April 30, 2013





Na Saleh Ally
KURUDI kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Pope, kumekuwa ni faraja upya kwa Wanasimba ambao walikuwa wakijiuliza maandalizi ya msimu ujao yatafanyika vipi.

Simba imepoteza dira kutokana na kuyumba kwa mambo mengi na sasa inaendelea kupigania nafasi ya tatu ambayo huenda isiipate kama haitakaza ‘buti’. Kutoka bingwa, hadi kugombea nafasi ya tatu!

Hans Pope aliamua kujiuzulu baada ya kutoridhishwa na mwenendo wa klabu hiyo kuanzia katika uongozi wa juu na migogoro mfululizo iliyokuwa inaendelea.

Juhudi kubwa zilifanyika kwa Wanasimba wakitaka arejee kwa kuwa walijua matatizo yaliyokuwa yakiendelea hakuwa akihusika, halafu alikuwa msaada mkubwa katika klabu hiyo, hivyo kujiuzulu kwake ni sawa na kuongeza matatizo zaidi ndani ya Msimbazi.


Katika mahojiano na Championi Jumatatu yaliyofanyika jana Jumapili, Hans Pope anasema kuna mambo muhimu ya kuzingatia ambayo Wanasimba wanatakiwa kuyafanya ili kuhakikisha kunakuwa na mabadiliko msimu ujao, la sivyo wataendelea kufeli.

Saleh Ally: Umerudi, labda umeridhika hasa na hali iliyopo Simba hadi umeona ni vizuri kurejea?
Hans Pope: Ndiyo, inawezekana mambo bado si mazuri lakini mimi na Wanasimba wote ndiyo tunapaswa kuweka mambo sawa. Hivyo lazima tuendelee kupambana kuhakikisha kila kitu kinakwenda vizuri.

Saleh Ally: Unafikiri  nini cha kufanya sasa?
 Hans Pope: Kuepusha migogoro, wale waliotaka kuutoa uongozi madarakani wasirudie tena, maana siku hizi katiba zimebadilishwa, hakuna yale mambo ya kizamani. Kwanza hakuna faida ya kufanya hivyo, wasubiri uchaguzi kama wanataka kufanya mabadiliko.

Saleh Ally: Maana yake unaona ni sawa kama kiongozi anavurunda, basi aendelee kufanya hivyo na wanachama wakae kimya tu hadi muda wake uishe?
 Hans Pope: Hapana, ninamaanisha hivi, hakuna haja ya kupinduana na tunapaswa kufuata katiba. Lakini kama kuna kiongozi anaona mambo yamemshinda, hapaswi kusubiri kusukumwa kufanya hivyo kwa kuwa anaona ukweli. Basi kitu kizuri kama anaipenda Simba, aachie ngazi kwa faida ya klabu.

Saleh Ally: Wewe ni mwenyekiti wa usajili, vipi mmeanza michakato ili kujenga kikosi imara msimu ujao?
 Hans Pope: Tayari tumeanza, lakini ninapenda kamati ya usajili iachiwe ifanye kazi yake. Yale mambo ya watu kila mmoja kuleta wachezaji wake yasipewe nafasi.

Saleh Ally: Kuleta wachezaji kivipi?
Hans Pope: Unajua kila mtu alikuwa akileta wachezaji anaowaona, anawaingiza na kuwasajili. Mwisho ikawa matatizo, lakini safari hii mambo yatafanyika kitaalamu zaidi.

Saleh Ally:  Mbona sisikii kama ukisema kocha Mfaransa naye atashirikishwa?
Hans Pope: Lazima atashirikishwa, lakini itabidi awe makini maana kocha aliyeondoka (Milovan) alipelekewa wachezaji akasema wanafaa. Lakini mwisho wakaboronga, yeye pia alichangia, kitu ambacho nisingependa kitokee.

Saleh Ally: Iwapo itakuwa kama ilivyokuwa kwa Milovan, nini kitafuatia kwa Mfaransa, Patrick Liewig?
Hans Pope: Hakutakuwa na mzaha, mara moja naye atatimuliwa. Tunapompa dhamana maana yake tunamwamini, akienda tofauti basi hatua zinachukuliwa.

Saleh Ally: Je, nafasi zipi mlizoanza kuzifanyia kazi ili kusajili, na wachezaji wangapi watatoka nje ya Tanzania?
Hans Pope: Kwanza tunaanza nyumbani, nafasi itakuwa ni mapendekezo  ya mwalimu na baada ya hapo tutakutana na kamati zinazohusika na mwisho usajili utafanyika. Kama atasema namba tatu, basi tutatafuta aliye bora tutamsajili, akisema beki wa kati, mara moja tutafanya hivyo. Hadi sasa kuna kazi tunaendelea kuifanya lakini tutafanya tathmini mara tu baada ya kumalizika kwa msimu.

Saleh Ally: Nashukuru kwa ushirikiano na siku njema.
Hans Pope: Ahasante sana, nawe pia.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic