August 7, 2013



  OKWI AKIITUMIKIA ETOILE DU SAHEL (PICHA: ESS, RUHUSA KWA SALEHJEMBE BLOG)
Na Wilbert Molandi
KLABU ya Simba imeiambia Al-Markhiya Sports Club ya Qatar imalizane na Etoile du Sahel ya Tunisia ili imsajili kiungo wake mshambuliaji, Emmanuel Okwi.
Kauli hiyo imetolewa saa chache baada ya klabu ya Al Markhiya Sports Club iliyomnunua kiungo mshambuliaji wa Simba, Mwinyi Kazimoto, kuonyesha nia ya kumsajili kiungo huyo mwenye kasi.
Akizungumza na Championi Jumatano, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya timu hiyo, Zakaria Hans Pope, alisema kuwa kama klabu hiyo ipo tayari kutoa dola 300,000 (zaidi ya shilingi milioni 480) izipeleke Etoile du Sahel ili imchukue Okwi.
Hans Pope alisema, Etoile du Sahel hawana shida, hivyo wawafuate kwa ajili ya kufanya mazungumzo, kwani bado ni mchezaji mzuri mwenye uwezo mkubwa wa kucheza soka.
“Sisi tunasubiri fedha zetu za usajili kutoka huko Etoile du Sahel tulizomuuzia Okwi, hatuwezi kuingilia mazungumzo, nyie kama mnamtaka wafuateni mkafanye nao mazungumzo.
“Kikubwa mnatakiwa kujua kuwa dau lake la usajili ni dola 300,000, zipelekeni Etoile du Sahel ili mumchukue,” alisema Hans Pope.
Naye mwakilishi wa Al-Markhiya Sports Club, Saleh Afif, alisema: “Tunataka kuiimarisha timu yetu ili ipande daraja kwenye msimu ujao, tunaamini tukimpata Okwi malengo yetu yatafanikiwa.
“Acha tukajadiliane kwanza na viongozi kabla ya kwenda kufanya mazungumzo na Etoile du Sahel,” alisema Afif.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic