Na
Saleh Ally
MARA
baada ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete kutembelea na kuzindua uwanja wa Azam
Complex, kuna mengi sana ambayo yamejitokeza na hakika inawezekana kabisa
vyombo vya habari havikutoa nafasi iliyostahili.
Ingawa
ilikuwa ni ziara ya uzinduzi wa uwanja huo, Kikwete ambaye anajulikana kwa kuwa
mwanamichezo na mwenye mapenzi ya dhati na michezo tokea akiwa mwanafunzi,
alisema maneno mazito na huenda yalistahili yapewe nafasi kubwa ili
kuwakumbusha wadau ambao wamekuwa wakididimiza michezo.
Siwezi
kusema Azam FC wao ni manabii, kila kilichosemwa na Rais Kikwete hakikuwagusa
kwa maana wako katika kundi la wakosaji, lakini waliepuka mengi kwa kuwa
wameweza kuonyesha mwendo mzuri.
Lakini
siwezi kusema Rais Kikwete ni ‘mchawi’, aliyoyasema yako wazi, yanaonekana na
kila siku ni wimbo lakini hakuna kinachobadilika.
Madongo
yake mengi yaliangukia kwa wakongwe Yanga na Simba kwenye matatizo yasiyoisha.
Huenda walikuwa wajanja kwelikweli maana hakuna kiongozi hata mmoja alikubali
kutia mguu kule Chamazi Complex, maana wanajua Rais Kikwete ‘hakopeshi’.
Lakini
kwa siku moja, Kikwete aligusa mambo mengi sana ya msingi katika soka ya
Tanzania, hakumkopesha mtu, hakuwa na aibu wala huruma na wanaovurunda.
Inawezekana kabisa ni wakati wa kuyatafakari kwa kuwa Saleh Ally huenda
aliyasema mara kadhaa, lakini yakapita sikio la kushoto na kutokea la kulia na
wahusika wakaendelea kuboronga kwa hasira zaidi.
Lakini
safari hii, Rais wa Tanzania, amefunguka na kusema madudu yote ambayo si siri
hata kidogo. Angalia maisha ya Simba na
Yanga, leo Azam FC inaonekana inawapita mengi ndani ya miaka mitano tu, lakini
zenyewe zilizaliwa miaka ya 1930 mwanzoni.
Kikwete
ameonyesha habatishi, najua kweli uozo ndani ya michezo. Angalia kuhusu kamati
za ufundi ambazo ni ushirikina mtupu, kuhonga wachezaji, kucheza kwenye viwanja
vya kuanzima au kukodisha, kusajili kwa kukomoana, namna wanachama
wanavyoziangusha timu zao. Amechambua kwa kina bila ya kupindisha.
Azam
kuogopewa na vigogo:
Kweli
Azam FC inaogopewa na vigogo Yanga na Simba na hatari zaidi kwa wale waliokuwa
wanaonekana vigogo wa daraja la pili kama Mtibwa Sugar ambao wamekuwa
wakitandikwa na Azam FC kama watoto.
Kuwepo
kwa Azam FC, kumefanya katika msimu mmoja wa ligi kuwe na ‘big match’ sita
badala ya mbili, awali ilikuwa ni Simba na Yanga zinapokutana katika mzunguko
wa kwanza na wa pili. Lakini sasa mechi mbili za Yanga dhidi ya Azam na Simba
dhidi ya timu hiyo, zimekuwa mechi kubwa na zinazongumziwa sana.
Ukiritimba
wa Yanga, Simba:
Zina
ukiritimba upi? Unaweza ukafikiri kwamba hazina kitu hicho lakini hakika
mashabiki wa timu hizo wamekuwa hawapendi kuona timu nyingine inatamba.
Wanaamini mpira wa Tanzania ni Yanga na Simba.
Unaweza
ukashangaa wakati mwingine, Yanga na Simba wako tayari kuungana ili kuhakikisha
timu nyingine mfano wa Azam FC haiwi bingwa. Kawaida kama ni ushindani, vizuri
timu bingwa ifanikiwe kwa uwezo wake.
Kutaka
kulazimisha timu ishinde au iwe bingwa kutokana na ukubwa wa jina lake ni
tatizo jingine kubwa katika soka nchini. Yanga na Simba wanahusika zaidi katika
hili.
Kamati
za ufundi:
Kikwete
anajua kuhusu kamati ya ufundi, hatari sana. Ina maana hawa jamaa ni maarufu sana
kwa kuwa hadi rais anawajua. Tunajua namna ambavyo fedha za klabu hizo
zinavyomegwa kwa vigezo vya ujanjaujanja.
Kamati
za ufundi ni mitaji ya wanachama na
viongozi maarufu wa klabu hizo, wanaamini eti wakifanya mambo ya ushirikina
timu itafanya vizuri. Hali halisi inajulikana, wanajua wanachofanya si sahihi
na ni kwa ajili ya maslahi ya klabu zao, badala wao binafsi.
Wakati
mwingine imefikia kwa mwezi klabu inatoa hadi Sh milioni 50 kimyakimya eti kwa
ajili ya kamati ya ufundi, hapa wanagawana wapambe wa viongozi. Hawa ni adui wa
klabu hizo, lakini ndiyo wamekuwa wanafiki wakubwa na wanaofikia hadi kulia
machozi kujidai wanazitetea, kumbe wanalilia maduka au ofisi kwa ajili ya
kuendesha maisha yao na wala si mapenzi.
Kuhonga
wachezaji:
Hili
tatizo Rais Kikwete ameonyesha kweli ni mtu wa michezo ikiwemo soka, anajua
kila kitu lakini hapa inawezekana kidogo pamoja na kuwakandia Yanga na Simba au
timu nyingine, basi angewaasa Azam FC pia.
Sidhani
kama Azam FC wanaweza kuwa wasafi moja kwa moja katika hili, inajulikana na
mambo ni mengi sana. Bado suala la hongo ni tatizo kubwa sana na wachezaji,
viongozi, makocha na hata waamuzi wamekuwa wakihusika.
Hatuwezi
kuwatoa Azam FC, bado tunatakiwa kuchunguza. Lakini alichokisema kinaendelea
kweli, ingawa wako ambao wamekuwa wakitaka kujisafisha bila ya kujua wanajipaka
zaidi vumbi la masizi ya mkaa. Hivi karibuni kulikuwa na taarifa kuna klabu
imeunda timu ya kuisaidia kushinda mechi kadhaa kwa kutoa rushwa, anayefanya
kazi hiyo anapata mshahara na posho na amepewa usafiri.
Leo
rais wa nchi anajua kuhusiana na kinachoendelea kuhusiana na upuuzi huo, lakini
kuna watu bado wanaendelea na inaonekana ni mambo ya kawaida kabisa. Hatari
sana, iko haja ya kujiangalia na kubadilika, soka linaweza kukua na bila ya
rushwa. Fedha wanazotoa, bora wawape vijana kama hamasa.
Viwanja
vya kuazima:
Hapa
ndiyo sehemu ya kichekesho kabisa, kama Rais Kikwete anajua Yanga na Simba
wanatumia viwanja vya kuanzima, maana yake anajua kila kitu kuhusiana na namna
Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage ambavyo amekuwa akitoa ahadi za ujanja
ujanja kuhusiana na uwanja na hakuna ambacho amekifanya.
Yanga
wana uwanja wao, lakini pia wameshindwa hata kuweka ‘pitch’ au sehemu ya
kuchezea na badala yake wamekuwa wakitangatanga kutafuta uwanja wa kufanyia
mazoezi. Kocha wao Ernie Brandts ya mungu amekuwa akilia. Wao wanaona ndiyo
maisha mazuri!
Kambi
za uhakika:
Mlo
wa wachezaji wa Kitanzania ni tatizo, Rais Kikwete alisisitiza ni vizuri wakala
vizuri badala ya kuendeleza tabia ya kula chips na mayai. Pia akashauri
wachezaji walale pazuri. Ukiangalia hapa anazungumza masuala ya kitaalamu.
Yote
hayo yamewashinda viongozi na hata wachezaji wenyewe kwa kuwa wamekuwa wazito
kujua au kuamini ya wanachoelekezwa. Wachezaji hawataki kupumzika, ikiwezekana
wanaona kuzunguka mitaani na kuonekana, au kwenda kucheza ndondo wakati
wanatakiwa kupumzika ndiyo jambo sahihi.
Lakini
bado viongozi wanaamini wachezaji kula vizuri, kulala sehemu nzuri ni suala la
anasa. Mifano yao ni ileile kwamba wachezaji wa zamani kama akina Sembuli, Ma:
Kusajili
mchezaji, asicheze timu nyingine:
Wakati
mwingine unajiuliza, rais anajua kuhusiana na upuuzi huu hasa wa Yanga na
Simba, kweli anafuatilia soka. Maana amelizungumzia suala ili, nakumbuka niliwahi
kuandika ukurasa mzima nikieleza namna Yanga na Simba zinavyoweza kukomoana
bila ya kujali hasara.
Timu
moja inaweza ikaamua kumsajili mchezaji fulani wakati haimhitaji, eti kisa
anaweza kusajiliwa na timu nyingine halafu ikapata sifa. Haiangalii yenyewe
inahitaji nini badala yake mtani wake anafanya nini, huo ni upuuzi!
Hili
limekuwa ni tatizo na utaona kuna wakati timu zinafeli kwa kuwa zilisajili kwa
lengo la kupata sifa kwa mashabiki na wanachama wake au kukomoa upande
mwingine. Wakati mwingine viongozi wakiona upuuzi umewazidi uzito,
wanauangushia kwa makocha na ikiwezekana wanawatimua
Wanachama:
Hapa
ndiyo kasheshe, sikushangaa Rais Kikwete kuonyesha anawajua vizuri wanachama wa
timu hizi. Amesema anaamini Azam FC inaweza kufika mbali kwa kuwa
haiendeshwi na wanachama.
Lakini
kauli hii ya Kikwete, kwamba wanachama zaidi wao ndiyo wanazitegemea klabu
kujiendesha ni kweli, kama nilivyoeleza awali. Wako wale wanaozipenda Yanga na
Simba kwa kuwa wanajua watakaa milangoni na kufanikiwa kupata cha ‘juu’.
Wanazipenda
ili waishi, lakini si mapenzi ya dhati. Wanachama wengi ndiyo wanaoongoza
kuzidhoofisha klabu zao, wababaishaji na adui wakubwa wa maendeleo ya klabu
hizo, nitatoa mifano.
Viongozi
wasio na uwezo, lakini wenye uwezo wa kutoa hongo wamekuwa wakishinda uchaguzi
na mwisho wanakua sumu kwenye maendeleo ya klabu hizo, ukiangalia chanzo ni
wanachama waliojali maslahi yao, matumbo yao kwa kuchukua hongo na kuwapigia
kura wasio na uwezo.
Kweli
nani atafanya hivyo kwa Azam FC, ndiyo kama alivyosema Rais Kikwete itakuwa na
nafasi ya kuendelea haraka zaidi kwa kuwa hakuna longolongo kupindukia na
hadithi nyingi za kusema “sisi ndiyo wenye klabu”, kumbe hata ada ya Sh 1000
kwa mwezi hawalipi na badala yake wanajali nafsi zao na kuwa tatizo tu.
SOURCE:
CHAMPIONI JUMATATU
0 COMMENTS:
Post a Comment