April 21, 2013




Na Saleh Ally
MGOGORO wa kimuziki kati ya msanii Judith Wambura Mbibo ‘Lady Jaydee’ na kituo kimoja cha redio umezidi kuchukua kasi huku makundi mawili, kila moja likitengeneza ngome yake na kuamini linachoamini.

Kundi ambalo linamuunga mkono Jaydee na kumuona ni mkombozi, anazungumza kwa niaba yake na wasanii wengine, la pili ni lile linalobaki upande unaoshambuliwa, linatetea ngome yake.

Jaydee anashutumu kubaniwa nyimbo zake na kituo hicho ambacho kupitia mitandao kadhaa ya kijamii ameeleza wazi kuwa wanambania, wanaziponda lakini hata watangazaji wake wamekuwa wakionyesha chuki binafsi dhidi yake.

Jaydee pia aliwaponda wasanii Ben Pol na Linah anayetokea THT kwamba walishindwa kutokea kwenye uzinduzi wa video ya wimbo wake wa Joto Hasira, kwa madai walizuiwa na bosi wao.


Ujasiri huu wa Jaydee ndiyo kitu bora ambacho kimekuwa kikitakiwa kufanyika kutoka kwa wasanii, yaani wapigane kutetea muziki wa Tanzania hasa kama kuna watu au kundi la watu limejikita katika kuuangamiza.

Lakini ni tofauti kidogo, kwani wasanii wengi wamekuwa imara na kuwa tayari kujitetea wenyewe tu na si vingine. Nasisitiza mara nyingi, wao ndiyo wahusika wa kwanza na wanapaswa kuanzisha mapinduzi kuanzia kwao, mfano kusema naonewa si kitu kibaya lakini je, umewahi kupigania wanaoonewa?

Kujitetea pekee unaweza kufanya, lakini vipi utafanikiwa kama asilimia kubwa ya kundi la wanamuziki linaendelea kuonewa. Ukibaki hauonewi pekee na asilimia kubwa ya wasanii au wanamuziki inaonewa, kunaweza kuwa na mapinduzi sahihi?

Ndiyo maana nashangazwa kusikia Jaydee leo anaona ubovu wa kituo hicho, anathubutu kusema hadharani akionyesha wazi ameumia. Lakini miaka 10 au zaidi iliyopita, Jaydee alikuwa kimya na hakuwaza kusema kwamba kituo hicho kinawabania wasanii wengine na ‘kumtukuza’ yeye hata kama muziki wake haukuwa wa kiwango kilichokuwa kinazungumzwa.

Siwezi kusema muziki wa Jaydee ni mbaya, nimekuwa kati ya mashabiki wake. Lakini yoyote atanichekesha akisema nyimbo albamu zake zote alizotoa zilikuwa katika kiwango cha juu sana na ndiyo maana leo ni maarufu.

Hakuna asiyejua kwamba miaka nenda rudi, wasanii wamekuwa wanaongoza kwa unafiki, kutopendana wenyewe, kugeukana na hata kujenga makundi lukuki, ndiyo maana kila kukicha wamekuwa wakishambuliwa maana katika maisha yao hawana umoja.

Jaydee alianza kuwa mtangazaji katika kituo hicho baada ya kuacha kurap, akaamua kuachana na kurap na mwisho kuwa msanii wa nyimbo za kubembeleza, mara ya kwanza akianza kutikisa na albamu ya Machozi, Solo Thang anaweza kuhadithia vizuri kuhusu hili.

Kuanzia albamu ya Machozi, kituo hicho ndicho kilisimama kuhakikisha anakuwa bora hata kama muziki wake haukuwa ukimzidi kila mwanadada wakati huo.

 Angalia, kulikuwa wasanii kama Stara Thomas, Carola Kinasha ambao kiuwezo walikuwa juu kuliko Jaydee, lakini hawakupewa nafasi ya kutosha, badala yake Jaydee ambaye hakuthubutu kuwatetea hata kidogo akaendelea ‘kubebwa’ na watu wakaamini ni bora kuliko yoyote kwa upande wa akina dada au kina mama katika kuimba, haikuwa hivyo.

Angalia albamu ya Binti, karibu nyimbo zote zilikuwa na ujumbe mmoja, ulikuwa ukimshambulia mwaname mmoja ambaye alikuwa amemuumiza Jaydee. Takribani ujumbe wa nyimbo karibu zote ulikuwa ni mmoja, lakini ilibebwa na kuonekana ni moja ya albamu bora kabisa kuwahi kuwepo katika muziki wa Tanzania, kitu ambacho hakikuwa sahihi.

Wakati huo wasanii lukuki walilia kubaniwa, mmoja wao alikuwa ni Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ ambaye ndiye alimtambulisha mwanadada huyo alipomshirikisha katika wimbo wa Mambo ya Fedha, kabla ya hapo hakuwa na jina. Jaydee hakuwahi kuungana naye hata kidogo hata kwa mstari mmoja wa kumtetea au kuunga mkono kutetea muziki wa Tanzania, kuonyesha anapinga mwenendo wa wanaolazimisha kuwabagua wasanii au kufanya mambo kwa mabavu kwa kuwa wameshika mpini.

Hakuna aliyesikia kilio cha Sugu, wasanii wanaochipukia bila ya kujua wasemacho, kisa nyimbo zao zinapigwa redioni, ili kuonyesha shukrani za dhati wakaanza kutangaza Sugu anatapatapa na amekwisha kimuziki!

Ajabu, asilimia kubwa ya maneno yake ndiyo yanayozungumzwa leo, ndiyo yanatumiwa na kila msanii anayebanwa au kuhisi kaonewa. Angalia, hata Jaydee naye ameingia huko! Swali langu hapa je, Jaydee na wengine wanaolalamika, wamekwisha kisanii?

Ndiyo maana nasema, tasnia ya muziki hasa muziki wa kizazi kipya umejaza watu wavivu kufikiri, wenye mioyo ya ‘Kichina’, wasio na uwezo wa kuthubutu hata kidogo ambao wanasubiri wayumbe au kuumizwa wao ili wamtafute wa kumuangushia lawama.

Jiulize, kama Jaydee alibebwa kwa miaka 10, halafu leo analalamika atakuwa sahihi? Sitaki kumpinga kwa kuwa kuna kitu anakiona lakini ninaamini alikiona tokea mapema, akauchuna.

Bado nasisitiza, yeye na wengine wote wanaolia baada ya kuguswa wao nawaita wanafiki, wanapigana kwa ajili yao na si kwa muziki wanaoutumikia. Iwapo wangekuwa tayari kupambana kwa ajili ya muziki huo, msanii kama Jaydee asingeanza vita leo.

NARUDI KWA JAYDEE
Sijawahi kuingia naye katika malumbano zaidi ya miaka 10 tokea alipokuwa mwanahabari mwenzangu na sasa msanii. Lakini nathubutu kumueleza kuwa ni kati ya wasanii wasiojali muziki wa Tanzania na wanajiangalia wao zaidi.

Picha ya unafiki na kujiangalia mwenyewe inaonekana sasa ingawa takribani miaka mitano iliyopita nilianza kuinusa. Leo analia, anabaniwa na anauona moto unaounguza muziki wa Tanzania ulivyo mkali.

Naamini aliuona miaka kibao nyuma, lakini kwa kuwa alikuwa akitetewa hakuweza kuangalia kwamba rafiki zake, wasanii waliombeba kabla walikuwa wakiungua. Akaendelea kuwapita kwa raha zake mustarehe.

Tungeweza kumuita Jaydee ni mpambanaji kama angewakosoa hao anawakosoa sasa katika kipindi walichokuwa wamempa mbeleko yeye, basi kweli ingeonekana anapigania muziki wa Tanzania. Sasa anapigania chake tu!

Jaydee amefika mbali kimuziki, alikuwa bora jukwaani na nyimbo kadhaa na nyingi zikapewa ‘over promotion’ lakini bado ninaweza kumuita mkongwe. Ajabu alibaki chipukizi hadi leo katika suala la kutetea haki za wasanii na muziki wenyewe.

Sitaki kumkatisha tamaa kwa mapambano aliyoyaanza, ninaamini ana nafasi ya kuanza kuusaidia muziki ambao umemsaidia. Lakini ndiyo kipindi ambacho anaweza kupata machungu waliyopata wasanii wenzake kunyeshewa mvua na kuunguzwa na jua wakati akiwa kivulini kwa ‘msaada’.

Anachokifanya leo Jaydee ni nyongeza tu ya walichokifanya Sugu au Afande Sele au wasanii wachache walioamua kuwa wakweli au wale walioamua kuwa wabunifu kama Ambwene Yessaya ‘AY’, aliyekimbia vita ya redio na kuingia katika kurekodi video bora zilizoendelea kumng’arisha.

Simzuii, Jaydee kuendelea kupambana, lakini namuasa anachokifanya kama ni kwa ajili ya muziki akipozwa tena, asirudi nyuma.

Ninachomkumbusha, hata yeye amekuwa kundi moja na analowalaumu ambao angeweza kuwashauri mapema ‘ndani ya mjengo’ kama angekuwa na nia nzuri na muziki wa kizazi kipya.  Msisitizo ‘Joto Hasira’ liwe la kweli.

18 COMMENTS:

  1. Wakati mwingine tunaundiwa mashujaa wa uongo nasi kuwakumbatia. Ni vigumu sana kuujua unafiki huo hadi uwe mtu mwenye mitazamo huru. lakini ukiwa juu juu tu unaweza kuishia kumuhurumia JD.

    ReplyDelete
  2. KIUKWELI ULICHOANDIKA NI SAHIHI KIAKA ANGU ALLY,UMENIFUMBUIA MACHO,NADHANI HAYA YOTE YAMEENZA BAADA YA MUMEWE KUHAMA KATIKA KITUO HICHO CHA RADIO.

    ANALIENJOY SANA,SASA NAONA NABANIWAM,ILA TUSIMKATISHE TAMAA AENDELEE KUPAMBANA,KAMA ULIVYONENA HATA AKIRUDI KUNDINI....

    ReplyDelete
  3. kaka umenena. Kuna unafiki mkubwa sana katika hili. Nimependa vile ulivyoweka wazi situation nzima tena kihistoria. Wakati umefika kama kuna msanii mpambanaji basi na apambane sasa sio kusubiri mpaka abaniwe

    ReplyDelete
  4. Joto hasira........ame copy na kupaste wimbo wa kijita......asijifanye anajua kutunga.Katweet jana Mungu si Ruge wala Kusaga...nikamuuliza hata wewe umetendwa?katumwa na mumewe na wala si mpiganaji wa kweli.....linah ni kipaji zaidi yake...akipata anachotafuta atanyamaza.

    ReplyDelete
  5. Ally mimi ni mmoja wa wadau wa muda mrefu wewe ni mmoja wa watu uliochukua muda mrefu sana kuliongelea hili. kwani lina sura mbili we umechagua moja. Kwa nini usiandike makala ambayo itauliza Ruge ama clouds kwa nini ni iwe wao tu wanaolalamikiwa. Umewahi kujua kwa nini Marlaw hayupo THT, Lady Jd alitumiwa kama anavyoweza kutumiwa mtu yeyote je ni wasanii wangapi sasa hivi wanatumiwa. Najua utakuwa unajua kama Dudu baya alitumiwa kumpiga Nice Diamond Jubileee na hao hao je hilo nalo hulijui

    ReplyDelete
  6. Hapo kuna ukweli kabisa jde alibebwa sana,, nadhani ni wakati wake kujua maumivu ambayo wenzake walikuwa wanayapata,, bravo bwana saleh siku zote nilikuwa najiuliza lkn leo umenipa kitu,, Jde hatishi kiviiile sema ni jinsi anavyopata promo na kuonekana bora, tuna wasanii wengi tu wa kike na wanafanya vizuri lkn hawapewi shavu kama yeye,

    ReplyDelete
  7. kaka salehe kama ulianza kunusa unafiki wa lady jaydee mbona hukuandika mapema kwa miaka yote hiyo kumi ulisubili aanze kupambana ndo umkatishe tamaa nina imani kavumilia sana ndo maana kaamua kuongea hata wakina Nyerere walivumilia sana utawala wa kikoloni hatimae wakachoka wakapigania uhuru
    SO unataka kusema na nyerere nae alikua ni........kwa maana alifanya kazi na wakoloni ALUTA CONTINUE JIDE

    ReplyDelete
  8. SWALI KWAKO WEWE ALLY, WE NI MUANDISHI KAMA UNAVYOJIITA, KULIKO KUKANDAMIZA SEHEMU MOJA JE UMEJIULIZA HIZI TUHUMA ANAZOZITOA JIDE NI ZA KWELI AMA UONGO ?????THEN BALANCE STORY, MI NAKUONA WEWE NI MMOJA YA WAANDISHI MAKANJANJA KAMA ALIVYOSEMA ROMA, NA UTAKUWA UNA MASLAHI BINAFSI YA KUKUFANYA UISHI MJINI HAPA, NIKIAMBIWA NITAJE WAANDISHI MIA BORA TANZANIA WE HAUMO.

    ReplyDelete
  9. mmh, kazi kweli kweli

    ReplyDelete
  10. WATU BWANA TU WA AJABU SANA, NAWASHANGAA HAWA WATU WA NNE WA MWISHO KWA COMMENT ZAO AMBAO NI WAZI WANAMTETEA JAYDEE. HUYU MMOJA ANASEMA NI UNBALANCED STORY...HII SIYO JUST A STORY KWA MAANA YA HARD NEWS, BALI NI FEATURE STORY AMBAYO MWANDISHI ANAAISHI ANAKUWA NA UHURU WA KUANDIKA ANACHOTAKA, HAKUNA KUBALANCE STORY HAPO FOR YOUR INFORMATION.

    LAKINI KWA UPANDE MWINGINE TUZUNGUMZE UKWELI, HATA KAMA TUNAMPENDA MTU. MWANDISHI HAKUSEMA KWAMBA ANACHOFANYA LADY JAYDEE NI KIBAYA, NA WALA HAMKATAZI KUENDELEA NA ALICHOKIANZISHA, BALI ANAZUNGUMZIA KUCHELEWA KUFANYA HIVYO TANGU MAPEMA NA KWAMBA HATA HAO WA SASA WAJIFUNZE ILI YASIWAKUTE YANAYOMTOKEA LADY JAYDEE. TUKUBALI KUKOSOLEWA, TUSONGE MBELE

    HUYU MWINGINE NAYE ANAMWITA SALEH ALLY NI KANJANJA, NADHANI AELEWI KITU CHOCHOTE, UKITAJA KATI YA WAANDISHI BORA WATATU WA MICHEZO, SALEH ALLY ATAKUWA KATI YAO.

    ReplyDelete
  11. Nice Article bro,hao wasomaji hapo juu nafikiri hawakufahamu kuwa wewe ni mwandishi bora hapa nchini na usiyeyumbishwa na mtu.Hiii Feature yako ipo fair> Aluta Continue

    ReplyDelete
  12. makala yako nzuri kaka unauwezo mkubwa sana wa kuandika kwa lugha ya picha na fikra zaidi ndivo muandishi anavotakiwa kutatua hoja na wasiwasi wa kihabari juu ya hoja tata kama hizi bila shaka nakufahamu vzuri salehe.nakupongeza ila bado na wasiwasi na uwezo wako juu yakutumikia kundi flani sipendi na sifurahii et ukipewa sifakubwa et wenikati ya wandishi wasio yumbishwa kiukweli japo sipo tz lkn nauhakika kwa tz bado hajazaliwa mwandishi asiye yumbishwa au labda yupo shule wengi ni watumwa navijakazi waserikali hebu gusa siasa tuone kama hauyumbishwi watu tunaocoment tuangalie nasifa tunazo wapa hawa waandishi..ndio maaana taifa letu linaendelea kuwa nawatu wazembe nawasio taka kuambiwa ukweli.

    ReplyDelete
  13. Watu wengine wanapaswa kupigwa bastola Saleh kajanja anamfaham kweli?? Eti Unbalanced mwambie arudie kusoma kama makala haijafusa pande zote zinazovutana. Heko na saluti bro Saleh

    ReplyDelete
  14. Alichokifanya SALEH ni kutumia uhuru alionao katika uandishi na tunachokifanya wachangiaji ni kutumia uhuru wetu wa kutoa mawazo so sioni tatizo kuponda au kumkosoa SALEH katika makala yake.
    kuna mchangiaji mmoja ametoa mfano mzuuri wa baba wa Taifa katika kupigania uhuru alikaa nao lakini mwisho wa siku akapambana nao japo si kwa kumwaga damu.
    Saleh kazungumzia unafiki uliopo katika mapambano ya JIDE NA KITUO HUSIKA na kujinadi kua alianza kuuona unafiki huu miaka mitano iliyopita kwa hiyo katika hili anakubali moja kwa moja kua hata yeye mwenyewe alikua ni MNAFIKI MWANZONI kwa kuufumbia macho unafiki aliouona tangia mwanzo,,nadhani angetumia kalamu yake kuuvumbua unafiki huu kipindi hicho angeliwashtua wengi ikiwa pamoja na huyo JIDE ambaye pengine alilewa na mbelelko inayozungumzwa.
    Ninachokiona sasa Tanzania sasa inaamka hasa vijana mapambano yaendelee kila mtu kwa sekta yake aliyopo WAANDISHI WAPIGANIE UHURU WAO WA KUPATA NA KUTANGAZA HABARI kuwafumbua macho wananchi na sisi tupiganie haki katika mahala petu.BIG UP JIDE (ANACONDA) mwanzo mzuri....BIG UP SALEH Unakipaji.

    ReplyDelete
  15. Hujamtendea haki Jide, huwezi kuwalaumu wapinzani wa ccm kwa vile tu hawakuzaliwa wapinzani na walianzia karibu wote ccm. siku Dr. Slaa alipotoswa CCM ndipo alipokuwa huyu tuliyenaye. Hata wewe kama sio mmiliki wa hayo magazeti unayoyaandikia, kunasiku takuja huku na harakati dhidi ya mabosi wako unaowapeti leo huku wenzako wakilalamika. hauko fair hata kidogo, wewe ni mnafiki kama wanafiki wote tu

    ReplyDelete
  16. hakuna jipy usiwatetee radio wafu

    ReplyDelete
  17. Salehe Al;ly kanjanja tu! tuel;eze ulisoema wapi masuala ya habari baada ya kuacha kucheza disko mwanza?

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic