Na
Mwandishi Wetu
WAJUMBE wa
kamati ya Marejeo ya klabu ya Simba, juzi walikutana na Profesa Tolly Mbwete wa
Chuo Kikuu Huria (Out) kujadiliana kuhusiana na mpango wa uendeshaji wa klabu
hiyo kisasa ‘strategy planning’.
Katika
kikao hicho kilichofanyika Kunduchi jijini Dar es Salaam, Simba walijadili
masuala kadhaa ikiwa ni pamoja kufumua mfumo wa sasa, kuangalia faida ambazo
Simba zinaweza kutumika, mapungufu na nini cha kufanya ili mambo yaende
kitaalamu katika uendeshaji wa klabu hiyo.
Wajumbe wa
kamati hiyo waliohudhuria ni pamoja na Crescentius Magori, Omari Gumbo, Francis
Waya, Honest Njau, Mulamu Ng’ambi, Michael Wambura, Evans Aveva na wengine
ambao walijadili masuala hayo.
Katibu Mkuu
wa Simba, Evodius Mtawala alisema kikao hicho kilikuwa na mafanikio makubwa na
walipiga hatua katika mjadala huo.
“Profesa
Mbwete ndiye aliongoza majadiliano hao na timu yake kwa kuwa wao ndiyo wana
utaalamu na uzoefu mkubwa kuhusiana na masuala hayo. Lengo ni kuibadilisha
Simba ili iendeshwa kitaalamu zaidi.
“Tuliangalia
mambo kadhaa, hapa Simba ilipo, tunakwenda wapi. Kuna kitu kinaitwa Swot
analysis. Yaani Simba ikiamua kwenye kibishara, ina nini kinachoiwezesha kupata
fedha, mazingira, nini matatizo au udhaifu na mengine mengi.
“Kwa kifupi
ni mchakato wa kuweka mambo kitaalamu zaidi tena kwa programu ya miaka mingi
baadaye. Simba itakuwa inajua nini kinatakiwa badala ya kukurupuka kila mwezi
kupanga cha kufanya.
“Bado
mchakato unaendelea na tutawataarifu nini kinaendelea,” alisema Mtawala ambaye
ni katibu mkuu kijana zaidi kuongoza katika klabu kubwa kama Simba.
Iwapo Simba
itakamilisha mpango huo chini ya Profesa Mbwete, itakuwa klabu ya kwanza nchini
kutumia mfumo huo ambao hutumiwa na klabu kubwa za Ulaya, Marekani na Asia, pia
makampuni makubwa dunia.
0 COMMENTS:
Post a Comment