UONGOZI wa Simba umeweka wazi kuwa kutokana na mahitaji makubwa ya jezi zao za msimu ujao wa 2021/22, mzabuni na mbunifu wa jezi hizo, Kampuni ya Vunjabei, amelazimika kuongeza oda ya utengenezaji wa jezi hizo ili kukidhi mahitaji ya mashabiki wa klabu hiyo kabla ya tamasha la Siku ya Simba ‘Simba Day’.
Simba inatarajia kufanya tamasha la Simba Day, Septemba 19, mwaka huu ambapo pamoja na matukio mengine, watatambulisha rasmi jezi hizo mpya watakazotumia kwa msimu ujao wa 2021/22.
Jezi za Simba zilianza rasmi kuuzwa Ijumaa ya wiki iliyopita na kuwa gumzo kubwa, ambapo kwa takwimu za uongozi wa Simba ndani ya saa nane ziliweka rekodi ya mauzo ya jezi 42,000 na kukadiriwa kuwa ziliingiza kiwango cha fedha kisichopungua Sh bilioni 1.4.
Jezi hizo zinaendelea kuuzwa katika maduka ya Vunjabei pamoja na mawakala wake kote nchini ambapo jezi ya mtu mzima ni Sh 35,000 huku zile za watoto zikiwa zinapatikana kwa Sh 25,000.
Akizungumza na Championi Ijumaa, Mwenyekiti wa Simba, Murtaza Mangungu, alisema: “Siwezi kuzungumza mengi kuhusiana na suala la mauzo ya jezi zetu mpya kwa sasa, kwa kuwa ni suala ambalo linashughulikiwa kwa kiasi kikubwa na mzabuni wetu kampuni ya Vunjabei.
“Lakini taarifa rasmi ambayo uongozi umeipata kutoka kwa Vunjabei ni kwamba, mahitaji ya jezi yamekuwa makubwa hali ambayo imesababisha mzabuni kuongeza oda ya utengenezaji wa jezi hizo na kuzisafirisha, ili kufanikisha lengo na ahadi ya kila Mwanasimba kuvaa jezi mpya katika tamasha la siku ya Simba.”
Wiki ya Simba inatarajiwa kuanza Septemba 13 na hapo kutakuwa na matendo ya huruma kwa jamii pamoja na usafi wa mazingira.
Pia Septemba 19 unatarajiwa kuchezwa mchezo wa kirafiki kati ya Simba v TP Mazembe ya DR Congo.
Tatizo jenzi huku vijini ni changamoto sana kuzipata tunawaomba muongeze ubunifu tuweze kupata kwa urahisi zaidi. Asante.
ReplyDelete