Yanga wameanza kusukuma tuhuma kwa Shirikisho la Soka
Tanzania (TFF), kwamba lina njama za kuwafanyia hujuma ili Azam FC iweze
kuwafikia katika msimamo wa Ligi Kuu Bara, ikiwezekana kuwapita na kutwaa
ubingwa.
Yanga wanaamini Azam FC ikitangulia kucheza mechi yao dhidi
ya African Lyon na kushinda, basi pengo litakuwa ni pointi tatu tu na baada ya
hapo ‘watawekeza’ nguvu katika mechi yao inayofuatia na ‘kuwamaliza’ ili
wawafikie.
Ukiangalia madai ya Yanga, yanaweza kuwa na hoja ya msingi
kwa kujiuliza kwa nini TFF wakurupuke na kubadili ratiba haraka bila ya
kuzitaarifu klabu katika muda wa kutosha?
Siku 14 kabla ya mechi unaweza kuwa wakati mwafaka, lakini
kwa nini leo waibuke na kusema ratiba imebadilishwa na sababu zao za msingi ni
Televisheni ya SuperSport kutaka kuonyesha mechi hizo moja kwa moja?
TFF imetangaza Super Week na mechi zilizofanyiwa mabadiliko
ni zile za kuanzia Aprili 11 hadi 18, wakati ile ya watani, Yanga na Simba, Mei
18, inabaki kama ilivyo.
Katika Super
Week, mabadiliko yapo kwenye mechi ya Azam dhidi ya African Lyon ambayo
imesogezwa mbele siku moja hadi Aprili 11, Yanga dhidi ya Oljoro iliyokuwa
ichezwe Aprili 10, sasa imekwenda hadi Aprili 13 (kesho).
Azam na Simba
imesogezwa siku moja mbele hadi Aprili 14, Coastal Union na JKT Ruvu
itakayochezwa Aprili 16 badala ya Aprili 10. Wakati mechi nyingine
zilizosogezwa mbele ni Mgambo Shooting na Yanga ambayo imesogezwa siku nne
mbele hadi Aprili 17, sawa na ile ya Mtibwa dhidi ya Oljoro.
Yanga wana hoja
za msingi kuhusiana na utaratibu kutofuatwa, ingawa ni vigumu kuamini kila
wanachokisema kuhusiana na TFF na Azam kwa kuwa ni kitu kinachohitaji
uthibitisho zaidi, suala ambalo ni gumu pia.
Lakini kwa
TFF ambayo ilitoa hoja yake kwamba inafanya vile kwa lengo la kuipa SuperSport
hamu ya kudhamini Ligi Kuu Bara mwakani, lazima iwe na mipango na kuamini hata
kama wao ndiyo wapangaji wa ratiba, lakini timu zina haki pia.
Ndiyo, timu
zina haki ya kujua ratiba mapema, vivyo hivyo kama kutakuwa na mabadiliko basi
zitaarifiwe mapema kwa kuwa zinakuwa katika maandalizi na zinatumia mamilioni
ya fedha.
TFF
isidanganye kwamba kwa kuwa wao ndiyo wanaosimamia mpira wa Tanzania, basi wanaweza
kufanya wanachotaka bila kuangalia wengine wanaathirika vipi.
Lakini pia
siamini kampuni kubwa na yenye uzoefu kama SuperSport wamebadilika kiasi hicho
na kufanya mambo kwa mtindo wa zimamoto. Nasema hivyo kwa kuwa nimewahi kupata
nafasi ya kufanya nao kazi kwa miezi kadhaa, tena makao makuu pale
Johannesburg, Afrika Kusini.
Najua namna
mpangilio wa kazi zao unavyokwenda, hivyo siamini kama wamebadilika na kushuka
kiasi hicho cha kufikia kufanya mambo kwa kubabaisha na kukurupuka ndani ya
wiki moja, eti wanataka kuripoti mechi fulani.
Ninaamini
kama TFF ingeomba kitu kwao kwa mtindo huo wa kukurupuka, lazima wangeambiwa
kuna ratiba ya mechi imepangwa kwa mwaka mzima. Ndiyo maana nashangazwa nao.
Lakini
nawashauri TFF kwamba bado hawapaswi kuvuruga tu mambo wanapoona wanaweza
kufanya hivyo kwa kuwa wao ndiyo viongozi. Lazima waangalie maumivu ya timu
husika.
Lakini pia
waondoe lawama kama hizo kwamba wanahusika kuzisaidia baadhi ya timu kwa kuwa
mwendo wao na mambo wanayoyafanya ndiyo vinazaa kinachozungumzwa.
Kusaidia
ligi ipate mkataba mzuri kutoka SuperSport ni jambo zuri, lakini kufuata
utaratibu ni jambo zuri zaidi ambalo lingesaidia pia kuondoa hisia tata na
imani za dharau au ubabe kutoka upande mmoja kwenda mwingine.
HOJA
SOURCE: CHAMPIONI NEWSPAPER
0 COMMENTS:
Post a Comment