Na Saleh Ally
Kikosi cha Coastal
Union kimeshashuka jijini Dar es Salaam tayari kwa mechi ya leo ya Ligi Kuu
Bara kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na wenyeji wao ni mabingwa wa
Tanzania, Yanga.
Rekodi inaonyesha
hivi, msimu uliopita, Yanga ilianza kushinda ugenini Mkwakwani kwa mabao 2-0,
waliporudiana Taifa, wageni Coastal Union wakagoma na matokeo yakawa ni sare ya
bao 1-1.
Hata kama rekodi ya
msimu uliopita inaweza isiwe dira ya kila kitu lakini inaonyesha kiasi gani
Coastal Union inaweza kupambana na Yanga na mechi ya leo itakuwa ya ushindani
zaidi kwa kuwa Wagosi hao wa Kaya wamebadilisha kikosi chao kwa asilimia 65
huku wachezaji wake wapya wakiwa na uzoefu mkubwa na ligi hiyo.
Haruna Moshi
‘Boban’, Jerry Santo kama atakuwa katika hali nzuri ni wazoefu wa ligi hiyo,
lakini Razack Khalfan, Juma Nyosso pia hawawezi kuwa na hofu ya uzoefu kama
ilivyo kwa Suleiman Kassim ‘Selembe’.
Pamoja na hivyo, kuna
wachezaji wawili wapya wageni mmoja ni Kato Yayo kutoka URA na The Cranes pia
kinda hatari, Crispin Odula aliyetokea Bandari lakini ni mmoja wa nyota wa timu
ya taifa ya Kenya ‘Harambee Stars’.
Mechi inawezekana
kabisa ikabaki kuwa gumzo kwa muda mrefu hasa kama wachezaji wote watapania
kuonyesha soka la uhakika. Kama jazba haitakuwa msingi, basi burudani kuu
zitakuwa ni tatu.
Beki:
Safu ya kila
upande inaonekana ni imara, wenyeji Yanga wana Mbuyu Twite au Kelvin Yondani na
Nadir Haroub ‘Cannavaro’ ambao msimu uliopita walijenga ngome ngumu zaidi ya msimu,
wanaweza wasiwe na hofu sana.
Lakini bado
wanatakiwa kuwa makini sana kwa kuwa wanakutana na washambuliaji wakali wawili,
mfano Odula ambaye ni kinda machachari lakini Yayo ambaye wakati alipokuja
nchini na URA, aliifunga Yanga na Simba, hivyo lolote linawezekana kwake.
Lazima Yanga wawe
makini pia kwa kuwa viungo makini kama Boban, Razack na Selembe wanaweza kuwa
na pasi ‘si za mkaa’ ambazo zitakuwa hatari kwa ngome yao.
Ngome ya Coastal
Union itaongozwa na Juma Nyosso ambaye wakati akiwa Simba, mara nyingi alizuia washambuliaji
hatari kushindwa kuipenya.
Achana na hivyo,
anasaidiana kazi na beki mwingine Marcus Ndeheli ambaye ametokea katika timu ya
jeshi (JKT Oljoro), hivyo ni imara na ana uwezo mkubwa wa kupiga mipira ya
vichwa, sifa yake nyingine ni king’ang’anizi.
Bado makipa wa
timu zote watakuwa burudani pia, kipa wa zamani wa Yanga, Shabani Kado ambaye
anaelezwa yuko katika kiwango kizuri, atataka kuwazuia Jangwani lakini Barthez
lazima aendeleze rekodi nzuri ya kufungwa mabao machache.
Kikubwa ni hivi,
katika mechi ya kwanza, beki ya Coastal haikuruhusu nyavu zao kutikiswa wakati
iliposhinda mabao 2-0 dhidi ya Oljoro wakati Yanga walikubali bao moja
walipoichapa Ashanti 5-1.
Kiungo:
Katika kiungo ni
burudani ya pili, hii inaweza kuwa na mvuto zaidi wakati ‘gozi la ng’ombe’
litakapokuwa linagombewa na viungo mahiri kama Athumani Idd ‘Chuji’ au Frank
Domayo dhidi ya Boban, Salum Telela dhidi ya Razack Khalfan lakini bado Niyonzima
atashuka kusaidia kati kama ilivyo kwa Selembe.
Kwa kuwa ni majani,
vumbi haliwezi kutimka lakini hakika kama timu zote zitaruhusu mpira uchezwe
katikati, basi kutakuwa na burudani ya kutosha.
Uhuru Selemani na
Selembe, bado wanaweza kuwa tatizo kubwa kwa ngome ya Yanga na lazima Juma
Abdul na Luhende wawe makini kulinda ‘mabawa’ yao ili kuepusha madhara na krosi
‘sumu’ kufika langoni mwao.
Hakuna timu yenye
kiungo dhaifu, ingawa kama utachukulia rekodi za mechi moja iliyopita, viungo
wa Yanga watakuwa juu kwa kuwa walizalisha mabao matano wakati Coastal ni mabao
mawili.
Bado Coastal
Union wanaweza kuimarika zaidi katika mechi ya pili na wakazalisha mabao zaidi
pia kuzuia wao kufungwa hata moja kama ilivyokuwa katika mechi iliyopita.
Ushambuliaji:
Utamu uko hapo,
hii ni burudani namba tatu na inawahusisha “wacheka na nyavu”, Coastal
wameshatikisa nyavu mara mbili wakati Yanga wana bao tano.
Kimahesabu kuna
tofauti lakini dakika 90 zinaanza upya na wa nyuma wanaweza kuwa wa mbele. Hakuna
timu inayoweza kwenda uwanjani ikawa na uhakika wa kushinda au kuizuia nyingine
kwa asilimia mia.
Kila upande kuna
wachezaji wenye uwezo wa kubadili matokeo kama wachezaji, yaani bila maelezo ya
kocha. Hii inaongeza utamu wa mechi ya leo na kama mwamuzi atakuwa makini na
wachezaji wakapiga soka, basi burudani itakuwa pomoni.
Matarajio ya
vikosi vya leo Uwanja wa Taifa ni hivi;
YANGA:
Ally Mustapha ‘Barthez’, Juma Abdul, David Luhende, Nadir Haroub
‘Cannavaro’, Kelvin Yondani/Mbuyu Twite, Athuman Idd ‘Chuji’/Frank Domayo, Simon
Msuva, Salum Telela, Jerry Tegete, Didier Kavumbagu na Haruna Niyonzima.
COASTAL UNION:
Shaaban Kado, Hamad
Juma, Abdi Banda, Marcus Ndeheli, Juma Nyosso, Razack Khalfan/Jerry Santo, Uhuru
Selemani, Haruna Moshi, Kato Yayo, Crispian Odula na Suleiman Kassim ‘Selembe’.
0 COMMENTS:
Post a Comment