Na Saleh Ally
MWANZONI mwa miaka ya 1990 Pamba
ya Mwanza ilitua na dege mjini Tanga, baada ya saa chache wachezaji wake
walikuwa uwanjani tayari kucheza na Coastal Union yenye wachezaji nyota.
Mechi hiyo ilikuwa ngumu na muhimu zaidi kwa Coastal Union kwa kuwa
kama ingefungwa, badi ingeteremka daraja, mashabiki walijitokeza kwa wingi
Uwanja wa Mkwakwani.
Pamba wakati huo maarufu kama TP Lindanda hawakuwa watu wa mchezo, waliingia
uwanjani wakitaka ushindi bila ya kujali Coastal Union wanataka lipi.
Mwisho wa mechi, Coastal Union 0 na Pamba 1, bao pekee likiwa limefungwa
na Edward Hizza. Hasira zikawashinda nguvu mashabiki wa Coastal ambao walianza
kuwachapa ngumi na mateke wachezaji na viongozi wa Pamba.
Pamoja na Polisi kuingilia haikuwa kazi rahisi, waliondoka uwanjani
hapo ndani ya karandika kama vile wao ni mahabusu hata safari siku hiyo
ikaahirishwa, wakalazimika kuondoka siku iliyofuata chini ya ulinzi kwenda Dar
es Salaam ambako walitua na kujaza mafuta kabla ya kuanza safari ya kurejea
Mwanza.
Pamba ya Mwanza au TP Lindanda, wana Kawekamo haikuwa timu ya mchezo.
Uwezo wake ulikuwa juu lakini hata uongozi wake ulikuwa wa kitaalamu zaidi
kuliko hata klabu kongwe kama Yanga na Simba zinavyoendeshwa.
Pamba ya miaka ile, imefanya mambo mengi ya kusimuliwa kwa mlengo wa
mafanikio wakati Yanga na Simba zaidi ni sifa tu lakini hata mambo ya miaka
1980 yaliyofanywa na Pamba, leo hawawezi kufanya!
Kwenda na ndege mkoa mmoja, timu inatua na kucheza halafu wachezaji
wanarudi kwenye ndege na kurejea hakikuwa kitu cha ajabu au kigeni kwa Pamba.
Mara mbili wamefanya hivyo, walitua Songea, wakaifunga Majimaji,
halafu wachezaji wakaongozana kwenda ukweni ambako mchezaji mwenzao Rajab
Risasi alifunga ndoa baada ya hapo wakamchukua ‘mke wao’ na kupanda naye ndege
kurejea Mwanza.
Ndege hiyo ya Mwadui, Shinyanya ilikuwa ikiwabeba Pamba kutokana na
mkataba maalum kati ya Bodi ya Pamba na uongozi wa mgodi wa Fred Williamsons
& Sons.
Ingawa ilikuwa zamani, Pamba waliendesha mambo yao kisasa, leo utaona
Arsenal, Manchester City, mabingwa wa England Manchester United na timu
nyingine ndiyo wanafanya hivyo.
Arsenal wana mkataba na Shirika la Ndege la Emirates, Man City mkataba
wao na Etihad na Man United wako na Turkish Airlines. Pamoja na kujipatia
fedha, mashirika hayo yanahusika na usafiri wa wachezaji.
Kupata mabasi kutoka kwa wadhamini ni jambo zuri, lakini timu kubwa za
Ulaya hazitaki kuingia gharama ya kuendesha ndege zinaona ni kama
kujichanganya.
Ndiyo maana zinaingia mkataba na mashirika ya ndege ili kupata fedha
na kusafirishwa wachezaji wake katika mechi muhimu.
Pamba walikuwa wanatoka Mwanza mchana kwenda mkoa mwingine, saa tisa
wanakuwa uwanjani kukipiga bila ya uchovu na wanapiga ‘mtu’ halafu wanarudi
kwenye ndege na kurejea Mwanza.
Inawezekana Pamba haikuwa na mkataba na mgodi wa Mwadui kama ilivyo
kwa Man United au Arsenal. Lakini makubaliano ya kupunguziana au kukubaliana
kutumia ndege hiyo kilikuwa ni kitu kinachofanya kazi.
Yanga na Simba wanapaswa kuwa wabunifu, makampuni ya ndege yako
lukuki. Wanaweza kufanya mipango na kuingia nao mikataba kwa kuwashawishi
kutokana na utendaji au ubora wa kazi zao.
Wakifanikiwa, maana yake wataingiza fedha lakini lakini wataweza
kupata usafiri na kupunguza kusafiri na basi zaidi ya kilomita 1,000 kwenda
kucheza mechi.
Ubunifu wa Pamba miaka hiyo unaweza kufanyika kipindi hiki lakini
ukiwa umeboreshwa kulingana na kipindi chenyewe na ukawa msaada mkubwa.
Usafiri bora ni sehemu ya motisha kubwa kwa wachezaji, ni sehemu ya
huduma bora kwa wachezaji kama ilivyo kwa malazi, chakula na hata malipo
mazuri.
Pamba waliliona hilo, ndiyo maana timu yao ilikuwa imara na itabaki
kuwa gumzo kwenye historia ya soka ya Tanzania milele.
Ubora huo usingekuja kwa ndoto, maneno mengi, ubinafsi na kulalama kwa
kutotaka kukosolewa kunakofanywa na viongozi wa timu hizo kongwe ambazo maendeleo
ni pale yanapopatikana tu, hakuna mipango.
Inawezekana bado kuna viongozi wanaamini wachezaji kusafiri na ndege
ni anasa, badilikeni. Usafiri wa ndege ni kama unavyosafiri na basi au gari
binafsi lakini umuhimu na utofauti wake unajulikana.
SOURCE: CHAMPIONI








0 COMMENTS:
Post a Comment