Na Saleh
Ally
Msimu uliopita, Yanga walikuwa ni timu iliyofanya mabadiliko makubwa kuhusiana na
suala la nidhamu, lengo lilikuwa ni kujenga kikosi imara chenye ushirikiano wa
karibu zaidi.
Wakafanikiwa,
maana kutoka nafasi ya tatu msimu mmoja hadi kuwa mabingwa wa Tanzania Bara,
tena wakifanikiwa kutwaa taji huku wakiwa na mechi mkononi, maana yake
walimaliza ligi wakiwa bora zaidi.
Si kwa
kuchukua kombe tu, hata kwa takwimu, Yanga ndiyo walikuwa na kikosi bora kwani
pamoja na kufunga mabao mengi zaidi kuliko timu nyingine kati ya zilizoshiriki
ligi, wao ndiyo waliofungwa mabao machache zaidi na wakabeba rundo kubwa zaidi
la pointi.
Kocha Mkuu,
Ernie Brandts, ambaye ni mahiri kwa kuwa na vikosi vinavyobeba mataji, anataka
zaidi ya walipofikia kwa kuwa msimu ujao Yanga itakuwa na kibarua kigumu cha
michuano ya kimataifa.
Yanga
watashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika, na Brandts anajua lazima kuwe na
mabadiliko makubwa na ikiwezekana, anasema atalazimika kuwa mkali zaidi.
Pamoja na
mambo yote, Brandts anaelekeza ukali wake zaidi katika nidhamu, anaamini
nidhamu ni muhimu zaidi kwake kwa kuwa imechangia kuleta mabadiliko makubwa.
Msimu
uliopita, baadhi ya wachezaji wakiwemo Simon Msuva, David Luhende na Athumani
Idd ‘Chuji’ walikumbana na adhabu ya kukatwa fedha zao za mshahara kutokana na
kukutwa na kibano cha utovu wa nidhamu.
Championi:
Labda kipi kitaongozeka ili kuboresha nidhamu?
Brandts: Kuna mambo mengi, lakini suala la kuwahi
mazoezini au kwenda na muda ni muhimu zaidi.
Championi:
Kivipi?
Brandts:
Mfano msimu uliopita niliwaondoa wachezaji katika kikosi kwa kuwa walichelewa,
tena ni wachezaji wakongwe. Lakini kuna waliokatwa fedha zao.
Championi:
Unafikiri hiyo inatosha au kutakuwa na mabadiliko?
Brandts:
Ndiyo, kutakuwa na mabadiliko. Kwani adhabu ya makato ya fedha itakuwa kubwa
zaidi. Kwanza hata suala la kusema mchezaji anaumwa halafu anabaki nyumbani,
halitakuwa na ruhusa.
Championi:
Kama kocha, lazima ukumbuke wachezaji nao ni binadamu, wanaweza kuugua. Au hilo
ni kosa?
Brandts: Si
kosa, ila kuna utaratibu wa kufuata, suala la mchezaji kuumwa halafu anatuma
ujumbe mfupi na kulala nyumbani haliwezi kuwa sawa. Sasa utaratibu lazima
ufuatwe, mchezaji lazima aje mazoezini,
daktari wa timu atampima na kujua anaendeleaje na mwisho ataamua apumzike au
la.
Championi:
Vipi kuhusu kuhakikisha wachezaji wanafuata maadili hata nje ya uwanja?
Brandts:
Mimi nataka wachezaji wanaojitambua, siyo ninaowachunga, maana yake hata wakiwa
nyumbani wajue wanachotakiwa kufanya kama vile kupumzika mapema, ikiwezekana
kuepuka kutoka na kwenda kwenye klabu za usiku.
Championi:
Lakini wachezaji wanaweza kwenda kujipumzisha kidogo na kunywa bia kidogo, je hilo
ina tatizo?
Brandts:
Inawezekana, huwezi kuwachunga, lakini mchezaji akinywa lazima ajue hatakiwi
kupitiliza hadi kuonekana amelewa, pia lazima ajue ni wakati gani wa kunywa,
mfano siku tatu kabla ya mechi. Tatizo lingine ni wanawake.
Championi:
Sijaelewa, unamaanisha timu ya wanawake?
Brandts:
Hapana, yaani suala la kuwa na wanawake kwao si zuri, wachezaji wengi wameshuka
kiwango kutokana na suala hilo. Najua kwa utamaduni wa Afrika naweza kuonekana
nakosea, lakini uzinzi ni adui mkubwa wa michezo. Katika soka, ukipenda suala
hilo ujue hutadumu na mafanikio yatakuwa duni.
Championi:
Lakini hutaweza kujua wachezaji wako kama wana tabia hizo au la kwa kuwa suala
hilo ni siri.
Brandts:
Ndiyo maana mwanzo nilisema sitaki kuwa na watu ambao nitawachunga, wala sitaki
kujua kama wanafanya hivyo au la. Lakini lazima wajue kwamba si sahihi kufanya
hivyo. Anayefanya hivyo anashusha kiwango chake na mwisho anaimaliza timu.
Championi: Unafikiri hayo yakifanyika, basi mnaweza
kufanya vizuri katika Ligi ya Mabingwa Afrika?
Brandts: Hayo ni sehemu tu, lakini Ligi ya Mabingwa
Afrika si mchezo kwa kuwa nilishiriki nikiwa na APR na tukatolewa kwa fitina na
Watunisia wa Etoile du Sahel.
Championi:
Unafikiri nini kingine kitawasaidia?
Brandts:
Pamoja na maandalizi mazuri, bado tunatakiwa kucheza soka la uhakika, kupunguza
makosa kwa kuwa katika michuano hiyo mambo ni tofauti sana na ligi ya hapa
nyumbani.
Brandts: Tofauti yake ni ipi?
Championi:
Pamoja na ubora wa ligi yenyewe kwa kuwa inakutanisha mabingwa wa kila nchi,
suala la umakini pia ni nguzo, kupunguza makosa pia ni muhimu sana. Unaweza
ukafanya makosa sita katika Ligi Kuu Tanzania Bara na bado kusiwe na madhara,
lakini katika Ligi ya Mabingwa kila kosa, ukajikuta umefungwa.
Championi:
Shukurani kwa ushirikiano, nakutakia safari njema kurejea Uholanzi kwa
mapumziko.
0 COMMENTS:
Post a Comment