Kocha wa Mtibwa Sugar, Mecky Maxime ambaye hivi karibuni
aliwahi kutoa ushauri wa kuwadhamini makocha wazalendo, ameshauri kusiwe na
papara ya kuwatimua makocha wa kigeni na hasa wazungu.
Maxime ambaye alikuwa beki mahiri wa Mtibwa Sugar na Taifa
Stars, amekuwa akikiongoza vema kikosi chake ambacho kwa msimu huu kimekuwa
kiboko ya Yanga na Simba.
“Ninaposema makocha wazawa wathaminiwe, sina maana wazungu au
wageni wafukuzwe. Waendelee kuwepo na wanaweza kuwa sehemu ya changamoto.
“Lakini nasisitiza kuwe na tabia ya kuamini hata makocha wa
Tanzania ni wazuri na kuna kila sababu ya kuwapima kutokana na kazi zao,”
alisema Maxime.
Katika mechi zake nne za Ligi Kuu Bara katika mizunguko
miwili, Mtibwa Sugar jumla ya pointi 10 huku kikiwa hakijapoteza hata mechi
moja.
Katika mechi za mzunguko wa kwanza, Mtibwa iliifunga Yanga
kwa mabao 3-0 na kusababisha kutimuliwa kwa aliyekuwa Kocha Mkuu, Tom
Saintfiet. Mechi ya mzunguko wa pili, matokeo yakawa sare ya mabao 1-1 Yanga
ikiwa chini ya Ernie Brandts.
Kwa upande wa Simba, mzunguko wa kwanza, Mtibwa Sugar
iliichapa Simba mabao 2-0 na kusababisha tafrani kubwa kwa mashabiki kuandamana
wakitaka nahodha Juma Kaseja na Geofrey Nyanga ‘Kaburu’ wajiuzulu.
Mechi ya mzunguko wa pili, safari hii Simba ikiwa na kocha
mpya Mfaransa, Patrick Liewig ambalo linatamkwa Lievig, Simba ikalala kwa bao
1-0 na kusababisha presha kubwa ndani ya Msimbazi.
0 COMMENTS:
Post a Comment