Na Saleh Ally, Zurich
ZIARA ya Ulaya safari hii inaishia
hapa katika jiji hili ambalo ni maarufu sana duniani kuhusiana na mambo mengi
kama vile amani, lakini ni pamoja na viongozi wengi wa Afrika kuficha fedha zao
hapa baada ya kuziiba.
Unaweza kusema mafisadi wengi
wamekuwa wakificha fedha zao hapa, lakini hiyo haikuwa kazi iliyonileta hapa.
Ziara ya Ulaya ilianzia hapa kabla ya kwenda Ujerumani na Ufaransa na juzi
nilikutana na mmoja wa rafiki zangu ambaye ni wakala wa kuuza wachezaji
anayetambuliwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa).
Katika mazungumzo yetu kuhusiana na
wachezaji, alitolea mfano wa wachezaji wawili waliokuwa wanacheza katika timu
moja ya vijana ya Ujerumani, mmoja sasa anacheza katika timu ya daraja la tatu
na anapata euro 3,000 (Sh milioni 7), wakati
mwenzake anacheza Werder Bremen inayoshiriki Bundesliga ambayo anaingiza euro
milioni moja (Sh bilioni 2.2 kwa
mwaka.
Kati ya wachezaji hao wawili,
anayeingiza kiasi kidogo ndiye alikuwa bora zaidi, lakini sasa mambo
yamebadilika. Kama hiyo haitoshi alielezea namna rafiki yake ambaye ni meneja
wa Thomas Muller wa Bayern Munich alivyokuwa hategemei kama mchezaji wake
atakuwa mmoja wa wachezaji bora.
Kwamba rafiki yake huyo aliamini
Muller hakuwa na umbo zuri la kumsaidia kuwa mchezaji bora wa kulipwa nchini
Ujerumani, aliamini huenda angeishia madaraja ya chini kwa kuwa alikuwa na
juhudi sana na ndiyo ungekuwa msaada wake. Lakini sasa ni bora katika soka la
kulipwa.
Nilipokuwa nikiendelea na mazungumzo
hayo wakati nikipata kahawa katikati ya moja ya mitaa inayopendeza ya Jiji la
Zurich, maneno hayo ya rafiki yangu yalinirudisha kwa Shomari Kapombe.
Kapombe amefanya majaribio katika
klabu za madaraja ya nne na timu ya pili ya AS Cannes timu ambayo ilimkuza
kiungo nyota duniani, Zinedine Zidane na wengine kadhaa.
Kapombe amefanya vizuri na timu hiyo
inaonyesha wazi kwamba kweli inamtaka, achana na kwamba kuna msaka vipaji
maarufu kama scout kutoka Zaragoza, lakini hali halisi ni kwamba Wafaransa
ndiyo wanaoonyesha zaidi kuvutiwa na Kapombe.
Lakini kumekuwa na mgongano wa njia
tatu, moja ni kwamba Kapombe anaonyesha wazi anataka kubaki Ufaransa na kucheza
soka, Wafaransa wanasema ‘yes’, wanamhitaji lakini watamhitaji kwa mkopo kwa
kuwa Tanzania si nchi maarufu kisoka na hawawezi kuweka fedha zao nyingi bila
ya kuwa na uhakika.
Walichoahidi Wafaransa ni kwamba wao
watakaa na Kapombe na kumuendeleza, wanaamini kwamba baada ya muda watamuuza na
kugawana fedha nusu kwa nusu na Simba.
Simba nao inaonekana wanahitaji
fedha, hivyo Kapombe kwenda kwa mkopo huenda inaonekana kama wanamtupa.
Ninaweza kuwa na wazo tofauti kwamba huenda ikawa hasara kwa sasa kwa Simba
lakini faida kubwa itaonekana hapo baadaye.
Bahati ya kucheza Ulaya bado ni
biashara kubwa kwa kuwa kama Kapombe kweli atafanya vizuri na wanamuamini anaweza
kufanya hivyo, basi vizuri wakikubali na akaenda.
Kama ni msimu mmoja au miwili
akiuzwa, basi watapata faida ambayo huenda itakuwa kubwa na itawafungulia soko
zaidi.
Akiuzwa katika klabu kubwa ni rahisi
kuwatangaza zaidi, huenda watakosa dola 100,000 au 150,000 kwa sasa, halafu
wakapata nyingi zaidi ya hizo baada ya miezi 12 ijayo ambapo bado itakuwa faida
kubwa, watakuwa wamejitangaza na kutengeneza mtandao mkubwa wa wacheza kuuza
wachezaji ikizingatiwa Simba wana vijana wengi.
Atakapoondoka Kapombe, bado watakuwa
na nafasi ya kumpa nafasi kijana mwingine ambaye pia ataingia katika nafasi ya
kuuzwa kwa kuwa Simba ina wachezaji wengi wanaoweza pia kuziba pengo la Kapombe
kwa wakongwe na makinda.
Inawezekana kwa viongozi wa Simba
suala hili lisiwe na faida kubwa kwa kuwa wanaweza kuangalia Kapombe anaweza
kuuzwa baada ya msimu mmoja au miwili, hivyo wao wanaweza wasiwe pale halafu ikawa ni sifa ya mwingine, lakini siku ya
mwisho itakuwa ni faida ya Simba na wao watakumbukwa kwa mchango wao.
Kikubwa ambacho wanachotakiwa kufanya
Simba ni kuwa makini sana katika mikataba watakayoingia (hasa kama watakubali
kumuachia kwa mkopo), ili kweli siku ya mwisho kama atauzwa faida hiyo nusu
iende kwao badala ya kujikuta wanaambulia patupu.
Biashara ya kuuza wachezaji ina faida
na hasara zake, inawezekana Kapombe akabaki Simba na bado siku ya mwisho
asiwape faida yoyote. Hivyo kazi kwenu kutafakari. Huu ni mtazamo wa Saleh Ally.







0 COMMENTS:
Post a Comment