May 27, 2013


Baba Ubaya akimwaga wino mbele ya Kaimu Makamu Mwenyekiti wa Simba, Joseph Itang'are aka Mzee Kinezi

Na Mwandishi Wetu
UONGOZI wa Simba umeonyesha umepania kufanya mabadiliko makubwa katika kikosi chake msimu ujao baada ya kusajili wachezaji watatu pamoja katika usiku mmoja.

Simba imewasajili kipa Andrew Ntalla kutoka Kagera Sugar ambaye atapambana na Juma Kaseja katika nafasi ya kipa namba moja atakuwepo Simba pamoja na Abel Dhaira raia wa Uganda.
 
Pazi akimwaga wino..
Imemsajili beki wa kushoto Issa Rashid maarufu kama Baba Ubaya katika nafasi ya beki wa kushoto ambayo zaidi alikuwa anategemewa Amir Maftah ambaye yuko kwenye mgogoro na uongozi wa Simba.

Mchezaji wa tatu ni Zahoro Pazi, mtoto wa kipa na kocha wa makipa wa zamani wa Simba, Iddi Pazi ambaye alikuwa anakipiga kwa mkopo JKT Ruvu akitokea Azam FC.
 
Ntalla akijifunga Simba...
Simba inaonekana imemchukua Pazi ili kuziba pengo la Mrisho Ngassa aliyekwenda Yanga, Ngassa alikuwa anacheza zaidi katika winga ya kushoto na mara kadhaa kulia nafasi ambazo mchezaji huyo mpya anazimudu.

Wachezaji wote watatu walianguka saini mbele Kaimu Makamu Mwenyekiti wa Simba, Joseph Itang’are maarufu kama Mzee Kinesi.
 
Messi kutoka Coastal na baba yake mzazi wakiwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Pope.
Simba inaendelea kufanya usajili kimya kimya ikilenga kuimarisha kikosi chake kwa ajili ya msimu ujao ikiwa imelenga kurejesha heshima baada ya kuishia katika nafasi ya tatu katika msimu uliomalizika Yanga kutwaa ubingwa na Azam FC kushika namba mbili.


Baba Ubaya alikuwa ameingia mkataba wa miaka miwili sawa na Pazi wakati Ntalla aliyekuwa kipa namba moja wa Kagera Sugar iliyoshika nafasi ya nne ikiwa chini ya Abdallah Kibadeni aliyerejea Simba, yeye amesaini miaka mitatu na wekundu hao wa Msimbazi.

Tayari Simba ilifanikiwa kumsajili winga wa Coastal Union Ibrahim Twaha maarufu kama Messi ambaye mkataba wake ulisainiwa mbele ya baba yake mzazi na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Pope.

Simba imekuwa ikifanya kila namna kuhakikisha usajili wake unakuwa bora ili kufanikiwa kutwaa tena ubingwa au kuishia katika nafasi ya pili msimu ujao ili ishiriki michuano ya kimataifa na kurejeshe heshima yake iliyopotea msimu huu.

Bado Simba inahaha kusajili beki wa kati pamoja na mshambuliaji wa kati, nafasi ambayo imewasumbua kwa kipindi kirefu kwa karibu msimu wote uliopita, hasa baada ya Kelvin Yondani kutua Yanga na Mzambia, Felix Sunzu kushindwa kuonyesha cheche.

SOURCE: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic