Na Mwandishi Wetu
MLEZI wa Simba, Rahma Al Kharusi amevunja ukimya wa
muda mrefu na kusema anaendelea kufanya shughuli za klabu hiyo kwa kuwa sasa
yuko nchini England.
Rahma maarufu kama Malkia wa nyuki amesema yuko jijini
London kwa ajili ya mkutano maalum na mmiliki wa Sunderland, Ellis Short
kujadili mambo kadhaa kwa faida ya klabu hizo na hasa Simba.
Short ndiye mmiliki wa klabu ya Sunderland na aliyempa
kazi kocha matata Muitaliano, Roberto Di Canio ambaye ana kibarua kigumu cha
kuikoa timu hiyo isiteremke daraja baada ya kukumbana na kipigo cha mabao 6-1
kutoka kwa Aston Villa, wiki iliyopita.
“Nipo, kama nilivyosema awali, zaidi nimewekeza nguvu
zangu kwa ajili ya msimu ujao. Sasa niko London na baadaye nitaenda Sunderland
kwa ajili ya kukutana na mmiliki wake.
“Kuna masuala kadhaa ya msingi kuhusiana na uhusiano
mpya wa Simba na Sunderland, najua Simba ndiyo itafaidika zaidi.
“Ratiba ni kwamba nitakutana na watu wa Sunderland na
ratiba yao na mimi itakuwa kuanzia Jumapili hadi Jumanne,” alisema Malkia we
nyuki.
Taarifa zinaeleza huenda Mwenyekiti wa Simba, Ismail
Aden Rage naye akaungana na Malkia wa Nyuki nchini humo ndani ya leo na kesho.
Akiwa jijini Dar es Salaam mwezi uliopita, Malkia wa
nyuki alizungumza na Short kuhusiana na suala la uhusiano wa klabu hizo mbili
na mmiliki huyo bilionea wa Sunderland akatoa mwaliko huo.
Iwapo Simba itafanikiwa kuingia mikataba ya
kimaendeleo na Sunderland yenyewe ndiyo itafaidika zaidi kwa kuwa Waingereza
hao wamepiga hatua zaidi kimaendeleo.
0 COMMENTS:
Post a Comment