SIMBA WAKIWA MAZOEZINI |
YANGA WAKIJIFUA |
Na Saleh Ally
RATIBA mpya ya Ligi Kuu
Bara msimu wa 2013-14 imekuwa gumzo kubwa na kuzua mijadala lukuki tokea
ilipotolewa wiki moja iliyopita. Ligi hiyo imepangwa kuanza kutimua vumbi
Agosti 24, mwaka huu.
Gumzo la ratiba hiyo kwa
wengi limekuwa ni namna gani Yanga na Simba zitacheza mechi nyingi nyumbani,
huku wanaochambua wakiwa wamejisahau kwamba hata wakianzia nyumbani, mwisho
lazima wacheze ugenini pia, hawawezi kukwepa.
Ratiba hiyo inaonyesha
kuna upungufu sehemu kadhaa kwa kuwa kuna timu zitakaposafiri mkoani, mfano
Yanga itakapokuwa Mbeya Septemba 14 kucheza na Mbeya City, haitaondoka mjini
hapo hadi Septemba 18 itakapocheza na Prisons na huo ni mpangilio mzuri katika
ubanaji wa matumizi.
Lakini bado kuna sehemu
zinaonyesha kuwa ratiba hiyo ina usumbufu na haijazipunguzia timu kazi kubwa ya
uchovu na nauli, kwani Septemba 18, Mtibwa Sugar itaikaribisha Mbeya City kwao
Manungu, halafu Septemba 21 inafunga safari kwenda Mbeya kwenda kucheza na
Prisons mjini Mbeya.
Gumzo kubwa ni namna timu
tano maarufu zaidi zitakavyokuwa na kazi kubwa ya kuchuana kuwania ubingwa na
nafasi ya pili ambayo ni muhimu kwa kuwa anayeipata anaiwakilisha Tanzania
katika michuano ya Kombe la Shirikisho.
Lakini kuna suala la
heshima, hili linakwenda katika nafasi ya tatu angalau hata kama timu haipati
nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa lakini inaonekana iko 3 Bora.
Timu ziko tano, unaweza
kusema Big Five, tofauti na inavyokuwa England katika Premiership kuna Big
Four lakini za hapa nyumbani ni Yanga,
Simba, Azam FC, Coastal Union na Mtibwa Sugar.
Inawezekana kabisa Kagera
Sugar wakawa tatizo kubwa kwa timu hizo tano kama ilivyofanya msimu uliopita na
kushika nafasi ya nne huku ikiipa presha kubwa Simba iliyoangukia namba tatu. Muhimu
zaidi ni mechi tano za mwanzo kwa kila timu ambazo zinaweza kuwa jibu kama
zimeteleza au zimeshika kasi kuelekea kwenye ubingwa.
Timu itakayofanya vizuri
katika mechi hizo tano za mwanzo, maana yake tayari imeanza na mguu mzuri na
kujiendeleza ni rahisi lakini ikipotea tu kuna mawili; kutumia nguvu nyingi
zaidi kujiweka sawa au kukubali imeshapotea mapema kabisa. Itakayoshinda tano
zote, maana yake ina pointi 15 na huenda itakuwa vigumu kuizuia.
Yanga:
Wanaonekana wamejiandaa vizuri
kutetea ubingwa wao lakini bado hawajakamilisha vizuri safu yao ya ushambuliaji
na Kocha Ernie Brandts anakubali hilo huku akifanya kila juhudi kupata straika
wa maana kwa kuwa anajua atakuwa na kibarua kingine cha Ligi ya Mabingwa
Afrika.
Upande wa ratiba, ndani
ya mechi tano, Yanga itakuwa na mechi ngumu zaidi tatu ambazo ni ya pili dhidi
ya Coastal Union, ya tatu dhidi ya Prisons ugenini Mbeya na ya tano dhidi ya
Azam FC.
Katika mechi hizo tano,
tayari Yanga itakuwa imepata jibu kuhusiana na mwenendo wake lakini kuna kila
sababu ya kuwa makini si sahihi kuzidharau Ashanti na Mbeya City kwa kuwa
zimepanda, hata kama hazina uzoefu lakini silaha zao hazijulikani.
Simba:
Lazima Simba wawe vizuri
kifiziki, maana timu tano wanazokutana nazo mwanzo zote zina sifa ya kuwa na
mazoezi magumu. Kwa kifupi katika mechi tano za mwanzo, Simba itacheza mechi tatu
na timu za majeshi.
Mechi ya kwanza ni dhidi ya
Rhino mjini Tabora, ya pili na Oljoro, Arusha, ya tatu ni Mtibwa na ya nne ni
Mgambo halafu ya tano ni dhidi ya Mbeya
City mjini Mbeya.
Lakini ukiachana na mechi
hizo tano, ndani yake Simba itakuwa na kazi ya kuivaa Mtibwa Sugar iliyoishinda
na kuifunga Simba msimu uliopita. Ukiangalia katika usajili inaonekana bado
Wekundu hao hawajatulia vizuri, hivyo kuna mambo ya kufanyia kazi mapema.
Azam:
Wamekuwa na mwenendo
mzuri baada ya kushika nafasi ya pili mara mbili na mara zote wameshiriki Kombe
la Shirikisho, msimu uliopita walionekana kuwa na mabadiliko chanya.
Kikosi chao hakina
mabadiliko makubwa, mechi ya kwanza dhidi ya Mtibwa Sugar inaweza isiwashitue
sana kwa kuwa wamekuwa wababe wa vijana hao wa Manungu kwa misimu miwili sasa,
ingawa hawapaswi kudharau.
Mechi ya pili dhidi ya
Rhino, Kagera na ile ya tano dhidi ya Yanga zitakuwa na msisimko lakini kama
Azam itaendelea na mwenendo ule wa msimu uliopita inawezekana ikapata pointi
nyingi katika mechi hizo tano.
Coastal:
Si vizuri kuwadharau,
msimu uliopita baada ya mzunguko wa kwanza waliwaacha wakongwe na kuongeza
vijana, lakini wakamaliza katika nafasi ya tano. Safari hii wana nguvu zaidi
kwa kuwasajili Haruna Moshi ‘Boban’, Juma Said Nyosso na Mkenya ambaye ni kati
ya wachezaji walioonekana tishio.
Coastal wana kila sababu
ya kuwa tishio ingawa nao katika mechi tano za mwanzo wanatakiwa kuwa bora kifiziki
kwa kuwa watakutana na timu nne za jeshi halafu moja ni dhidi ya mabingwa
watetezi, Yanga.
Timu za jeshi nyingi
zinakuwa fiti zaidi kutokana na mazoezi yao, hivyo ni lazima suala la kujiandaa
kwa Coastal hasa kuhakikisha wako fiti lipewe kipaumbele.
Mtibwa:
Hawa jamaa, msimu
uliopita walionekana kama wameamka na walizisumbua sana Yanga na Simba. Lakini
baadaye wakapoteza mwelekeo kidogo na Kagera wakabeba sifa yao.
Lakini maandalizi yao ya
ukimya yanaweza kubadili mambo, huenda wakaibuka wakiwa fiti zaidi kwa mazoezi
makali wanayofanya jirani na mashamba ya miwa. Hata hivyo lazima wajipange
katika mechi tano za mwanzo kwani watakutana na timu mbili za Big Five.
Mechi ya kwanza dhidi ya
Azam, ya tatu na Simba na moja dhidi ya timu ya jeshi ambayo ni Prisons, lakini
itakuwa na mechi nyingine ngumu dhidi ya ‘ndugu’ zao Kagera Sugar.
MECHI 5 ZA YANGA
Yanga v Ashanti Dar
Yanga v Coastal Dar
Mbeya City v Yanga Mbeya
Prisons v Yanga Mbeya
Azam FC v Yanga Dar
MECHI 5 ZA SIMBA
Rhino v Simba Tabora
Oljoro v Simba Arusha
Simba v Mtibwa Dar
Simba v Mgambo Dar
Simba v Mbeya City Mbeya
MECHI 5 ZA AZAM FC
Mtibwa v Azam Manungu
Rhino v Azam Tabora
Kagera v Azam Bukoba
Azam v Ashanti Dar
Azam v Yanga Dar
MECHI 5 ZA COASTAL
Oljoro v Coastal Arusha
Yanga v Coastal Dar
Coastal v Prisons Tanga
Coastal v Rhino Tanga
Coastal v R.Shooting Tanga
MECHI 5 ZA MTIBWA
Mtibwa v Azam Manungu
Mtibwa v Kagera Manungu
Simba v Mtibwa Dar
Mtibwa v Mbeya City Manungu
Prisons v Mtibwa Mbeya
0 COMMENTS:
Post a Comment