Vinara wa Ligi Kuu Tanzania Bara,
Yanga wameendeleza kasi yao ya kushinda mfululizo baada ya kuichapa Kagera
Sugar kwa bao 1-0.
Yanga imefanikiwa kuibuka na
ushindi katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam
leo na kufikisha pointi 42.
Yanga inakuwa timu ya kwanza
kufikisha pointi zaidi ya 40 msimu huu lakini ikiwa ndiyo dalili za kuelekea
kuwavua ubingwa watani wake wa jadi Simba wanaosua katika nafasi ya tatu.
Bao pekee la Yanga leo lilifungwa
na kiungo Myarwanda, Haruna Niyonzima na kumfanya awe amefunga mabao mawili
katika mechi mbili na kuisaidia Yanga kubeba pointi sita mfululizo.
Niyonzima ndiye aliyefunga bao
pekee katika mechi iliyopita ya Yanga dhidi ya Azam FC ambayo ilikuwa ni muhimu
kupiga hatua na kuwaacha vijana hao wauza unga wa ngano na sembe.
Yanga sasa iko kileleni kwa
tofauti ya pointi sita, jana ilipoteza nafasi nyingi za wazi za kufunga ukiwemo
mkwaju wa penalti ambao aliupiga mshambuliaji wake Didier Kavumbagu raia wa
Burundi.
Katika mechi nyingine za ligi
zilizochezwa leo, Coastal Union ikiwa nyumbani ilishindwa kufurukuta mbele ya
Ruvu Shooting na kujikuta ikilazimishwa sare tasa na Kocha Mkuu, Mohammed Morocco
akawalaumu vijana wake kwa kupoteza nafasi nyingi za wazi za kufunga.
Mtibwa Sugar ambaye mechi yake ya
mwisho iliitwanga Simba kwa bao 1-0, leo imeshikiliwa na Prisons ya Mbeya baada
ya kulazimishwa sare isiyokuwa na mabao.
Polisi Moro ambayo imeamka katika
mzunguko wa pili wa ligi hiyo, iliendeleza ushindi baada ya kuilaza Mgambo
Shooting kwa bao 1-0. Timu hiyo haikushinda hata mechi moja katika mzunguko wa
kwanza hali iliyosababisha kocha wake, John Simkoko kutupiwa virago na nafasi
yake ikashukuliwa na mkongwe mwingine Adolf Rishard.
0 COMMENTS:
Post a Comment