April 29, 2013




Wiki iliyopita, Kocha Mkuu wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Kim Polusen alitangaza kikosi cha pili cha timu hiyo ambacho kilichukua wachezaji kadhaa waliokuwa wameonyesha uwezo wao katika mechi za Ligi Kuu Bara.

Wachezaji wengi walioteuliwa na Poulsen ni wale waliokosa nafasi katika kikosi cha kwanza cha Taifa Stars kutokana na ushindani mkubwa wa namba uliopo.

Wazo la Poulsen ni zuri sana, huenda kama liliwahi kufanyika lakini kwa makocha lukuki waliopita hawakuwahi kupendekeza suala hilo.

Kwanza niseme ninampongeza Poulsen kutokana na wazo hilo, lakini pia Shikirisho la Soka Tanzania (TFF) ambao wameona ni jambo la kiungwana na linaweza kuwa na faida hapo baadaye.


Lakini kuna kitu kingekuwa kizuri zaidi kwamba kwa vile katika benchi la ufundi la timu kubwa, Poulsen ana wazalengo kama msaidizi wake, Sylvester Marsh na kocha wa makipa, Juma Pondamali, basi ulikuwa wakati mzuri wa kufanya kazi na wazalendo wengine.

Kwamba badala ya kuendelea kukinoa kikosi hicho cha pili kwa kushirikiana na Marsh na Pondamali, basi angeteua wazalendo wengi wawili ambao atafanya nao kazi. Mfano, msaidizi wake anaweza kuwa Abdallah Kibadeni wa Kagera Sugar na Kocha wa Makipa akawa, Ali Bushiri wa Zanzibar.

Hii itasaidia mambo mengi sana, kwanza ni kwake Poulsen kuongeza wigo wa kufanya kazi na makocha wazakendo, huenda akajifunza zaidi kuhusiana na uwezo wao.

Lakini atajua mambo kadhaa kwa kuwa mfano Kibadeni ni kocha mkongwe na mwenye uwezo mkubwa wa kung’amua vipaji vya wachezaji wa Kitanzania na kuna utuhibitisho wa mambo mengi kama ilivyo kwa Bushiri ambaye amewahi kuitumikia Stars kwa mafanikio makubwa ukiachana na kwamba alikuwa kipa mahiri enzi zake.

Haina maana niliowataja mimi ndiyo wamepitishwa, walikuwa ni mfano tu. Lakini ukiachana na Poulsen kufaidika, lakini taifa letu nalo litafaidika pia.

Tunakubaliana kuwa Poulsen ni kati ya makocha wazuri wa kigeni ambao tumewahi kuwapata, kufanya kazi na wazalendo maana yake analifadisha taifa letu kwa kuwa nao watapata mambo kadhaa kutoka kwake.

Hivyo kama katika kikosi kikubwa atakuwa na wazalendo tofauti na wale watakaokuwa timu B, basi wigo wa faida utakuwa mkubwa zaidi kwa kuwa watakayojifunza, watayarudisha katika timu zao na kufaidisa wengi zaidi.

Ukiachana na hivyo, inawezekana kabisa siku moja Tanzania ikafikiria kuanchana na makocha wageni na kuwaamini wazalendo ambao watakuwa ‘wamenyonya’ mambo kadhaa kutoka kwa wageni na mwisho wakawa msaada kwa soka ya Tanzania.

Mwisho niwapongeze waliochaguliwa katika kikosi hicho cha pili cha Taifa Stars. Inawezekana kabisa walikuwa wakitamani siku moja kuichezea Taifa Stars kubwa na hiyo ndiyo njia ya kufika huko.

Kitu kikubwa wanachotakiwa kufanya ni kazi, waondokane na majungu, hisia tata na ushabiki wa timu badala yake wafanye kazi ya kiushindani kwa ajili taifa na wao wenyewe. Kila la kheri.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic