June 3, 2013


Na Khatimu Naheka
KIPA wa Simba raia wa Uganda, Abel Dhaira (pichani), amewasilisha ombi kwa uongozi wa timu hiyo akitaka kuondoka.

Simba hivi karibuni ilimsajili aliyekuwa mlinda mlango wa Kagera Sugar, Andrew Ntalla na kufikisha idadi ya makipa watatu; wengine ni Dhaira na Juma Kaseja, hali inayosababisha ushindani wa namba katika safu hiyo msimu ujao utarajiwe kuwa mkubwa.

Dhaira ambaye ni kipa namba moja wa timu ya taifa ya Uganda, hivi karibuni aliuambia uongozi wa Simba kuwa anaomba kurudi katika klabu yake ya zamani ya I.B.V ya nchini Iceland kwa ajili ya kufanya nayo mazoezi.

Tangu atue katika kikosi cha Simba katikati ya msimu uliopita akitokea katika kikosi hicho cha I.B.V, Dhaira ameshindwa kupata namba Msimbazi, akipigwa benchi na Kaseja.
Dhaira akiwa alidaka michezo mitatu tu msimu uliopita, ameshtukia kwamba kiwango chake kitashuka, hivyo ameutaka uongozi wa Simba arejee katika kikosi chake cha zamani.

Taarifa ambazo Championi Jumatatu limezipata kutoka kwa mtu wa karibu na kipa huyo mrefu kuliko wote kwenye Ligi Kuu Bara, zinasema kipa huyo amekuwa hana raha kutokana na kukalia benchi.

“Abel hana raha kabisa, kifupi ninachoweza kukwambia ni kwamba hafurahishwi na jinsi anavyotumika katika kikosi hicho, sasa hapa kitu pekee kinachoweza kumkwamisha ni mkataba wake na Simba, ambao umebakiza mwaka mmoja na zaidi,” alisema rafiki huyo.

Alipoulizwa kuhusiana na suala hilo, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zakaria Hans Pope, alisema: “Kweli dhaira aliomba kuondoka kurudi katika klabu yake hiyo ya zamani, ila ni kwa lengo la kwenda kujifua katika kipindi hiki ambacho ligi imesimama, lakini hatujakubaliana na ombi lake. Tumemjibu haiwezekani kwa kuwa tunajiandaa na Kagame.”

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic