Inawezekana kuna watu wanashindwa kusema kwa hofu ya kuambiwa wanatumika. Hii imekuwa kawaida, viongozi wanaoshindwa kazi yao kama watakosolewa, basi hawachelewi kuanzisha kiampeni za kusema fulani anatumika kwa lengo la kuhamisha hoja ya msingi na kuwajaza watu upuuzi ili waachane na kinachojadiliwa ambacho ni cha msingi.
Sidhani kama mtu mwenye nia nzuri na anachokiamini anaweza kukwama kutokana na hoja nyepesi kama hiyo ya fulani anatumiwa. Kila kitu kiko wazi kwamba Simba imefeli kila idara ukianzia ndani ya timu, suala la fedha za klabu na hata kuwaunganisha wanachama wake.
Hata kama kutakuwa na kundi linaloupinga uongozi, lakini kama mambo yanakwenda kwa mpangilio, mfano wachezaji wanalipwa mshahara na fedha zao vizuri, hakuna madeni ambayo yangewezekana kulipwa kama kusingekuwa na ufujaji na timu inafanya vizuri, vipi hayo makundi yangepata nafasi ya kuivuruga timu?
Achana na hayo ambayo yamekuwa kama ni mpito na ambayo nimekuwa nikiyazungumzia kila kukicha bila ya hofu ya kuonekana natumika au eti nina chuki na fulani, leo nilitaka niendelee kuwaanika na kuwashangaa watu ambao wamekuwa ni tatizo kubwa katika mpira.
Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage na washauri wake, lakini hata kama wako wanaompinga, basi wote watakuwa ni watu wasiokuwa na busara na wanaofanya mambo yao kwa kubabaisha ,huku wao wakiamini wana akili sana.
Naweza kuwafananisha na programu inayopatikana katika simu na kompyuta maarufu kama Bluetooth ambayo kazi yake ni kunyonya tu mambo inayotumiwa. Haitafakari uzuri, ukubwa wala ubaya wake. Ndicho walichofanya walioandaa mapokezi ya Rage, naye akakubali na wengine wakaandaa watu kwenda kumpinga.
Nasema hivyo kwa kuwa kitendo cha wanachama na mashabiki wa Simba kwenda Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) kwenda kumpokea Rage na wengine kwenda kumzomea, inaonyesha kiasi gani wanachama wamekuwa ni bendera fuata upepo. Hao ndiyo baadhi ya wanachama na mashabiki wa klabu zetu wenye maneno mengi, wanaojidai wanazipenda klabu hizo lakini kumbe wanazipenda ili ziwalishe na kuendeleza maisha yao.
Ndiyo maana wanakubali kuwa wanasesere wanaoweza kuchezeshwa wakati wowote ili kuwafurahisha viongozi fulani. Mfano, kwa wale waliokwenda kumpokea Rage eti kwa mbwembwe nyingi, wakiwa katika magari na wamevaa sare kwa kipi hasa? Walifuata nini? Rage alikuwa na kipi kipya cha kufanya wanachama kwenda kumpokea? Maana yake walipangwa na kutakiwa kufanya hivyo ili kupoza hali ya hewa iliyochafuka hasa baada ya baadhi ya wanachama kukutana na kutangaza kumng’oa Rage.
Nani mwenye akili zake timamu, anayejua anakifanya ni kipi? Anayeangalia muda na uchumi wake atakubali kufanya kitu hicho? Simba ilikwenda kupambana na Libolo nchini Angola, huku wachezaji wakiwa wanadai fedha zao, lakini walicheza na mwisho wakafungwa mabao 4-0. Kama kweli mashabiki wanajali, vipi hawakwenda kuwapokea askari waliokwenda kupigana kwa ajili ya rangi nyekundu na nyeupe wanazozipenda? Rage amepigania nini? Upuuzi kabisa!
Lakini kama wako wanaompinga Rage, vipi nao waliamua kutuma mashabiki na wanachama kwenda wakiwa kwenye basi aina ya Toyota Coaster na kuanika mabango yanayompinga? Mwisho wakaambulia kipigo kutoka kwa wale walioandaliwa na upande wa Rage. Angalia hawa watu walivyo na mawazo ya kizamani, angalia wasivyotafakari na kujali muda na fedha. Hakika viposho kidogo tu vimewatoa roho na kuamua kwenda uwanja wa ndege bila ya kutafakari kwamba wanachokifanya hakiisaidii klabu hiyo.
Inawezekana wanajua, lakini kilichowasukuma kwenda huko ni fedha kidogo tu za kusukuma siku, au ushawishi wa maneno ambayo hawakuyatafakari. Rais Jakaya Kikwete alichambua mambo kadhaa baada ya kutembelea na kuzindua uwanja wa Azam Complex, Chamazi jijini Dar.
Kati ya aliyoyazungumzia ni matatizo ya wanachama, na hawa waliokwenda uwanja wa ndege kumpokea na wengine kumpinga Rage ndiyo hasa sehemu ya waliolengwa kwa kuwa ni sumu na matatizo makubwa kwa klabu.
0 COMMENTS:
Post a Comment