June 3, 2013

Sehemu ya wanakamati wa mazishi ya msanii Albert Mangweha.
Na Joan Lema
KAMATI ya Mazishi ya aliyekuwa Msanii wa Bongo Fleva, Albert Mangweha ‘Mangwea’, mpaka jana mchana ilikuwa imekusanya jumla ya shilingi milioni 32 kutoka kwa wadau mbalimbali.
Kamati hiyo inahitaji shilingi milioni 50 kwa ajili ya kusaidia kusafirisha mwili wa marehemu kutoka Afrika Kusini mpaka Morogoro kwa ajili ya mazishi. Fedha hizo pia zinahitajika kwa ajili ya kuratibu shughuli nzima ya mazishi.
Mangwea alifariki dunia Jumanne iliyopita nchini Afrika Kusini na mwili wake ulitarajiwa kuwasili nchini jana lakini ikashindikana kutokana na kuelezwa kuwa ripoti ya uchunguzi wa madaktari ilichelewa kutoka pamoja na michakato mingine ya vibali.
Kamati ya Mazishi bado inaendelea na mchakato wa kuratibu shughuli hiyo jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na Championi Jumatatu akiwa Mbezi Goig jijini Dar ambako ndiko kwenye msiba huo, mmoja wa waweka hazina wa kamati hiyo, Paul Matthysse ‘P-Funk’, alisema mpaka sasa kamati yake imefikisha shilingi 32,259,000 ingawa wanatarajia kuendelea kupokea michango mbalimbali kutoka kwa wadau.
Miongoni mwa watu wa kwanza kutoa michango yao katika msiba huo ni P-Funk aliyetoa Sh milioni tano, Clouds Media Group (Sh milioni tano) na Push Mobile (Sh milioni tano). Juzi Kampuni ya Global Publishers ilitoa Sh milioni moja.
“Nawasisitiza Watanzania waendelee kutoa michango yao kwa ndugu yao ili kuonyesha umoja tulionao. Fedha zikiwa nyingi tunataka kumfanyia kitu mama yake ili kuendelea kumfariji kwani kipindi hiki ni kigumu kwake,” alisema P-Funk.
Wakati huohuo, taarifa kutoka Morogoro zilisema mama mzazi wa Mangwea aishie mkoani humo, Denisia Mangwea, alipandwa na presha baada ya jana kupata taarifa kuwa mwili wa mwanaye umezuiwa Afrika Kusini kutokana na uchunguzi wa madawa ya kulevya. Alikimbizwa hospitali na inadaiwa anaendelea vizuri. Mangwea aliwahi kutamba na nyimbo kadhaa kali zikiwemo Gheto Langu, She Got a Gwan, Mikasi na Nipe Dili.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic