipindi cha pili mambo yaligeuka na ushindi ukawa kwa Azam FC.


 Mshambuliaji Idris Mbombo alipachika bao dakika ya 72  kwa pasi ya Salum Abubakar, ‘Sure Boy’ aliyekuwa nahodha kwenye mchezo huo na lile la tatu lilipachikwa na Lusajo Mwaikenda ambaye ni beki ilikuwa dakika ya 78.

Licha ya Mbombo kufunga rekodi zinaonyesha kuwa mshambuliaji huyo aliweza kuingia ndani ya eneo la 18 la wapinzani wake mara 39 na ni mara mbili alikuwa na mpira huku mara 37 akiwa katika eneo hilo bila ya mpira.

Pia alipiga jumla ya pasi 16 na aliweza kukokota mpira mara mbili ndani ya dakika 87 ambazo alitumia alionyeshwa kadi moja ya njano na mwamuzi wa mchezo huo na aliotea mara nne. Nafasi yake ilichukuliwa na mshambuliaji mwenzake Rodgers Kola.

Pia rekodi nyingine ambayo iliwekwa kwenye mchezo huo ni Azam FC kucheza jumla ya dakika nne wakiwa pungufu ambapo alikuwa ni Lyanga alitoka baada ya kuumia na mbadala wake alikwama kuingia kwa wakati kwa sababu mpira ulikuwa unaendelea.

Lyanga alitoka dakika ya 81 na mchezaji ambaye aliingia kuchukua nafasi yake ambaye ni Ismail Kader aliingia dakika ya 85, licha ya Azam FC kufanya jitihada za kutoa mpira katika dakika ya 83 mwamuzi aliruhusu ngoma iendelee kuchezwa kama kawaida.

Kiungo msumbufu kwenye mchezo huo alikuwa ni Nado ambaye aliweza kupewa jukumu la kupiga mipira iliyokufa ikiwa ni kona pamoja na faulo.Jambo hilo lilifanya aweze kuchezewa faulo mara nyingi ikiwa ni pamoja na ile ya mwanzo kabisa dakika ya 19 nyingine dakika ya 32 na 43. Kona alipiga dakika ya 3, 10 na 35, faulo alipiga dakika ya 44.

Nahodha Sure Boy alikuwa ni mzee wa kazi chafu ambapo alicheza faulo dakika ya 4 na dakika ya 17 aliweza kusababisha kona moja na alipiga mashuti mawili ambayo hayakulenga lango ilikuwa ni dakika ya 29 na 35.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic