
Na Joan Lema
KOCHA Mkuu
wa Yanga, Ernie Brandts, amewaonya vikali wachezaji wa klabu hiyo, Hussein Javu
na Rajabu Zahir kwa kuchelewa kufika kwenye maandalizi ya timu hiyo kabla ya
mechi ya Mtibwa Sugar wikiendi iliyopita.
Chanzo
makini kutoka ndani ya klabu hiyo kilisema kuwa, mara baada ya kumalizika kwa
mechi hiyo iliyopigwa Uwanja wa Taifa na Yanga kuibuka kidedea kwa ushindi wa
mabao 3-1, Brandts aliwajia juu wachezaji hao kwa kuchelewa.
Kikizungumza
na Championi Jumatano, chanzo cha ndani kutoka Yanga kilisema wachezaji hao walionyesha
utovu wa nidhamu kwenye kikao cha kabla ya mechi kilichofanyika kwenye makao
makuu ya klabu hiyo Jangwani jijini Dar es Salaam.
Chanzo hicho
kilisema kuwa wachezaji hao walikuwa kwenye kikosi cha kwanza kwenye mchezo huo
dhidi ya Mtibwa, lakini kutokana na kuchelewa huko, Brandts aliwaondoa na
kuwafanya wachezaji wa akiba.
“Kocha alisisitiza kuwa hatataka jambo hilo
kujirudia tena, kwani hapendezwi na utovu wa nidhamu wa aina yoyote.
“Kocha
alikuwa awaanzishe lakini hali hiyo ilisababisha awatoe kwenye kikosi cha
kwanza, hili ni onyo, nafikiri wakirudia tena watakumbwa na adhabu kali,”
kilisema chanzo hicho.







0 COMMENTS:
Post a Comment