WAZEE wa
zamani wa klabu mbili kongwe za Yanga na Simba walikuwa wakiangalia sana
mapenzi kama muongozo wa utumishi katika klabu zao.
Dunia
inakwenda inabadilika kutokana na utandawazi, utaona mfumo huo wa wazee hao wa
zamani unaenda unapotea, ingawa ukichunguza utagundua hata kama waliongozwa na
busara, bado walikuwa watu bora waliofikiri mbali zaidi.
Kwa
wachezaji wanaocheza siku hizi, suala la mapenzi halina nafasi kubwa na badala
yake kazi au fedha ndiyo imechukua nafasi kubwa.
Kama ni
fedha, basi si lazima mchezaji awe na mapenzi makubwa kwa timu anayokwenda
kuichezea, badala yake weledi inabidi uchukue nafasi zaidi. Kwamba awe mtu
makini na anayefanya mambo yake si kwa kufurahisha watu au kutanguliza siasa.
Biashara
kati ya Simba na kiungo nyota, Mrisho Khalfan Ngassa, ilikuwa haina umakini,
kila upande ulifanya mambo ikionekana wazi siasa na fedha ndizo ziliongoza ‘mchezo’.
Utaona kama
ni mapenzi kama yale mapenzi ya wazee wa zamani wa Yanga na Simba, basi Ngassa
asingepata nafasi ya kucheza soka Simba, hili ni kosa la viongozi wa Msimbazi
kumchukua.
Lakini kama
ni suala la utandawazi, basi Ngassa pia hakuwa mtu makini kwa kuwa alijua wazi
anakwenda sehemu ambayo hakuhitaji kucheza na badala yake fedha ndizo
zilimvutia lakini mwisho akashindwa kuwa ‘professional’.
Simba
ilitanguliza siasa, Ngassa akatanguliza fedha na mwisho muunganiko wao ukawa ni
wenye mashaka makubwa kila siku zilivyokuwa zikisonga mbele.
Taarifa
zilieleza kuwa, Azam FC waliamua kuachana na Ngassa mara baada ya kuibusu na
kuivaa jezi ya Yanga huku bado akiwa mchezaji wao, tena alivaa juu ya jezi ya
Azam FC.
Lakini ili
kumuumiza moyo, wao wakahakikisha kama wakimtoa kwa mkopo, basi haendi Yanga,
timu ambayo ameonyesha analazimisha kurudi kwa kuwa ndiyo ilimuuza Azam FC kwa
Sh milioni 98.
Wakafanya
mazungumzo na Simba, walijua wazi huko asingehitaji kwenda. Wakafanikiwa kwa
kuwa Simba nao walikuwa katika hatua za kujibu mapigo ya kuchukuliwa Kelvin
Yondani, hivyo ikawa ni siasa na Ngassa akatua Msimbazi huku ikionyesha wazi
alijua anakwenda ‘kupumzika’ kwa muda kabla ya kurudi Yanga, hasa kwa kuwa
alikuwa hatakiwi tena Azam FC.
Siasa:
Kulikuwa na
kila dalili za Simba kulazimisha kumpata Ngassa kama sehemu ya kuwaonyesha
mashabiki wao kazi imefanyika.
Lakini
ilionekana Simba walimtaka Ngassa ikiwa ni kama sehemu ya kuziba kosa lao la
kufanya uzembe na kumuachia beki Kelvin aondoke na kutua Yanga.
Hivyo,
pamoja na kuwa na taarifa kwamba Ngassa alizungumza na Yanga na kufikia
makubaliano, Simba waliingilia kati kama sehemu ya mashindano ya kukomoana.
Inawezekana
kabisa Simba walijua Ngassa hakuhitaji kwenda Msimbazi, lakini wakataka
kuonyesha tu. Hiyo ndiyo siasa badala ya maslahi zaidi.
Kumsajili
mchezaji aliyechezea Yanga si kitu kibaya, lakini suala la yuko tayari kwa
dhati bado linabaki kuwa muhimu badala ya kumlazimisha aipende sehemu kwa
ushawishi wa fedha.
Mazungumzo:
Yanga
walisema kwamba wao walianza mazungumzo na Ngassa ajiunge nao baada ya mkataba wa
Azam FC. Lakini Simba wakaingilia kati na kuzungumza na Azam FC ili wamchukue,
kweli wakafanikiwa.
Utaona hapa
ni uleule usajili wa kuonyeshana, lakini si mipango hasa ya kipi wanakihitaji
na kukiamini. Kwamba ‘kuipiga bao’ Yanga ndiyo kitu muhimu. Siku zote usajili
wa namna hii hauna faida na sasa kinachotokea kinaonekana.
Ushahidi:
Ngassa
alionyesha hataki kwenda Simba kwa vitendo, aliibusu jezi ya Jangwani katika
mechi ya Kombe la Kagame wakati bado ana mkataba na Azam FC.
Alifanya
hivyo mbele ya umati wa watu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar. Vipi Simba siku
chache baadaye inamshawishi na kumchukua, wakati hisia zake alizianika
hadharani?
Lazima walifanya
hivyo si kwa sababu ya uwezo wake, bali ni kuwakomoa Yanga na baadaye uwezo
ungefuatia!
Kutomuamini:
Pamoja na
kwamba Simba ndiyo walitumia ushawishi mkubwa kwa Ngassa atue Msimbazi huku
wakijua wazi hakuwa na mapenzi nako, wao ndiyo waliishi naye maisha ya ‘magutu’!
Magutu ni
hali ya kutoaminiana, muda wote walikuwa na hofu na hata uchezaji wake walikuwa
wakiufuatilia kwa karibu kuliko mchezaji
mwingine.
Mara nyingi
kila Ngassa alipokosa bao, wapo viongozi wa Simba waliamini amefanya makusudi
na mjadala ukaendelea na siku nyingine kukosa huko kukatumika kama kumbukumbu
ya makosa.
Sasa kuna
haja gani ya kuishi na mtu unayeamini hakuhitaji, zaidi ni kujiongezea maisha
ya hofu tu!
Somo kwa
Ngassa:
Ngassa ni
mmoja wa wachezaji bora waliowahi kutokea Tanzania, hakika anastahili sifa.
Lakini bado
kuna haja ya kujifunza uongozi wa soka na kufanya mambo yaende kitaalamu zaidi.
Kubusu jezi
ya Yanga wakati akiwa na mkataba na Azam FC mbele ya watazamaji lukuki hakikuwa
kitendo cha kiungwana. Inawezekana mapenzi na Yanga ni kitu binafsi, lakini
kazi hasa suala la kuheshimu mikataba lina misingi yake.
Mtu makini
anaweza kuwa bora katika heshima ya mkataba alioingia. Lakini bado inakuwa
hatari kwa Ngassa kwa maana ya kusaini Yanga akiendelea kuitumikia Simba.
Inawezekana
ikaonekana ni kawaida, lakini Ngassa ni mchezaji mkongwe na makini, hakupaswa
kufanya hivyo.
Inawezekana
kabisa angeyaendesha mambo yake kitaalamu zaidi kuliko alivyofanya hivyo. Kuna
haja ya yeye kuyaangalia hayo kwa kutafakari zaidi kwa kuwa hata Yanga siku
moja wanaweza kuwa na hofu naye kwamba huenda akasaini na timu nyingine wakati
akiwa nao au huenda akaibusu na kuivaa jezi ya timu nyingine tena kwa kuwa kama
mapenzi, yana wigo mpana yanaweza kuwa yale ya dhati tu au hata yanayoendeshwa
na fedha.
Kilichotokea
kwa Ngassa na Simba kinaweza kuonekana ni kitu cha kawaida, lakini ni zaidi ya
darasa kwa timu zote zilizohusika na zilizoshuhudia mchezo huo pamoja na
mchezaji mwenyewe.
Vizuri
siasa isiwe muongozo wa kufanya mambo katika soka, badala yake mipango na
uhitaji sahihi ndiyo vitumike kusukuma mambo.
Fedha
walizotumia Simba kumpa Ngassa huenda wangeweza pia kuwatengeneza vijana kama
ambavyo wamekuwa wakifanya sasa, wasingekuwa katika presha kama ambayo
wanaipata na mwisho inawasumbua kwa kuwa kila msimu inaonekana Yanga wanapata
ushindi dhidi yao kwa kumchukua mchezaji wanayemhitaji sana!
SOURCE: CHAMPIONI NEWSPAPER
0 COMMENTS:
Post a Comment