Mechi ya Ligi Kuu Bara kati ya Ruvu Shooting na Simba
iliyokuwa ichezwe leo (Aprili 25 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam sasa
itafanyika Mei 5 mwaka huu kwenye uwanja huo huo.
Mabadiliko hayo yametokana na Serikali kuutumia uwanja
kwa ajili ya maandalizi ya sherehe za Muungano ambazo kitaifa zitafanyika kesho
(Aprili 26 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limetangaza
kuahirishwa kwa mechi hiyo dakika chache zilizopita na kuomba radhi washabiki
kwa usumbufu uliojitokeza.
Hata hivyo, bado hali hiyo imewashangaza baadhi ya
wadau kwamba TFF hawakuwa wakijua kwamba kutakuwa na maandalizi leo.
“Maandalizi ya muungano si kitu kigeni na siku ya
muungano inajulikana kila mwaka, sasa vipi ijulikane leo,” alisema Mhariri wa
Championi Ijumaa, John Joseph.
“Lakini kama haitoshi, angalau wangeahirisha jana ili
watu wajue leo mapema, wanatangaza sasa saa saba kasoro mchana, maana yake
wengine wako njiani wanakwenda uwanjani. Si kitu kizuri na inabidi waliangalie
hili.”
Ligi hiyo inaendelea kesho (Aprili 26 mwaka huu) kwa
mechi kati ya Coastal Union na Azam itakayochezwa Uwanja wa Mkwakwani jijini
Tanga wakati Jumapili (Aprili 28 mwaka huu) itakuwa katika Uwanja wa Taifa, Dar
es Salaam ni Simba dhidi ya Polisi Morogoro.







0 COMMENTS:
Post a Comment