Haikuwa kazi kwa Borussia Dortmund kutinga fainali
ya Kombe la Uefa Champions League pamoja na kupoteza mechi kwa kufungwa bao 2-0
na wenyeji wake Real Madrid.
Cristiano Ronaldo na kocha wake Jose Mourinho
waliokuwa na ndoto ya kufika fainali wakiwa na Madrid waliwashuhudia Dortmund
walioshinda bao 4-1 katika mechi ya kwanza wakisonga kwa ulaini.
Kipindi cha kwanza kilikuwa na kosakosa kila upande
na Madrid ndiyo walipoteza nafasi zaidi ya tatu za kufunga.
Lakini kipindi cha pili, Dortmund ndiyo
walishambulia mfululizo likiwamo shuti la Lewandowski lililogonga mwamba.
Pamoja na kupoteza nafasi nyingi Madrid walipata
mabao katika dakika ya 83 kupitia Sergio Ramos na dakika ya 88 mfungaji akiwa
Sergio Ramos.
Madrid ilitakiwa ishinde kwa mabao 3-0 ili kusonga
mbele, hivyo hadi mechi iliyochezeshwa na Muingereza Howard Webb inafika dakika
90, mabao 2-0 hayakuisaidia Madrid kusonga mbele zaidi ya kutengeneza heshima.
Michael Essien, Ramos, Angelo Di Maria, Benzema,
Ozil walikuwa kati ya waliofanya vizuri lakini Ronaldo hakuwa na siku nzuri
sana kutokana na kutocheza katika kiwango kizuri na kuisaidia timu yake kama
ilivyotegemewa.
Kesho mechi nyingine ya nusu fainali itakuwa kati
ya wenyeji Barcelona kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Camp Nou dhidi ya
Wajerumani wengine, Bayern Munich.
Katika mechi ya kwanza mjini Munich, Barcelona walilala
kwa mabao 4-0, hivyo wanalazimika kushinda 5-0 ili kusonga mbele.
0 COMMENTS:
Post a Comment