Na Saleh Ally
Taifa Stars imefungwa mabao 4-2 na
wageni wake Ivory Coast katika mechi ambayo imekuwa ni kama msumari katika
mioyo ya Watanzania wapenda soka ambao tayari walikuwa na matumaini makubwa.
Matumaini makubwa ya mashabiki wa soka
yalikuwa ni kuiona Stars ikivuka na kukwea pipa la kucheza Kombe la Dunia
mwakani kule Brazil.
Tuliamini inawezekana kwa kuwa timu yetu
ilionyesha inaweza, ilicheza vizuri na kufanikiwa kupata ushindi kama mechi
ngumu zikiwemo zile zinazoihusisha Morocco ambayo ni moja ya timu kubwa barani
Afrika, ikalala kwa mabao 3-1.
Achana na wale Watanzania ‘feki’ ambao
wameshaanza kuibeza Stars kisa imefungwa na Ivory Coast! Lakini walishangilia
pamoja nasi wakati Stars hiyohiyo ilipoinyoa Morocco kwa mabao 3-1. Nawaita
wanafiki.
Ninapolenga, pamoja na mchezo mzima,
nilikuwa naangalia vita ya wachezaji uwanjani. Naweza kusema wachezaji wa
Tanzania hata kama walifanya makosa lakini walijitahidi kwa kiasi kikubwa.
Kuna mambo kadhaa ya kuangalia, lakini mfano
wangu mzuri wakati nikiwa nyuma ya goli la Ivory Coast na baadaye Taifa Stars,
niliona beki kinda wa Stars, Shomari Kapombe akifanya kazi ya kumzuia Yaya
Toure.
Inawezekana mmesahau, Kapombe ni beki wa
Simba, Yaya anatokea Manchester City ya England. Hapa ndipo sinema inaanzia,
taratibu utagundua ninachotaka kuelezea. Kidogo narudi kwenye ‘trela’ kabla
‘picha’ kuanza.
Mwaka 2009, nilikuwa nchini Ivory Coast
kwa siku 20, moja ya sehemu nilizotembelea ni ‘akademi’ ya Asec Mimosa ya
jijini Abidjan. Nikiwa pale niligundua mfumo mzuri sana wa kukuza wachezaji
ambao hauna tofauti na ule wa Ulaya.
Wafaransa lukuki wameajiliwa pale,
wanalipwa mamilioni ya fedha kuhakikisha mambo yanakwenda vizuri na mmoja wao
ni mke wa aliyekuwa kocha wa Simba, Patrick Liewig.
Kati ya wachezaji waliopitia Asec Mimosa
ni Yaya na kaka yake Kolo Toure na baada ya hapo wakaanza safari ya kwenda
nchini nyingine kama Ufaransa na kwingine. Sasa ‘picha’ linaanza.
Makuzi:
Toure amekulia maisha ya soka hasa, hana
tofauti na wachezaji wa Ulaya, lakini makuzi ya Kapombe kila kitu kinaonekana
kinaendana na kubahatisha kwa kuwa amekulia kwenye ‘akademi’ zetu za kuunga.
Ndani ya Mimosa, viwanja bora vinne kwa
ajili ya vijana, mmoja mkubwa kwa ajili ya timu ya wakubwa, sehemu ya madarasa,
sehemu ya kulala wachezaji na hoteli kubwa ya kisasa inayomilikiwa na timu
hiyo.
Lakini hakuna ubishi Kapombe amecheza
katika viwanja vigumu, vyenye mabonde na kwa kifupi ni katika hali ngumu sana.
Ukiangalia hata mpangilio wa mlo, pale
Mimosa kila kitu ni kwa mpangilio na wakati mwingine wachezaji waandikiwa
kwenye karatasi. Tafakari mwenyewe kuhusiana na Kapombe.
Walimu:
Waaivoriani, wameajiri Wafaransa kwa
ajili ya kuwakuzia watoto wao kisoka. Mmoja wao ni Yaya, maana yake mambo
yanakwenda kitaalamu zaidi.
Lakini angalia Kapombe amefundishwa na
walimu wetu ambao huwezi pia kuwalaumu kwa kuwa hakuna mipango madhubuti ya
kuwaendeleza zaidi ili wasaidie vijana wetu. Badala yake nao wamekuwa wakitumia
vipaji vyao tu.
Hata maslahi, Wafaransa wa pale Mimosa
wanalipwa zaidi ya dola 20,000 kwa mwezi, hivyo wanaifanya kazi yao kwa ufasaha
na kujituma kuhakikisha wanazalisha. Lakini hapa Tanzania makocha walioanza
kumkuza Kapombe, huenda walikuwa wakifanya kazi kwa kujitolea au kwa mshahara
usiozidi Sh 200,000.
Ulaya:
Mwaka 2001 hadi 2003, Toure alikuwa akiichezea
Beveren ya Ubeligiji, timu hiyo wamepita wachezaji kama Emmanuel Eboue,
Romaric, Arthur Boka, Gervino na wengine wengi. Halafu 2003-05 akahamia FC
Metalurh Donetsk ya Ukraine.
Another unique sport writer i admire Saleh, angle nzuri sana umeichukua, keep it up
ReplyDelete