*Akumbushia
Yanga walivyomtosa na kutua Simba
*Aamua
kurudi shule nchini Sweden
Na Saleh
Ally
MWANZONI
mwa miaka ya 2000, Simba ilikuwa ina kiungo mchezeshaji aliyekuwa kipenzi
kikubwa cha mashabiki na wanachama wa klabu hiyo.
Ukimuona
anacheza, huenda utafikiri kuwa hana uwezo mkubwa, lakini alianza kucheza soka
la Ulaya tangu enzi hizo, wengine wanafuatisha, leo ndiyo maana utaona
wanamsifia mtu kama Salum Abubakary ‘Sure Boy’.
Shekhan
Rashid Abdallah alikuwa kiungo namba nane, wakati huo namba sita unamkuta ‘mnyama’
Selemani Matola. Ndiyo maana kiungo cha Simba kilikuwa gumzo.
Shekhan
alitokea Yanga, alianza kukipiga katika timu ya vijana, lakini baadaye hakupata
nafasi kwa kuwa waliokuwa wakifanya usajili walimdharau, huenda kuna kitu
kilimponza.
“Inawezekana
walinidharau kutokana na wembamba wangu, nilikuwa mwembamba mno. Wakaona
sitaweza kuhimili mikiki, ndiyo maana nikatua Simba,” anasema katika mahojiano
maalum kutoka Stockholm, Sweden anakoishi.
Tayari
Shekhan ni baba wa watoto wawili, Maryam, mwenye mwaka mmoja na miezi mitatu na
Jamal, mwenye wiki mbili sasa na yeye ameamua kuendesha familia yake.
“Naweza
kusema nimeacha soka, sichezi tena soka la kiushindani. Nimerudi shule, kwa
sasa ni mwanafunzi lakini kila ninapopata muda wa mapumziko ninakuwa naichezea
timu ya FC Kilimanjaro ambayo inaundwa na Watanzania hapa Sweden.
“Timu
inatukutanisha Watanzania na ina malengo, lakini mimi zaidi nakuwa kama kocha
na kusaidiana na wenzangu katika kutafuta maendeleo kwa pamoja kwa kuwa
tunaishi kama ndugu,” anasema Shekhan.
Familia:
Kweli sasa
mimi ni mtu wa familia na nimetupa nguvu zangu zote huku, ni familia yenye
furaha, unaweza kusema happy family.
Watoto
wangu kweli ni wadogo na sijajua wanataka nini wakikua na siwezi kuwachagua
kuwa wanasoka kama hawatataka, lakini nitahakikisha ninawaunga mkono katika
kile watakachokuwa wanataka kufanya kwa ajili ya maendeleo ya maisha yao.
Simba
kuyumba:
Niko mbali,
lakini naona namna mambo yanavyokwenda Simba, kwangu siwezi kusema ina
wachezaji wasiojua mpira, nawaona wachezaji wengi na wenye uwezo mkubwa pale.
Tatizo liko
kwa uongozi, vizuri ukajirekebisha na kujenga umoja. Kama uongozi hauna umoja,
Simba haiwezi ikafanya vizuri hata kidogo. Lazima kuwe na mabadiliko katika
hilo na uongozi ndiyo unaotakiwa kufanya vizuri.
Kujirekebisha:
Simba
inaweza kurudi katika hali yake, haijafanya vizuri lakini haijaharibu katika
kiwango cha kutisha hadi unaweza kusema mambo ni mambo sana. Lakini kila kitu lazima kianzie kwa uongozi
ambako mambo yaliharibika.
Baada ya
hapo, hata wachezaji wanapaswa kuwa na umoja ndiyo mambo yatakwenda vizuri, la
sivyo kutakuwa hakuna mabadiliko.
Mechi:
Naikumbuka
sana mechi ya mwaka 2002, ilikuwa fainali ya Kombe la Tusker, tuliwafunga Yanga
mabao 4-1 na kutwaa ubingwa, nilicheza vizuri sana.
Lakini
nakumbuka Yanga ilikuwa timu bora wakati huo, sisi pia. Hivyo ushindani ulikuwa
mkubwa sana licha ya kufanikiwa kuwafunga mabao mengi.
Kikosi
bora:
Simba
imekuwa na vikosi vingi sana bora, lakini wakati wetu kikosi bora kilikuwa
hiki; kipa ni Mohammed Mwameja, 2. Said Sued ‘Panucci’, 3.Ramadhani Wasso,
4.Amri Said ‘Stam’, 5.Boniface Pawasa ‘Baba P’, 6.Selemani Matola, 7.Steven
Mapunda ‘Garincha’, 8. Shekhan Rashid, 9.Nteze John, 10.Yusuf Macho Lwenda,
11.Mark Sirengo au Joseph Kaniki.
Katika
kikosi hicho, kama atatoka Nteze au Macho, nje kulikuwa na super sub, Emmanuel
Gabriel, maarufu kama Gabriel, nakuambia hautoki hapo, hata kama atakuja TP
Mazembe.
Fedha:
Kungekuwa
na fedha wakati huo, tungefika mbali sana kwa kuwa tulikuwa na uwezo mkubwa.
Lakini kipindi hiki watu wamepata sana fedha lakini ndiyo hivyo.
0 COMMENTS:
Post a Comment