Na Mwandishi Wetu
HATUA za awali za kumsaka Redd’s Miss Tanzania sasa
zinaanza kushika kasi, wakati wiki hii kutakapokuwa na kinyang’anyiro katika
vitongoji kadhaa vya kusaka warembo wao.
Kazi kubwa itaanza Morogoro, wakati atakaposakwa Redd’s Miss High
Learning atakayeuwakilisha mkoa huo katika kumpata mrembo kutoka Vyuo vya Elimu
ya Juu, shindano litakalofanyika kwenye Ukumbi wa Sirvoy.
Wakati Morogoro Miss High Learning akipatikana kesho, shughuli pevu ipo
keshokutwa (Jumamosi) pale kutakapokuwa na shindano la kumsaka Redd’s Miss
UDOM, litakalofanyika katika Ukumbi wa Kilimani, Dodoma.
Siku hiyo pia atapatikana mwakilishi wa vyuo vya elimu ya juu kutoka
Kagera na Mwanza, shindano ambalo litafanyika Yacht Club, Mwanza.
Akizungumzia kuhusu Redd’s Miss Morogoro High Learning, mratibu wa
shindano hilo, Verdian Kamugisha alisema kila kitu kimekamilika na kutakuwa na
burudani za kufa mtu.
“Tumekamilisha kila kitu na warembo wote wako katika hali nzuri na
kutakuwa na burudani za kumwaga, wakazi wa Morogo wanatakiwa kuja kwa wingi
kushuhudia kile kitakachotukia,” alisema.
Mratibu wa Shindano la Redd’s Miss UDOM, Rachel Matina naye alisema kila
kitu kwao kipo tayari na watu wanatakiwa kufika kwa wingi kushuhudia jinsi
warembo kutoka Chuo Kikuu Dodoma, walivyopania kulitwaa taji la Redd’s Miss
Tanzania mwaka huu.
Joseph Rwebangira wa anayeratibu shindano la wanafunzi wa Vyuo vya Elimu
ya Juu kwa mikoa ya Kagera na Mwanza naye alikiri kukamilika kwa maandalizi
yote na kutakuwa na burudani za kila aina siku ya onyesho.
Upande wa kanda ya kaskazini mwa nchi kutakuwa na shindano la kumsaka
mrembo wa kitongoji cha Hai ambapo shindano hilo linatarajiwa kufanyikia katika
ukumbi wa Hotel ya Snow View na mkoani Mara katika kitongoji cha Tarime
shindano litakuwa katika ukumbi wa JJ Club na maandalizi kwa sehemu zote husika
yameshakamilika kwa kiwango kikubwa.
Redd’s Miss Tanzania kwa sasa inadhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania
(TBL) kupitia kinywaji chake cha Redd’s Original.







0 COMMENTS:
Post a Comment