Mshambuliaji Thomas Ulimwengu aliyekuwa akikipiga kwenye kikosi cha TP Mazembe ya DR Congo, muda wowote anaweza kujiunga na Azam FC kwa ajili ya kufanya mazoezi kabla ya kutimkia Ulaya.
Ulimwengu ambaye hivi karibuni alimaliza mkataba wake wa kuitumikia TP Mazembe, kwa sasa yupo jijini Dar es Salaam kwa mapumziko ya muda mfupi huku mchakato wa yeye kwenda kucheza soka Ulaya ukiendelea kusukwa.
Awali ilikuwa ikielezwa kuwa, Simba na Yanga zinamtaka straika huyo, lakini wakala wake, Jamal Kisongo, amesema kwa sasa mchezaji wake huyo ni wa Ulaya na si kwingine kwani tayari amefanya mambo makubwa ndani ya Afrika akiwa na TP Mazembe.
Kisongo amesema kuwa: “Ulimwengu yupo Dar, kwa sasa atapumzika kwa wiki moja bila ya kufanya mazoezi kwani ametoka kwenye majeraha, baada ya hapo atakutana na daktari Gilbert (Kigadye) kuangalia maendeleo yake.
“Akionekana yupo fiti, ndiyo ataanza programu za mazoezi na naweza kumpeleka Afrika Kusini au Ubelgiji kule alipo Mbwana Samatta au ajiunge na Azam FC kwa ajili ya mazoezi.
“Huku akiendelea kulinda kiwango chake, tutakuwa kwenye mazungumzo ya mwisho mwisho na timu tatu za Ulaya ambazo zimeonyesha nia ya kumuhitaji, Ulimwengu si mchezaji wa kubaki tena Afrika, wala kwenda bara lingine zaidi ya Ulaya.”
0 COMMENTS:
Post a Comment