MOJA ya makocha wenye rekodi tamu ndani ya uwanja kwa zama za sasa ni pamoja na Pep Guardiola ambaye anainoa timu ya Manchester City kwa sasa ambao ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu England.
Alijiunga na Manchester City Julai Mosi na mkataba wake unatarajiwa kumeguka Juni 30,2023 na aliweka wazi kwamba hana mpango wa kubaki hapo anataka kupata changamoto mpya.
Kumbukizi yake ya kuletwa duniani ni Januari 18,1971 kwa sasa umri wake unasoma miaka 50 na bado Mungu anamlinda anaonekana kuwa na siha njema pamoja na tabasamu mwanana.
Mfumo wake anaopenda kutumia ni ule wa 4-3-3. Amefundisha kwa mbinu hiyo hata alipokuwa ndani ya FC Bayern Munich alipokuwa hapo msimu wa 2013/14 mpaka mkataba wake ulipomeguka Juni 30,2016 alikaa benchi kuiongoza timu hiyo katika jumla ya mechi 161.
Pia amepita na mbinu hiyo alipokuwa ndani ya Barcelona ilikuwa ni msimu wa 2008/09 mpaka dili lake lilipomeguka Juni 30,2012 na alikaa kwenye benchi katika jumla ya mechi 247.
Mafanikio yake ambayo yanabebwa na mataji aliyotwaa katika timu alizopita ni moja ya heshima kwake na rekodi tamu ambayo anajivunia na pengine ni sehemu ndogo hapa unaipata kwa kuwa ametwaa mataji yakutosha.
Akiwa Barcelona alitwaa tuzo mbili za kuwa kocha bora ambapo ni ule msimu wa 2008 na 2010 huko pia aliweza kuongoza kikosi hicho kutwaa mataji mawili ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ilikuwa ni 2008/09 na 2010/11.
Mara tatu ametwaa taji la La Liga ilikuwa ni 2008/09,2009/10 na msimu wa 2010/11 ilikuwa ni ndani ya Barcelona. Hata alipokuwa ndani ya Bayern Munich bado nyota yake iliwaka na kufanya vizuri.
Ilikuwa ni taji moja la UEFA Super Cup msimu wa 2013/14 na mawili alinyanyua akiwa na Barcelona hivyo jumla ni mataji matatu ya UEFA Super Cup alitwaa, mataji matatu ya Bundesliga ilikuwa ni msimu wa 2013/14, 2014/15 na 2015/16.
Kwa sasa ndani ya City pia cheche zake zinawaka kwani ameipa timu hiyo mataji makubwa matatu ambayo ni ya ubingwa wa Ligi Kuu England na taji moja la FA ilikuwa ni msimu wa 2018/19.
0 COMMENTS:
Post a Comment