Na Saleh Ally
Bila ya kupepesa, hatimaye yametimia na mshambuliaji wa Simba, Felix Sunzu amepewa ruhusa ya kuondoka.
Ingawa jambo hilo limekuwa likienda kimyakimya, Simba wamekubaliana kwamba baada ya kumaliza msimu, Sunzu raia wa Zambia mwenye asili ya DRC, aende zake.
Simba imebakiza mechi mbili dhidi ya Ruvu Shooting itakayochezwa Mei 5 na ile dhidi ya watani wake wa jadi Yanga itakayopigwa Mei 18 na inaonekana ndiyo mechi za mwisho za Mzambia huyo akiwa na Simba.
Chanzo cha uhakika kutoka ndani ya Simba, kimeeleza kuondoka kwa Sunzu kunatokana na kutoonyesha kiwango kizuri kwa misimu miwili.
Lakini mzigo wa mshahara wa dola 3,500 (Sh milioni 5.6) kwa mwezi limekuwa ni tatizo jingine kwa Simba inayokabiliwa na ukata katika kipindi hiki.
“Kweli Sunzu ataondoka, hatakuwa tena na nafasi na kila kitu kimeonekana. Tumeona kwa kuwa mkataba wake umekwisha aondoke kwa amani.
“Suala lake lilijadiliwa katika kamati ya utendaji na watu wa ufundi wameona bora iwe hivyo,” kilieleza chanzo cha uhakika.
Tokea ameondoka Milovan Cirkovic aliyekuwa kocha Simba, Sunzu amekuwa haelewani na kocha wa sasa, Patrick Liewig.
Aliwahi kumsimamisha baada ya kutoweka kambini, siku chache baadaye aliporejea mazoezini akamtimua na kumtaka aandike barua.
Pamoja na kuandika barua, lakini akaonyesha hataki arejee hadi uongozi ulipoingilia na kumrudisha Sunzu pamoja na kiungo Mwinyi Kazimoto.







0 COMMENTS:
Post a Comment