Na Saleh Ally
Baada ya Cardiff kupanda Ligi Kuu
England, hakuna hata mmoja aliyewahi kutaka kujua kuhusiana nayo, mchezaji
mmoja tu, Craig Bellamy, ndiye angeweza kuzungumziwa.
Bellamy amekipiga Liverpool na Man City,
kazi yake inajulikana, lakini wengine hawakuwa na umaarufu kiasi hicho katika
uso wa dunia ya soka.
Lakini kwa eneo inapotokea timu hiyo,
usithubutu, hawajali wala kufuatilia sana kuhusiana na timu nyingine kama Man
United , Arsenal au Real Madrid. Namba moja ni timu yao.
Mashabiki wasiokata tamaa wa timu hiyo,
wanaamini timu yao ndiyo bora zaidi ya nyingine, sema haijapata nafasi ya
kucheza madaraja ya juu, hivyo kwao wanajitosheleza.
Inawezekana ushindi wao wa mabao 3-2
utawaongezea mashabiki zaidi na kuwafumbua macho wengi kutaka kujua. Ni timu
yenye mambo mengi ambayo shabiki Mtanzania wa soka aliyeshangazwa na ushindi
wao huo dhidi ya City angependa kujua.
Wanaitwa ‘Roho ya paka’, katika maisha
yao, suala la kukata tamaa halipo hata kidogo na wanataka kutimiza ndoto bila
ya kujali wapi walikosea. Wana mengi ambayo unaweza kuyajua.
MMILIKI MATATIZONI:
Mmiliki mpya wa Cardiff, raia wa
Malaysia, Vincent Tan, aliingia katika mgogoro mkubwa na mashabiki wa klabu
hiyo mara baada ya kuamua kubadili rangi ya jezi kutoka bluu hadi nyekundu.
Lakini pia katika nembo alimuondoa ndege
wa blue na kumweka dragon, lakini mmiliki huyo alishikilia msimamo wake na sasa
wako mashabiki wanaamini ndege na rangi ya blue ilikuwa mkosi au kutokuwa na
bahati kwao maana siku chache baada ya kuibadili wamepanda hadi Ligi Kuu
England.
KIM BO:
Mkorea Kim Bo-Kyung aliweka rekodi ya
aina yake na kuonyesha mapenzi yasiyokuwa na mfano kwa timu hiyo. Pamoja na
kwamba iko daraja la kwanza lakini aliamua kukataa kujiunga na timu kubwa kama
Celtic na Borussia Dortmund.
Alitokea Cerezo Osaka ya Japan, akatua
Cardiff na kuonyesha uwezo mkubwa hadi alipoisaidia kupanda hadi Ligi Kuu
England.
Sasa ni kati ya wachezaji wenye furaha
na ameonyesha kwamba katika maisha si lazima kukimbilia vinavyong’ara tu,
badala yake unaweza kutengeneza chako kikawa bora.
NAHODHA HASA:
Nahodha wa timu hiyo kwa sasa ni
Bellamy, lakini nahodha mwenyewe hasa ni Mark Hudson ambaye amelazimika
kustaafu soka katika hatua za mwisho kabisa.
Hudson aliyeichezea mechi 31 za Ligi
Daraja la Kwanza kabla ya kuumia na kulazimika kuachana na soka, bado amekuwa
akishirikiana kwa karibu kabisa na kikosi hicho.
Ingawa majukumu ya unahodha amekabidhiwa
Bellamy, beki huyo wa zamani wa Crystal
Palace na Charlton, kila mechi ya timu hiyo amekuwa akiingia katika vyumba vya
kubadilishia nguo kutoa maoni yake alivyouona mchezo, kama alivyofanya dhidi ya
Man City na kikosi chake kuibuka na ushindi wa mabao 3-2.
AYATOLLAH KHOMEINI:
Inaweza ikawashangaza wengi hasa kwa
timu kutokea Ulaya, kwani mashabiki wa Cardiff wanavutiwa zaidi na uimara na
historia ya maisha ya kiongozi wa Kiislam wa zamani wa Iran, Ayatollah
Khomeini.
Walianza kuonyesha hisia zao kwake
wakati wa mazishi yake mwaka 1989, na tokea hapo wamekuwa wakishangilia katika
mfumo wa kuonyesha kumuunga mkono au kuunga mkono utamaduni wa Iran.
Mashabiki wa timu hiyo wameonyesha kiasi
gani hawajali kuonekana ni watu tofauti na mara nyingi wamekuwa wakisisitiza
kwamba timu nyingi zimechagua mashujaa wao, nao pia wana haki. Mfano Wes Brom
‘wanamzimikia’ Lincoln, Man City kipenzi chao ni Dam Buster, nao wamemchagua Khomeini.
CAMPBELL:
Mshambuliaji wao nyota, Frazier Campbell,
anaaminika ndiye atakuwa hatari zaidi kwa msimu huu katika Ligi Kuu England kwa
kuwa si mgeni tena katika ligi hiyo ngumu.
Campbell aliwahi kuzichezea timu kubwa
za Ligi Kuu England kama Manchester United, Hull City, Spurs na Sunderland.
Ingawa mshambuliaji huyo mwenye miaka 25 hakupata nafasi ya kutosha sasa ni
moto wa kuotea mbali, kwani ameuonyesha pia katika mechi dhidi ya Man City kwa
kufunga mabao mawili.
Alionyesha ni hatari zaidi akiwa na
Cardiff baada ya kufunga mabao sita katika mechi 11 za Ligi Daraja la Kwanza,
lakini akasababisha faulo nyingi zaidi kuliko mchezaji mwingine katika ligi
hiyo.
ROHO YA PAKA:
Kikosi cha timu hiyo kinaaminika kwa
kuwa na roho ya paka, kwani mara ya mwisho kucheza Ligi Kuu England ilikuwa ni
mwaka 1957, lakini miaka yote wamekuwa wakielezea nia ya kupanda na
waliposhindwa, msimu uliofuata walianza upya.
Kama hiyo haitoshi kwa miaka kumi
mfululizo wamekuwa kati ya timu zinazokosa kidogo tu kupanda daraja na bado
wakapambana kushinda kila mechi.
Bado walionyesha wao ni roho ya paka
kweli baada ya kupoteza zaidi ya fainali mbili za Kombe la FA, lakini
wameendelea kuahidi siku moja watakuwa mabingwa.
Wachezaji, viongozi na hata mashabiki wa
timu hiyo wanaamini ndiyo watu wasiokata tamaa hata kidogo katika mchezo wa
soka kwa nchi za Uingereza.
WAO, SWANSEA:
Wapinzani wao namba moja ni Swansea, wakikutana
basi Wales inasubiri kila kitu hadi watakapocheza kwa kuwa hata vile vikundi
vya watukutu navyo hufanya mazoezi kujiandaa na mechi hiyo.
Jeshi la polisi huandaa vikosi maalum na
wakati mwingine hulazimika kuomba msaada kutoka England ili kuhakikisha kila
kitu kinakwenda vizuri.
Mwaka 1988 ilielezwa mashabiki 30 wa
Cardiff walizamishwa mtoni na wengine kuuwawa wakati wanakimbizwa na watukutu
wa Swansea. Wakati huo walikuwa wanatumia Uwanja wa Vetch Field ambao uko
jirani na mto.
FIN.
0 COMMENTS:
Post a Comment