Na Saleh
Ally
KUONDOKA
kwa aliyekuwa Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Marcio Maximo kuliamsha hoja nyingi
sana ambazo nyingi hazikuwa na nguvu badala yake zilionyesha upande wa pili wa
Watanzania wapenda soka.
Watanzania
wengi wapenda soka ni waoga, wanaamini kupita kiasi na wasio na uwezo wa
kuthubutu, ndiyo maana wana hofu sana na mabadiliko.
Mara
nyingi, mabadiliko hayapatikani bila ya kuwa na watu wanaoweza kujitolea na
kupambana bila ya kuwa na uoga. Kawaida waoga hubaki salama lakini bila ya
kupiga hatua.
Maximo raia wa Brazil aliyefanya kazi nchini kwa miaka minne,
alikuwa mmoja wa makocha ambao hatasaulika nchini kwa mambo mengi likiwemo la
mabadiliko.
Alisaidia mengi, lakini yalikuwepo aliyoboronga na wadau wengi wakawa
waoga kuona anakosolewa hata alipoboronga, huenda bado kuna hisia za kuwahofia
wageni au wazungu ambao tunaamini wanapatia kila kitu.
Uzuri:
Pamoja na kwamba alileta mabadiliko katika kikosi, lakini alikuwa
mjanja katika uhamasishaji nje ya uwanja, alitokea kupendwa na mashabiki ambao
alitumia muda mwingi kuwahamasisha. Poulsen hana uwezo huo na macho yote katika
kazi yake.
Alijitahidi kuchagua kikosi cha wachezaji vijana, ingawa naweza
kusema hakuwa mzuri zaidi kwa upande wa kuamini vijana. Zaidi aliwapa zaidi
nguvu wakongwe kama Salum Sued, Mecky Maxime, Shadrack Nsajigwa na walicheza
vizuri.
Ingawa bado kiasi fulani vijana wachache aliwajenga kama Jerry
Tegete na Kiggi Makasi wakati alipokuwa kocha, walifanya vema.
Tatizo:
Alikuwa kocha mwenye gubu, anayenuna na asiyetaka kusamehe. Ugomvi
mkubwa ulikuwa ni kuwanunia Athuman Idd ‘Chuji’, Haruna Moshi ‘Boban’ na Juma
Kaseja. Mbaya zaidi hakuwa akisema hata sababu ya msingi.
Badala yake alisisitiza hatawaita, kitu ambacho hakikuwa sahihi
hata kidogo, kama mtaalamu alilazimika aeleze mambo yake kitaalamu.
Waoga walihofia kumpa changamoto, lakini Tanzania haina waoga
tupu, wako waliomueleza na hadi alipomaliza mkataba anabaki na sifa zake na
upungufu wake.
Tanzania ilionekana kuyumba baada ya Jan Poulsen kutoka Denmark
kushika nafasi, babu huyo kidogo ukali wake ulimuathiri na timu haikufanya
vizuri.
Lakini Jan Poulsen ambaye alimpendekeza kwa ajili ya timu za
vijana alikuwa bora zaidi na leo mabadiliko makubwa yanaonekana kiuchezaji
lakini vijana amewapa zaidi nafasi kuliko hata Maximo.
Asilimia 75 ya kikosi cha Stars ni vijana, hata wakongwe waliopo
wanaendelea kukaa benchi ingawa inapobidi anawapa nafasi na wengi wamekuwa
wakionyesha uwezo.
Frank Domayo, Simon Msuva, Salum Abubary ‘Sure Boy’, Shomari
Kapombe, Waziri Salum, Raadhani Singano ‘Messi’, Jonas Mkude, Christopher
Ewards ni kati ya vijana ambao wamewahi kupata auw anaendelea kupata nafasi
kutoka kwa Poulsen.
Mwenendo wa Stars iliyo chini ya Poulsen unaleta majibu mawili.
Kwanza uzalendo kwa taifa badala ya kocha binafsi. Pili, inaonyesha hivi bila
ya kujali jina au mtu, Stars inaweza kusonga mbele.
Mwisho, hakuna timu inayoweza kwenda bila ya mabadiliko. Kwa kuwa
wakati wa Maximo ulifikia kikomo, ilikuwa lazima waje wengine na maisha yaendelee.
Mara nyingi mabadiliko yako hivi, yuko anayeanzisha lakini baada
ya hapo safari inaendelea na wengine wanaendelea kuyachangia zaidi kama ambavyo
ilivyo sasa. Watanzania tunapaswa kujiamini na kujua nini kinatakiwa kwa
maslahi ya nchi yetu.
Maximo alifanya kazi yake, sisemi ni mbaya, lakini leo Poulsen
anafanya kazi nzuri zaidi na anapaswa kupewa sapoti zaidi. Tunakumbushana tu.








0 COMMENTS:
Post a Comment