June 19, 2013



PICHA NAMBA MOJA
PICHA NAMBA MBILI


Na Saleh Ally
BADO naendelea kusisitiza, kikosi chetu cha Taifa Stars kilifanya kila kinachowezekana kadri ya uwezo wake lakini ndiyo hivyo, mwisho wa mchezo kikawa kimelala kwa mabao 4-2 dhidi ya wababe Ivory Coast.
Kila mmoja ambaye alifanya juhudi zake kuhakikisha anaona Stars inaibuka na mchezo huo anastahili pongezi, mashabiki ni sehemu ya walioonyesha uzalendo wa dhati.

Lakini kila kosa lazima liwe msaada, nikimaanisha kila unapokosea ni lazima kujifunza kwa ajili ya kusaidia mambo hapo baadaye.

Ukiangalia mechi hiyo ya kuwania kufuzu kucheza Kombe la Dunia kati ya Taifa Stars na Ivory Coast kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Jumapili iliyopita, utagundua hakuna tofauti kubwa ya soka.
 
PICHA NAMBA TATU

Lakini Ivory Coast walionyesha walijua wanachofanya na mambo mengi waliyopanga yalikwenda kama walivyopanga. Kosa kubwa zaidi kwao ni bao la kwanza la Stars alilofunga Amri Kiemba, walijisahau wakashindwa kufunga.


Kosa hilo likahamia Stars na utaona picha katika ukurasa huu zinaonyesha tofauti kubwa kati ya Ivory Coast na Taifa Stars hasa katika suala la ukabaji ‘marking’.

Bao la kwanza:
Ukiangalia bao la kwanza walilofungwa Stars, utaona wachezaji wawili wa Ivory Coast (Yaya Toure na Lacina Traore wakiwa katika boksi ya 18 na wachezaji wanne wa Taifa Stars ambao ni Salum Abubakari ‘Sure Boy’, Frank Domayo, Kelvin Yondani na Nadir Haroub ‘Cannavaro’.
 
PICHA NAMBA NNE
Ajabu hakuna hata mchezaji mmoja wa Stars ambaye alikuwa amemkaba Yaya au Traore, ndiyo maana mara baada ya Gervinho kutoa pasi kwa Toure, wakati Cannavaro anamfuata, mara moja akatoa pasi kwa Traore ambaye pia alikuwa peke yake, akapachika bao kilahisi kabisa. (Angalia picha 1&2).
Bao la nne:
Mabao mengine mawili yalikuwa ya penalti na lile la faulo. Lakini ukiangalia bao la nne pia, baada ya Gervinho kumtoka Erasto Nyoni na kupiga krosi iliyoguswa na Kaseja, wachezaji wote wa Stars walikuwa upande mmoja.

Hata kama mpira uliguswa, kama ‘marking’ ingekuwa makini, hapa shaka mabeki ndiyo wangekuwa wa kwanza kuuwahi. Kama mambo yangeenda kwa mpangilio, hata baada ya Kaseja kuuguza ule mpira, basi beki mmoja tu angepotea.
 
PICHA NAMBA TANO
Kitendo cha mabeki wote kwenda kucheza mpira mmoja huku wachezaji wawili wa Ivory Coast, Yaya  na Bonny Wilfried kuwa ‘free’ ikawa ni lahisi kwao kufunga kwani hata angeukosa mfungaji basi ule mpira ungeenda kwa Yaya ambaye pia angefunga.
Umakini:
Angalia Ivory Coast walivyokuwa makini katika suala la ulinzi, huenda ingekuwa bora zaidi kama Stars wangefanya hivyo. Angalia picha namba tatu inaonyesha Thomas Ulimwengu akiwa ameruka katika msitu wa mabeki watano wa Ivory Coast, huo ndiyo ulinzi.

Lakini angalia namna kipa wa Stars, Kaseja akiwa ameruka kuda mpira kwenye msitu wa wachezaji wa Ivory Coast lakini hatua kama nne au tano hauoni hata beki mmoja aliye tayari kumsaidia.

Bado angalia picha namba nne, faulo imechongwa ndani ya lango la Ivory Coast, mabeki wao wawili wameruka pamoja na kipa kumthibiti mchezaji mmoja wa Stars.

Lakini ukiangalia wachezaji wengine wa Stars kila mmoja amethibitiwa. Didier Zokora amemkumbatia Mbwana Samatta na Souleman Bamba amemkumbatia Kiemba. Kwa kifupi hawajawapa nafasi hata kama mpira utamtoka kipa, wako karibu hao kuokoa.

Lakini angalia picha namba tano ambayo Kaseja ameruka na kudaka mpira ndani yam situ wa wachezaji wanne wa Ivory Coast na hakuna aliye karibu kusaidia iwapo atafanya kosa kama binadamu.

Hili ni somo kubwa, huenda soka Stars haikuzidiwa sana. Lakini ujuzi zaidi, umakini unaotakiwa ndiyo uliwangusha kwa kuwa walikosa siku hiyo. Hivyo Kocha Kim Poulsen inabidi ayafanyie kazi haya.

Si lahisi timu ikawa inafunga halafu lahisi kufungwa, ndiyo maana ugumu ulionekana siku hiyo na Ivory Coast wakayatumia makosa hayo kuiangusha Stars.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic