Waitaliano
wanatumia neno calico derby, wakimaanisha mechi ya watani wa jadi, mfano katika
Serie A zinapokuwa zinakutana AC Milan na Inter Milan, kawaida vituko vinakuwa
lukuki.
Hapa
nyumbani tunasema mechi ya watani wa jadi, zinapokutana Yanga na Simba, hakuna
ubishi ndiyo mechi kubwa zaidi kuliko nyingine zote Afrika Mashariki.
Utaona
maandalizi ya mechi hiyo yanakuwa tofauti na nyingine zote, wachezaji wanapata
huduma na ofa za kila namna, ili mradi kila upande unataka kushinda katika
mechi hiyo bila ya kujali kama ni katika Ligi Kuu Bara, basi ushindi wake ni
pointi tatu na mabao mawili kama ilivyo ushindi dhidi ya Ruvu Shooting au
Polisi Moro.
Hakuna
anayeweza kuzishusha calico derby zirudi na kulingana na mechi nyingine kwa
kuwa zina ujazo wa mambo mengi na historia inaonekana kusomeka zaidi
zinapofikia kupambana.
Kitu
ninachotaka kukizungumzia ni namna mambo ambavyo yamekuwa yakienda, viongozi wa
kila upande katika timu hizo wamekuwa wanabadilika na ikiwezekana kumuona kila
mtu ni msaliti kwao.
Hisia za
kuona kama wanasalitiwa ndiyo zimekuwa muongozo, hali ambayo inafanya kambi za
timu hizo kuwa kama ubalozi wa nchi fulani ambao una hofu ya kulipuliwa na
mabomu.
Ulinzi
unaongezwa, kutoaminiana kuanzia ndani ya kambi hadi nje kunazidi kuongezeka na
kwa kifupi hata gredi ya amani inaporomoka kwa kuwa hata kuangaliana kati ya
viongozi na wachezaji kunabadilika.
Wakati
fulani wachezaji walikuwa wakipokwa simu, hali hiyo imekuwa ikiendelea hadi
sasa. Lakini hisia za kumuona kila mmoja ni kama adui hazijawi kupungua na
ndiyo maana utaona kila baada ya mechi hiyo, viongozi lazima watakuwa na wa
kumuangushia lawama.
Hisia
zisizo sahihi ndizo zimekuwa zikiendesha ‘vichwa’ vya viongozi wa soka, pia wanajisahau
na kutaka kila mtu azitumikie klabu hizo kwa wakati huo bila ya kujali kwamba
soka ni burudani kwa wengine na si kazi kama ilivyo kwao.
Mfano, juzi
nilisikia kuna mmoja wa maofisa wa Simba ambaye aliacha kazi klabuni hapo, siku
chache zilizopita alionekana katika ofisi ya kiongozi mmoja wa sasa wa Yanga.
Imekuwa ni kosa kubwa na analaumiwa kwamba huenda alifika pale kuchukua fedha
kwa ajili ya kuwapelekea fedha wachezaji wa Simba ili ipoteze mchezo.
Ukiwauliza
waliokuwa wakitoa tuhuma hizo, hakuna hata mmoja mwenye uhakika na kuchukuliwa
kwa fedha hizo hizo na kupelekwa, lakini kwa kuwa tu ameonekana naye, basi
inaaminika alikwenda kuchukua fedha.
Iko haja ya
kutokuwa na hisia hasi ambazo hazijengi pia ni vziuri kumtuhumu mtu kwa
ushahidi badala ya hisia kwa kuwa hakuna maana kama wapenda soka watashiriki
mchezo huo halafu wasiwe marafiki. Utani si uadui au ugomvi.
Lakini
nguvu nyingi zikielekezwa kwenye maandalizi, huenda kutakuwa na mafanikio mengi
kuliko hisia za kuhujumiwa kuonekana kama ndiyo muongozo, mbaya zaidi karibu
wote inakuwa kama ‘akili’ zimekosa moto na badala yake wanahisi kuhujumiwa kila
wakati na maisha yao yanakuwa ni lawama tu.
Kama Yanga
na Simba zitaendeshwa kwa hisia tu, basi hazitafanya vizuri kwa kuwa hali
halisi ndiyo inapaswa kuchukua nafasi na kufanya mambo kwa uhakika (si
kubahatisha), kutasaidia kubadilisha mambo.
Wakati
mwingine huwa ninaamini wachezaji wengi hasa Watanzania wamekuwa hawachezi kwa
uwezo wao wote mechi za Simba dhidi ya Yanga kwa kuwa wana hofu ya kuonekana
wamehujumu, hivyo hata kama kulikuwa na sehemu mchezaji alitaka kujaribu kupita
na anaaminianaweza, basi ataacha kwa hofu akipoteza mpira ataonekana ni
mhujumu, hivyo anatoa pasi ilimradi huku akiacha kutumia ubunifu alionao
kuisaidia timu!
0 COMMENTS:
Post a Comment