Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Mpira wa Miguu (FIFA)
limesema litaifungia Tanzania iwapo itabainika kuwa Serikali imekuwa ikiingilia
shughuli za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
FIFA imesema kumekuwa na shutuma kupitia taarifa mbalimbali
za vyombo vya habari nchini kuwa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo
imeonesha nia ya kuingilia uendeshaji wa TFF.
Kwa mujibu wa barua ya jana (Machi 10 mwaka huu) ya FIFA
kwenda kwa Rais wa TFF, Leodegar Tenga, vyombo vya habari vimemkariri Waziri
(Dk. Fenella Mukangara) kuwa Serikali imeiagiza TFF kutumia Katiba ya mwaka
2006 katika uchaguzi wakati tayari imeshafanyiwa marekebisho.
“Pia imeelezwa kuwa TFF imetakiwa kufanya Mkutano Mkuu pamoja
na ule wa uchaguzi kwa tarehe ambazo zimepangwa na Serikali. Vilevile imeelezwa
kuwa Serikali inakusudia kuunda Kamati ya Muda iwapo TFF haitatekeleza maagizo
yake,” imesema sehemu ya barua hiyo iliyosainiwa na Katibu Mkuu wa FIFA, Jerome
Valke.
FIFA imesema iwapo yaliyoripotiwa na vyombo vya habari
yatathibitika kuwa kweli, maana yake huo ni uingiliaji wa wazi wa Serikali kwa
shughuli za TFF.
“Tunapenda kuwakumbusha kuwa wanachama wote wa FIFA
wanatakiwa kuendesha shughuli zao kwa uhuru bila kuingiliwa na mtu mwingine
kama ilivyoelezwa katika ibara za 13 na 17 za Katiba ya FIFA.
“Hivyo kama maagizo hayo yanayodaiwa kutolewa na Serikali
yatatekelezwa, suala hili litapelekwa katika mamlaka za juu za FIFA kwa hatua
zaidi ikiwemo kuisimamisha Tanzania kama ambavyo inakuwa pale panapokuwa na
uingiliaji wa Serikali,” imesema barua hiyo.
Barua hiyo ambayo nakala yake pia imetumwa Shirikisho la
Mpira wa Miguu Afrika (CAF) imeelezea baadhi ya athari ambazo Tanzania
itakumbana nazo endapo itasimamishwa ni timu za taifa pamoja na klabu
kutoshiriki mechi za kimataifa kwa mujibu wa Ibara ya 14 ya Katiba ya FIFA.
Vilevile si TFF au wanachama wake na maofisa wengine
watakaoweza kunufaika na programu za maendeleo, kozi au mafunzo yanayotolewa na
FIFA na CAF.
“Madai ya uamuzi uliofanywa na Wizara ya Habari, Vijana,
Utamaduni na Michezo ni ya kusikitisha kutokana na ukweli kuwa FIFA
ilishatangaza itatuma ujumbe wake kuchunguza jinsi hali ilivyo kwa sasa na
kutoa mapendekezo yake. Kutokana na hali hii, ujumbe wa FIFA uliokuwa uje
kuchunguza (suala la uchaguzi) itabidi usubiri kwa vile ni muhimu kushughulikia
tatizo hili kwanza.
“Katika mazingira haya tunaomba ueleze msimamo huu wa FIFA
kwa mamlaka zinazohusika (Serikali) na athari ambazo mpira wa miguu wa Tanzania
utakumbana nazo. Tunakushuru na tunatarajia utatufahamisha kila hatua
inayoendelea katika suala hili,” imesema barua hiyo.
0 COMMENTS:
Post a Comment