Moja ya mikakati ya Taifa Stars
kwenye mechi ya kesho (Julai 27 mwaka huu) dhidi ya Uganda kuwania kuwania
tiketi ya kucheza Fainali za Tatu za Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN)
zitakazofanyika mwakani nchini Afrika Kusini ni kushambulia kwa muda mwingi wa
mchezo.
Kocha Kim Poulsen amesema
maandalizi ya Taifa Stars jijini Mwanza kwa ajili ya mechi hiyo ambayo Uganda
inaongoza kwa bao 1-0 yalikuwa mazuri, lakini mabao ni muhimu hivyo
watashambulia bila kusahau kulinda lango lao.
“Unapocheza mechi za aina hii
za nyumbani na ugenini, huku mwenyeji akiwa anaongoza mabao yana maana kubwa
katika mechi. Mabao yanabadili mchezo na pia wachezaji kifikra,” amesema Kim
akizungumza na waandishi wa habari kwenye hoteli ya Mt. Zion ambayo Stars
imefikia.
Amesema katika mechi ya kwanza
walitengeneza nafasi nyingi lakini hawakuzitumia, hivyo wamekuwa wakifanya
mazoezi ya kushambulia, jinsi ya kutengeneza nafasi, na jinsi ya kumalizia.
“Hivyo tuko hapa (Kampala) kwa
ajili ya kufunga, ni lazima tufunge ili tuweze kuendelea na mashindano. Lakini
ngome yetu nayo ni lazima iwe makini ili kutoruhusu bao,” amesema Kim na
kuongeza kuwa kikosi chake cha kwanza ni lazima kitakuwa mabadiliko kutoka na
Mwinyi Kazimoto kuingia mitini na Shomari Kapombe kwenda kwenye majaribio
Uholanzi.
Amesema angalau kutakuwa na
mabadiliko kwa kuingiza sura mbili mpya katika kikosi cha kwanza, na kuongeza
kuwa wachezaji wanafahamu umuhimu wa mechi hiyo kwani timu ikienda kwenye
Fainali za CHAN itakuwa manufaa kwao binafsi.
Taifa Stars inayodhaminiwa na
Kilimanjaro Premium Lager imefanya mazoezi ya mwisho leo jioni Uwanja wa
Mandela ulioko Namboole ambao utatumika kwa ajili ya mechi hiyo kesho.
Mechi hiyo itaanza saa 10
kamili jioni kwa saa za Afrika Mashariki na itachezeshwa na waamuzi kutoka
Madagascar wakiongozwa na Kanoso Abdoul Ohabee wakati mwamuzi msaidizi namba
moja ni Andirvoavonjy Pierre Jean Eric. Mwamuzi msaidizi namba mbili ni Jinoro
Velomanana Ferdinand huku Andriamiharisoa Hubert Marie Bruno akiwa mwamuzi wa
mezani (fourth official). Kamishna wa mechi hiyo namba 38 ni Ismail Kamal
kutoka Ethiopia.
0 COMMENTS:
Post a Comment