Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia
Hans Pope amesema wamemkabidhi Kocha Mkuu, Patrick Liewig jukumu la kueleza
mapungufu ambayo wao watayafanyia kazi.
Hans Pope amesema Liewig atawaeleza wao mapungufu
na wachezaji katika nafasi gani wanatakiwa kusajiliwa ili kuwa na kikosi bora.
“Baada ya kocha kusema, basi sisi mara moja
tutaanza kuyafanyia kazi na kama kusajili tutasajili.
“Kikubwa tunatoa nafasi kwa kocha aeleze anataka
nini, baada ya hapo kazi yetu itakuwa ni kufanya usajili,” alisema Hans Pope
ambaye alikubali kurejea Simba hivi karibuni.
Kati ya wachezaji wanaoonekana kukutana mapema na
panga la Liewig raia wa Ufaransa ni mshambuliaji Mzambia, Felix Sunzu.
Tokea ametua Simba na kuchukua nafasi ya Milovan
Cirkovic amekuwa akitumia kikosi cha vijana huku akiwa na mgogoro na wachezaji
wengi wakongwe akiwemo Sunzu.
Sunzu ni kati ya wachezaji aliowasimamisha, lakini
baadaye alirejea baada ya kukubali kuandika barua kuelezea sababu za msingi
zilizomfanya atoweke kambini bila ya taarifa.
Kingine kitakachomuondoa Sunzu Simba, ni kutofanya
vizuri msimu mzima huku akiwa analipwa kitita kikubwa zaidi cha mshahara cha
dola 3,500 ambacho ni kikubwa zaidi kuliko anacholipwa mchezaji mwingine wa
Ligi Kuu Tanzania Bara.








0 COMMENTS:
Post a Comment