Mshambuliaji mwenye minguvu wa Simba, Elius Maguli, ameonekana
kujiamini kupitiliza baada ya kutamka kuwa atafanya kazi yake kwa ufasaha na
kuwazidi ujanja Laudit Mavugo na Khamis Kiiza ili yeye awe bora zaidi yao.
Maguli ameenda mbali zaidi kwa kusema, yeye
ndiye mbadala wa straika Emmanuel Okwi aliyejiunga na Klabu ya Sonderjyske ya
Denmark na siyo mchezaji mwingine yeyote.
Tayari Kiiza ameshajiunga na Simba lakini
Mavugo bado yupo kwao akimalizia mechi za timu yake ya Vital’O ndipo aje nchini
kujiunga na Wekundu wa Msimbazi.
Maguli alisema haangalii rekodi bali anasubiri
kuona uwezo utakaoonyeshwa na wachezaji hao na atapambana nao kwa kufanya
mazoezi ya nguvu kuwapiku.
“Unadhani nitaangalia eti nani kafanya nini?
Siogopi lolote kwa hao jamaa ninaogombea nao namba, mimi nitapambana kwa
mazoezi binafsi na tukikutana kwenye mazoezi ya wote watauona moto wangu,”
alisema Maguli.
Hadi sasa Mavugo anaelezwa kufunga mabao 34
katika msimu unaomalizika huko Burundi katika michuano yote na uwezo wa kufunga
wa Kiiza unafahamika tangu alipokuwa Yanga msimu uliopita.







0 COMMENTS:
Post a Comment